·
Asilimia
95 ya waathirika ni wanaume
·
Asilimia
50 ya wanaopata matibabu hurudia matumizi ya mihadarati
·
Manyara
na Arusha mirungi inatumika hadharani
Na Dinah Christian.
Kutokana na utafiti uliofanywa
katika Hospitali ya Kilutheri ya Haydom katika kitengo cha kuwahudumia
waathirika wa dawa za kulevya na pombe maarufu kama Amani Ward, asilimia 90 ya waathirika wa dawa za kulevya na pombe ni
vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 40.
Kwa
mujibu wa muuguzi msaidizi anayefanya kazi katika kitengo hicho, Naomi Marissa,
matumizi ya dawa hizo zinaongezeka pamoja na kuwapo kwa vituo mbalimbali
vinavyotoa elimu na kuongeza kuwa hali hiyo ni kutokana na jamii kutokufanya
uhamasishaji juu ya elimu inayotolewa.
Takwimu
zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2011 hadi mwaka 2013 wagonjwa 171 walipokelewa
katika kitengo hicho ambapo wanaume walikuwa 162 na wanawake 9 ambao ni
asilimia 5 tu ya waathirika ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 95
Hata
hivyo utafiti unaonesha kuwa 45% hadi 50% (takriban nusu) ya wagonjwa waliopata
matibabu hurudia matumizi ya dawa hizo, hali inayoelezwa kuwa inatokana na
wagonjwa wengi kutokumaliza matibabu yao baada ya kuona kuwa wameanza kupata
ahueni na hivyo kurudi katika utumiaji wa mihadarati.
Pamoja
na kitengo hicho kutoa matibabu hayo kwa gharama nafuu lakini bado jamii
inauelewa mdogo kuhusu madhara na namna ya kukabiliana na matumizi ya pombe na
mihadarati na wagonjwa wenyewe kutohudhuria katika mafunzo na vikao vitolewavyo
kwa waathirika wa dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kuogopa gharama za
matibabu.
Aidha,
takwimu zaidi zinatanabaisha kuwa, waathirika wengi wa mihadarati na pombe
waliopata matibabu katika hospitali hiyo kubwa zaidi katika mkoa wa Manyara,
wanatokea katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam huku mikoa ya
Tabora, Mwanza na Manyara ikiwa na idadi ndogo zaidi ya waathirika wa dawa
hizo.
Pamoja
na mkoa wa Manyara kuwa na idadi ndogo ya watumiaji wa dawa hizo, lakini
uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, mihadarati aina ya mirungi inatumika
sana na kwa wazi katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Manyara na Arusha. Watumiaji
wakubwa wa mirungi ni mawakala wa mabasi, madereva wa magari ya mizigo,
madereva wa bodaboda na waongoza watalii
Katika
miaka hivi karibuni, Tanzania imejizolea sifa mbaya zaidi kuwahi kuwakumba
wananchi wake wanaosafiri nje ya nchi baada ya Watanzania wengi kukamatwa
sehemu mbalimbali duniani wakisafirisha mihadarati.
Wengi
wa waliokamatwa ni vijana hasa wasanii huku ikisemekana kuwa wimbi la vijana
kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya linazidi kuongezeka kila kukicha.
Aidha, uchunguzi wa Mbiu ya Jamii umebaini kuwa vijana wengi hujiingiza katika
matumizi ya mihadarati kwa kufuata mkumbo na kupenda kuiga na kujaribu kila
kitu wanachokiona, tamaa ya utajiri wa haraka na umaskini uliopindukia.
Wakati
wanaharakati mbalimbali, mashirika ya dini na yasiyo ya kiserikali yakipiga
kelele ili serikali idhibiti matumizi na usafirishaji wa dawa hizi, bado dawa
hizi zipo kila mahali huku ikidaiwa kuwa vigogo ndio wanaoendesha biashara hii
wakiwatumia vijana.
No comments:
Post a Comment