Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Wednesday, October 1, 2014

Uchambuzi wa Kitabu: GOOD MUSLIM, BAD MUSLIM: America, the Cold War, and the Roots of Terror.

GOOD MUSLIM, BAD MUSLIM: America, the Cold War, and the Roots of Terror.
 
Na Ado .S. Ado
Prof. Mahmood Mamdani


Mahmood Mamdani ni mwanazuoni galacha kwenye fani ya Sayansi ya Siasa na Anthropojia. Kuanzia nyumbani kwake Uganda mpaka nchi nyingine za Afrika na Marekani anakofundisha, Mamdani amejizolea sifa kemkem miongoni mwa wana-akademia. Ni kutokana na umahiri huo, haikushangaza pale kitabu chake, ‘’Citizen and Subject: Contemporary Africa and the Legacy of Late Colonialism’’ kilipotunukiwa tuzo ya kitabu bora kwa lugha ya kiingereza mwaka 1996 (African Studies Association (USA)‘s Herskovitz Prize) na kujumuishwa kwenye orodha ya vitabu bora vya kiafrika vya karne ya ishirini ya taasisi ya maonesho ya vitabu ya Zimbabwe. Mwaka 2008, Mamdani alishika nafasi ya tisa kwenye orodha ya Jarida la Prospects (Uingereza) ya wanazuoni miamoja mashuhuri wa mwaka huo.

Mahmood Mamdani ameandika vitabu, makala na maandiko mengi kwenye nyanja anuai kiasi kwamba linapokuja suala la mjadala wa kisomi kwenye masuala ya machafuko ya kisiasa, siasa na utamaduni, ugaidi, na ukoloni barani Afrika, vitabu vyake ni rejea ya kutumainiwa.

Baadhi ya vitabu vyake maarufu ni pamoja na ‘’When Victims Become Killers: Colonialism’, ‘Nativism, and the Genocide in Rwanda’’, ‘‘From Citizen to Refugee: Politics and Class formation in Uganda’’ na ‘‘Saviors and Survivors: Darfur, Politics and the war on Terror’’.

Binafsi, nilianza kuuonja ufundi wa kalamu ya Profesa Mamdani mwaka 2010 nilipokisoma kitabu chake, Good Muslim, Bad Muslim: America, the Cold War and the Roots of Terror, ambacho bingwa wa sarufi Noam Chomsky amekielezea kama “kazi ya kiudadisi inayoibua maswali ya msingi na kukuza uelewa wetu kuhusu matukio makubwa ya ulimwengu wa leo”.

Ni muhimu nikiri wazi kwamba, licha ya kuwepo kwa msemo wa kutokihukumu kitabu kwa jalada lake, mimi nilishawishika kukinunua kitabu hicho mara tu baada ya kukiona kwa mara ya kwanza kwenye kongamano lililoandaliwa na taasisi ya Kigoda cha Mwalimu Nyerere katika Umajumui wa Afrika pale chuo Kikuu cha Dar es salaam. Jina la kitabu lilinifikirisha sana: “Mwislamu mzuri na mwislamu mbaya?” Nilijiuliza peke yangu.

Kitendawili changu kilitanzuliwa baada ya kukisoma. “Good Muslim, Bad Muslim’’ ni kitabu kinachopambanua kinaganaga kuhusu asili ya ugaidi ulimwenguni hasa kuanzia katika karne ya ishirini. Mjadala kuhusu kiini cha ugaidi duniani umejikita katika hoja kuu mbili; mosi, dini, hasa uislamu na pili, siasa.

Katika kitabu chake chenye utangulizi, sura nne na hitimisho, Profesa Mamdani anajenga hoja kwamba ugaidi tunauona leo ulimwenguni, kwa sehemu kubwa, una mahusiano ya moja kwa moja na masuala ya kisiasa hasa wakati wa vita baridi kuliko hoja za msukumo wa kidini au utamaduni.

Jina la kitabu, Good Muslim, Bad Muslim, linaakisi fikra mpya kuhusu Uislamu na ugaidi iliyomea miongoni mwa Wamarekani na ulimwengu kwa ujumla baada ya tukio la kushambuliwa kwa majengo ya World Trading Centre (WTC) na Pentagon almaarufu kama ‘Septemba 11’ .

Mwandishi anachambua jinsi mstari ulivyochorwa baina ya waislamu baada ya kulipuliwa kwa majengo hayo. Akitangaza kuzinduliwa kwa vita dhidi ya ugaidi baada ya tukio la Septemba 11, rais George Bush wa Marekani aliweka wazi umuhimu wa kuchora mpaka baina ya “waislamu wazuri’’ na “waislamu wabaya’’.
Kwa mujibu wa mtizamo huu wa rais Bush, “waislamu wabaya’’ ndiyo wanaopaswa kuwajibika kwa matukio mengi ya kifedhuli ya ugaidi duniani wakati “waislamu wazuri’’ ni wale inaowaita kuwa waliostaarabika, waso na shari na, bila shaka, wanaowaunga mkono wamarekani. Kwa mtazamo wa rais Bush, hawa hawastahili kuguswa na vita dhidi ya ugaidi.

Baada ya kujadili kwa kirefu kuhusu kumea na kukomaa kwa vikundi vya msimamo mkali duniani (fundamentalists) tangu neno hilo lilipoasisiwa mwaka 1920 na mchungaji Curtis Lee Lewis huko marekani na kudurusu kwa kina jinsi makundi mbalimbali yanayoitwa ya kigaidi yalivyochomoza, mwandishi anahitimisha kwa mtazamo kwamba kihistoria, Marekani yenyewe inapaswa kulaumiwa kwa kuzaliwa kwa wale inaowaita “waislamu wabaya’’ na kukua kwa ugaidi kutokana na yenyewe kusimamia kwa uthabiti uundwaji na kuvilea vikundi vingi vya kigaidi vya kimamluki (Proxy) hasa wakati wa vita baridi. Kwa lugha nyepesi, Profesa Mamdani anamaanisha Marekani inavuna ilichokipanda.

Katika makala haya, tutachambua, japo kwa ufupi, maeneo mbalimbali ambayo profesa Mamdani ameyatolea mfano kama uthibitisho wa hoja yake kuhusu ushiriki wa marekani katika kulea magenge ya kigaidi, madikteta na waasi.

1. AFRIKA

Profesa Mamdani anaanza kwa kuituhumu Marekani kushirikiana na mamluki Mobutu Sese Seko kumuua kikatili aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Patrice Emery Lumumba
(2 Julai 1925 – 17 Januari 1961) baada ya jaribio la awali la CIA kumuua kwa kemikali iliyotengenezwa kwa sumu ya kobra kufeli. Dhambi ya Lumumba ilikuwa kushirikiana na Sovieti (USSR) na hivyo basi utawala wa rais Dwight D. Eisenhower wa Marekani kumbatiza kuwa “Castro wa Afrika’’ anayestahili kung’olewa.

Baada ya mauaji ya Lumumba, Marekani ilitumia gharama kubwa kuhakikisha dikteta Mobutu anasalia madarakani. Hata pale wananchi wa Kwilu (1963), na Kivu (1964) walipoanzisha vuguvugu la kumng’oa dikteta Mobutu, mwandishi anatujuza, ni wamarekani kupitia CIA walioandaa genge la askari mamluki kuzima vuguvugu ambao pamoja na mambo mengine, walivamia vijiji, kupora mali, kunyonga mateka kikatili na kufanya vitendo vingine vya kimumiami.

Pia, Profesa Mamdani anaelezea kwa kina jinsi Marekani ilivyounga mkono na kuvisaidia kwa hali na mali vikundi vya waasi nchini Angola kama vile the Front for National Liberation of Angola (FNLA) na the Union of Total Liberation of Angola(UNITA) ili kudhibiti chama cha kupigania uhuru cha MPLA kilichoungwa mkono na Cuba. Msaada kama huo pia ulitolewa kwa RENAMO cha Msumbiji ili kuidhibiti FRELIMO. Pia, chama cha wazalendo cha ANC cha Afrika kusini kiliingizwa kwenye orodha ya wamarekani ya vikundi vya kigaidi.

2.AMERIKA YA KATI

Baada ya mapinduzi ya Nicaragua ya mwaka 1979, Marekani ilishirikiana na magenge ya waasi ya Counterrevolutionaries almaarufu kama Contras chini ya dikteta wa zamani Anastasio ("Tachito") Somoza DeBayle

Baada ya baraza la Congress kupitisha sheria (the Borand Amendment, 1984) kuzuia misaada ya kipesa na kijeshi kwa waasi wa Nicaragua, profesa Mamdani anatujuza, serikali ya rais Ronald Reagan iliruhusu kwa siri mtandao wa biashara ya madawa ya kulevya kama ilivyofanya Vietnam ili kukuza kipato kwa waasi.

Licha ya ukweli kwamba Nicaragua haikuzalisha coca, malighafi muhimu katika uzalishaji wa cocaine, CIA ilikuwa muhimu katika uwezeshaji wa uzalishaji wa madawa hayo toka Columbia na kusafirishwa toka Amerika ya kati kwenda sehemu mbalimbali duniani. Ili kufanikisha hili, ilibidi kushirikiana na magenge ya ki-mafia. Haikushangaza hivyobasi mwaka 1988, Jorge Luis Ochoa Vásquez na Pablo Emilio Escobar Gavíria, viongozi wa kimafia wa mtandao wa madawa ya kulevya walivyoingizwa kwenye orodha ya jarida la Forbes ya watu wenye utajiri zaidi duniani.

3. MASHARIKI YA KATI.

Uchambuzi kuhusu kumea kwa ugaidi mashariki ya kati ndiyo kiini cha kitabu chenyewe. Mwandishi anajenga hoja kwamba kabla ya vita ya kuung’oa utawala wa kisovieti nchini Afghanstan, historia ya uislamu haikushuhudia matukio ya kigaidi katika karne ya ishirini. Hivyo basi, kuchipua kwa matukio ya kigaidi katika miongo mitatu iliyopita ni zao la ‘uhandisi’ wa Marekani kuanzia vita vya Afghanstan vya mwaka 1979.

Ili kuiondosha serikali ya Afghanstan iliyopigwa jeki na Sovieti, Marekani ilikuwa tayari kutumia gharama yeyote ikiwemo umwagaji damu. Kwa kushirikiana na shirika la kijasusi la Pakistan-ISI (Inter-Services Intelligence) mwandishi anadai, Marekani iliandaa makundi ya wapiganaji wa Mujahadin, waliokusanywa nchi mbalimbali na kuwapa mafunzo ya kijeshi, utaalamu wa kutengeneza milipuko na misaada ya kipesa ili kufanikisha kufurushwa kwa Sovieti nchini Afghanstan.

Madai haya ya Mamdani yanaungwa mkono na ukweli kwamba wapiganaji wa Mujahadin, ambao walikuja kuwa mwiba kwa marekani baadaye, walikaribishwa hadi ikulu ya Marekani na kupongezwa kwa kufanya Jihad ya kujenga demokrasia. Mwandishi anaipiga kijembe Jihad hii na kutujuza kuwa ilikuwa Jihad ya Wamarekani.

Kinachoweza kumduwaza msomaji ni pale majina makubwa kama Sheikh Azzam na Osama bin Laden yanapotajwa kwamba yameletwa kwenye ramani ya ugaidi na CIA. Ipo pia simulizi ya kusisimua ya jinsi mhandisi Osama bin Laden alivyopewa zabuni na Wamarekani ya kujenga miundombinu ya kivita ya milimani ambayo baada ya vita ya kuing’oa Sovieti, ilitumika kupambana na Marekani na washirika wake!

Kwa vipi marafiki (Marekani na vikundi vya Jihad ilivyovianzisha na kuvilea) wakageuka maadui mithili ya paka na panya? Mwandishi anatujuza kuhusu tofauti ya fikra baina ya Marekani na vikundi vya kipiganaji hivi.

Baada ya kumalizika kwa vita vya Afghanstan, vikundi hivyo vilidhamiria kutumia stratejia zilezile kuzindosha dola nyingine kama Saudi Arabia, kipenzi cha Marekani. Marekani ilishindwa kuvidhibiti vikundi vya Mujahadin vilivyokusanywa toka nchi mbalimbali ili kumng’oa Mrusi Afghanstan na sasa, anadai mwandishi, vimesambaa dunia nzima vikipambana na Marekani na Washirika wake.

Pia mwandishi amechambua kwa kina jinsi Saddam Husein, swahibu wa zamani wa Marekani kwenye vita vya Iraq na Iran, alivyolipa gharama ya kwenda kinyume na matakwa ya Marekani na kuthibitisha usemi maarufu ulionenwa na Condoleza Rice kwamba Marekani haina maadui wa kudumu (na wala haina marafiki wa kudumu bali ina maslahi ya kudumu). Yapo pia maelezo ya kina kuhusu chimbuko la mgogoro wa Israel na Palestina.

Swali la kujiuliza ni kama kitabu cha Profesa Mamdani, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia (Marekani) aliyewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, UDSM kati ya mwaka 1973-1979, kinaakisi mazingira ya ulimwengu wa leo.

Akiandika kuhusu chimbuko la Boko Haram, Profesa Wole Soyinka, mwanazuoni wa kinaijeria, anajenga hoja kwamba hata kikundi hicho, kimejivika mwamvuli bandia wa dini huku kikiwa na malengo ya kisiasa (rejea makala yake kwenye jarida la kielektroniki la “Pambazuka’’ yenye kichwa cha habari “The Next Phase of Boko Haram Terrorism”).

Katika kuhitimisha, hebu nifuate ushauri wa mwalimu wangu, profesa Paramagamba Kabudi, aliyetufunda kupenda kufanya uchambuzi unaojikita katika uhakiki wa sura zote za jambo (critique) badala ya kujikita kwenye ukosoaji peke yake.

Kwanza, Kwa maoni yangu, licha ya kujenga hoja egemezi kuhusu uislamu, ugaidi na sera za nje za Marekani, profesa Mamdani ametanua mno mawanda ya kitabu chake kwa kugusa kila madhila yaliyofanywa na marekani kila pembe ya dunia na kuhama kwenye dhima yake kuu.

Pilli, licha ya kitabu kugusa sehemu kubwa ya vita baridi, Profesa amejikita zaidi kwenye maovu ya Marekani na kutozungumza hata punje ya madhila yaliyoletwa na Sovieti. Pia, mjadala wake, licha ya kuthibitishwa na utafiti wa kina na kila namna ya ushahidi, umejibinya kwenye chanzo kimoja tu cha kuenea kwa ugaidi na kujenga picha ya Marekani pekee kuwa chanzo cha ugaidi.

Kwa watu wenye mahaba na sera ya mambo ya kigeni ya Marekani, Profesa Mamdani anaweza kutazamwa kama mtu aliyedhamiria na kufanikiwa kuitwisha marekani peke yake zigo lote la ugaidi.

Hayo ndiyo machache niliyoyaona. Pengine Wanaantropojia, Wataalamu wa sayansi ya siasa na wale wa mahusiano ya kimataifa wanaweza kuona mengi zaidi. Licha ya hayo, kama alivyosema JM Coetzee mwanafasihi nguli wa Australia aliyejinyakulia tuzo ya Nobel ya fasihi (2003), “Good Muslim, Bad Muslim” ni kitabu “kinachofunua wazi uzushi, ghalati na mitazamo ya jumlajumla” iliyojaa kwenye sera ya mambo ya kigeni ya Marekani.


Maoni Kwa Mwandishi, Simu: 0653619906 Baruapepe: adoado75@hotmail.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda