Muhimu: Orodha ya
wanafunzi wanaodaiwa karo ya chuo mwaka 2012/2013.
“KUMB:
kama mwanafunzi atashindwa au kuchelewa kulipa kabla ya tarehe iliyopangwa,
itamlazimu kulipia asilimia 10 zaidi au kusitishwa kuendelea na masomo yake.
malalamiko yote yafikishwe kwa mkuu wa taaluma mapema iwezekanavyo”.
|
Hivyo
ndivyo lilivyosomeka tangazo kubwa kwenye mbao zote za matangazo zilizopo chuoni
kwetu ilikuhakikisha kuwa wahusika wanaliona kwa urahisi na wanachukua hatua zinazotakiwa kwa haraka.
Nikisema ni kwa bahati mbaya kuliona tangazo hilo nitakua ninakosea kwani asubuhi na mapema,
wakati niko njiani kuingia darasani hilo ndilo tangazo la kwanza na pekee kukutana na macho yangu.
Na ukweli ni kwamba sio kuwa nilikua sifahamu
kuwa ninadaiwa ADA, la hasha! ila kwa kweli mara tu nilipoliona tena hilo
TANGAZO mwili wangu ulikosa nguvu na
kuanza kutoa kijasho chembamba.
Moyo wangu ulishtuka sana mithili ya mtu aliyepata
habari za ghafla. Hamu ya kuingia darasani iliisha ghafla na mawazo chungu nzima yakaanza kutembea
kupishana kwenye ofisi za kichwa changu.
Nilihakiki tena jina langu ili kujiridhisha nikagundua ni la kwangu kweli na
lilikuwa limeeshikialia nambari tatu
kati ya wadaiwa sugu kumi tu kwa wanafunzi takribani 200 wa darasa la
mwaka wa pili; baada ya macho yangu kuridhika niliahirisha kuingia darasani,
nikaamua kurudi zangu nyumbani ninakoishi ili kutafuta ni jinsi gani naweza kupata hela ya kulipia ada.
Najua
wengi mtauliza, Je! huna wazazi au
ndugu na jamaa wa kukulipia? Jibu sahihi
ni kwamba wazazi wangu wote wako hai na Baba yangu ni mtangazaji maarufu sana
hapa TANZANIA na hata nikitaja jina lake utagundua kuwa si kweli kuwa BABA yangu hana uwezo wa kutoa msaada
wowote katika maisha yangu.
Sikuwahi
kuishi na BABA na MAMA yangu hata siku moja tangu nimezaliwa, Baba na Mama
walikutana kwenye starehe wakiwa vijana na huo ndio mwanzo wa mimi kupatikana
lakini kipindi mama anajifungua Baba ALIMTELEKEZA na kutuacha tukiwa hatujui
pa kuanzia.
Kipindi
hicho mama yangu alikua mwanafunzi, kitendo cha yeye kupata ujauzito akiwa
shuleni kilimtenganisha na wazazi wake , ndugu ,jamaa na hata marafiki, alibaki
kuwa jeshi la mtu mmoja na kusukuma maisha yake yeye kama yeye.
Nimekulia
mikononi mwa mama yangu ambaye ana fanya kila awezalo mimi niweze kuishi hata
kwa kubangaiza. Waswahili wana msemo usemao, “uchungu wa mwana ajuaye ni mzazi” ila mimi naomba nirekebishe kidogo, “uchungu wa mwana ajuae ni mama asikuambie
mtu”.
Mama ndio kila kitu kwangu, moyo
wake wa huruma uliombatana na uchungu alioupata kutokana na kutelekezwa na
mwanaume asiyejua anachokifanya unamfanya afanye kila awezalo kunitunza na
kunitengenezea maisha mazuri “huku akiniusia kuwa na moyo wa utu na kutokuwatendea vibaya watu wengine,kila mara
nazikumbuka kauli za mama na zimenipa nidhamu kubwa katika miasha yangu. tangu
nikiwa sekondari nilimuahidi kuwa nitakuwa mtii na muangalifu na nikipata kazi
yeye atapumzika na nitaanza kumtunza mpaka mwisho wa maisha yangu, lakini
sitamsamehe baba yangu na hilo ndilo agano nililoweka kwake na mbele za mungu”.
Nilipofika
“Nyumbani”
nilipanda kitandani na kuanza kumlilia Mungu kwa hasira huku nikifahamu kuwa NIME
MUASI KWA KUTOKUMSAMEHE BABA YANGU. Kwa kweli sikuwa na msaada mwingine
sikuweza kumwambia mama kwa kuwa hali yake ya uchumi ninaifahamu vyema,
ananisomesha kwa kukopa huku na huko, lundo la madeni limemuandama, hela ya
chakula, kodi ya nyumba na maji vinapatikana kwa ugumu sana, biashara yake ya
kuuza mboga za majani anayoifanya barabarani na mitaani ndiyo chanzo cha kipato
chetu, huku macho yetu yakimshuhudia baba kila siku usiku akitangaza taarifa
mbalimbali kwenye televisheni na kufurahia maisha yake.
Niliendelea
kulia kwa muda mrefu hatimaye usingizi ulinipitia na ndipo NDOTO HII ILIPONIJIA.
“
|
Niliota
niko barabarani natembea nikiwa pamoja na mama yangu, mbele yetu tulimuona
mwanaume mmoja wa makamo akiwa amezungukwa na vijana anapigwa na watu.
Tulipigwa na butwaa ila wale watu walipotuona walikimbia. Yule mzee alikuwa ameumia sana, tulipomkaribia zaidi
tuligundua kuwa ni BABA YANGU, Hasira zilinipanda nilitamani na mimi NIMUONGEZEE KIPIGO KINGINE ila mama
alinizuia na akaniomba nimsaidie.
Ilikuwa
ngumu sana kumsaidia kwa kuwa yeye hakuweza kunijali hata kidogo tangu nikiwa
tumboni mpaka sasa. Moyo wake wa unyama
haukustahili msaada wangu hata kidogo,
kwa uwezo alionao mimi sikupaswa kupata shida hata sekunde moja, wakati yeye
anakula na watoto na makahaba wake mimi ninakosa hata kipande cha sabuni cha
kuogea, nimeishi maisha ya kuomba omba kwa ndugu jamaa na serikali kama mtoto
yatima, kumbe nina baba mwenye uwezo na jina kubwa hapa mjini.
UKIYAJUMUISHA
YOTE HAYO SIKUWA NA SABABU HATA MOJA YA KUMSAIDIA NA wakati nawaza nimsaidie au
nimuache NILISHTUKA.
mmhhhhhhh!!!!!
mpaka sasa sijui nianzie wapi kupata HELA YA
ADA ila pia sijui maana ya hii ndoto, sina wa kumwambia
zaidi ya kuandika ili WATU WAISOME TENA ASOMAYE ASOME KAMA MAJI.
Ila nadhani
ndoto hii imekuja kutokana na ugumu wa maisha ninayopata na mawazo juu ya baba
yangu niliendelea kutafakari na kung’amua hili na lile na bila kujitambua
midomo yangu ikafunguka na kutamka TAFADHALI MUNGU RUDIA TENA SIJASIKIA
USEMALO.
MC AMON 0712000781)
No comments:
Post a Comment