Miaka 14 imepita toka
Taifa letu lipate msiba mkubwa wa
kutokwa na kiongozi aliyependwa na watu wengi ndani na nje ya nchi yetu. Ilikuwa
ni Alhamisi ya tarehe 14 mwezi Oktoba 1999, aliyekuwa rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa alipoutangazia umma wa Watanzania
juu ya msiba huo, ambao uliacha majonzi makubwa sana nchini.
Nyimbo ziliimbwa na
maombolezo ya siku 30 yalitangazwa nchi nzima na siku 7 za mapumziko, ili
kumuenzi kiongozi aliyekuwa siyo tu alama ya Utaifa wetu, bali pia alikuwa
nguzo na tegemeo la bara zima la Afrika.
Miaka 14 baada ya
Alhamisi ile iliyojaa majonzi, nchi yetu imesonga mbele bila uwepo wa Mwalimu.
Mwalimu hayupo nasi bali falsafa zake zingali hai pamoja nasi, kama wengine waliotutoka
walituachia pengo, mwalimu alituachia ubogoyo kabisa.
Wakati tunaadhimisha
miaka 14 toka Baba wa Taifa atutoke, ni vizuri tukatambua kuwa kimsingi
hatuadhimishi kifo chake bali tunaenzi zawadi ya maisha yake. Hakuna namna
nzuri na bora zaidi ya kumuenzi Mwalimu zaidi ya kumuenzi kwa vitendo hasa
falsafa zake ambazo zililenga kujenga haki na usawa baina ya binadamu wote. "Binadamu
wote ni ndugu zangu, na Afrika ni moja"
"Katika kipindi
cha uhai wake, mwalimu alikemea rushwa na kila aina ya uonevu, mwalimu alijenga
umoja wa kitaifa na kutufanya Watanzania wote kuwa kama ndugu japokuwa
tunaasili na tamaduni tofauti zinazoundwa na makabila zaidi ya 120."
Leo hii, yale aliyokuwa akipigania Mwalimu
tumeyasahau, badala yake nchi yetu inaanza kukumbwa na matukio ya Udini na
Ukabila huku kukiwa na matabaka baina ya Watanzania, maskini na matajiri.
Mwalimu alitekeleza
sera na falsafa zake kwa vitendo, mwalimu hakujilimbikizia mali kama viongozi
wetu wa sasa na mwalimu hakupeleka watoto wake wakasome nje kama wanavyofanya
viongozi wetu sasa. Mungu alitupa zawadi kubwa sana Watanzania kuwa na mtu kama
Mwalimu ambaye hutokea pengine mara moja katika karne nzima katika dunia nzima,
lakini hatujaitendea haki zawadi hii na kuienzi badala yake, tunamsifu tu
midomoni wakati matendo yetu yapo kinyume kabisa na tunayoyahubiri majukwaani.
Mwalimu hakuwa mfano wa
kuigwa barani Afrika pekee, bali dunia kwa ujumla na ameingia kati ya viongozi
mashuhuri zaidi duniani katika karne ya 20 akiwa katika kundi moja na akina
Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchill, Mao na Fidel Castro japo Tanzania
ilikuwa nchi changa na moja ya nchi maskini zaidi duniani. Aliheshimika duniani
kote hasa wanazuoni wa ndani na nje ya Afrika na kwa kuutambua mchango wake, na
misimamo yake iliijengea heshima nchi yetu. Ukisema wewe ni Mtanzania,
uliheshimika.
Lakini sasa,
hatuheshimiki tena, tumekuwa nchi ya kudharaulika sana siyo tu na mataifa
makubwa bali hata na majirani zetu, vijana wetu wamekuwa makontena ya kubeba
madawa ya kulevya na nchi yetu imegeuzwa "dampo" la bidhaa feki baada
ya kuviua viwanda ambavyo Mwalimu alivianzisha ili kutoa ajira kwa vijana wetu
na kuzalisha bidhaa bora nchini. Sasa tunaagiza hadi "toothpick"
kutoka China. Tunauza magogo kisha tunanunua samani zinazotengenezwa na vumbi
la mbao kutoka nje.
Tumewapa
"wageni" migodi yetu na ardhi yetu, tunasafirisha wanyama kuwapeleka
nje ya nchi, tunaua tembo ili kuuza meno na mbaya zaidi rushwa na udini
vimekuwa kawaida. Kama tunadai kumwadhimisha Mwalimu na maisha yake, tufanye
hivyo kwa vitendo na si maneno matupu. Badala ya kuendelea kuomboleza na kuimba
nyimbo za "Kama Nyerere angekuwepo" na "Kama siyo juhudi zako
Nyerere", tufanye kwa vitendo ili Mwalimu aendelee kuishi nasi katika
matendo yetu. Wahenga walinena, "Ada ya mja hunena, kwa muungwana ni
Vitendo"
No comments:
Post a Comment