Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Friday, October 18, 2013

KALAMU YA MAKALA:Tuwekeze katika michezo kukuza uchumi.Upo msemo usemao samaki mkunje angali mbichi. Ikiwa na maana samaki akishakauka suala la kumkunja litakuwa ni hadithi kwakuwa atavunjika. Msemo huu unatuasa kwamba kuna mambo yasiposhugulikiwa mapema yanaweza kuleta shida siku za usoni. Nikitafakari msemo huu na hasa kwa wale wapenda michezo watakuwa ni mashahidi kuwa wengi wa wachezaji wazuri kwenye michezo mbali mbali duniani ni wale walioandaliwa vyema tangu utotoni. 

Michezo ni moja ya ajira kubwa kabisa duniani na ni nyenzo muhimu katika kukuza na kutangaza utalii katika nchi husika. Hii ina maana kuwa, kupuuza michezo ni sawa na kusema ajira hii hatuitaki au nyenzo hii ya kukuza utalii sisi hatuitaki. Wengi wetu tumeonekana kuwa mashabiki wazuri sana wa michezo ila hali ya michezo kwa hapa kwetu si shwari kabisa.

 Kwahiyo, utakubali kwamba sisi wananchi tunaonekana kuipenda sana michezo na ndio maana huku mitaani watu ni wafuatiliaji wazuri wa michezo ya nchi mbali mbali hapa duniani kiasi cha kujivika ushabiki wa timu za huko ughaibuni ilihali hizi za hapa kwetu zinachechemea.

Hali hii ni ishara tosha ya uwajibikaji mbovu wa viongozi waliopewa dhamana ambapo mtu mmoja au kundi fulani dogo linaamua kufanya maamuzi yanayokuja kuligharimu taifa kwa miaka mingi kama hali ilivyo sasa. Haingii akilini kwanini mtu anaamua kufuta michezo mashuleni wakati ndio ilikuwa njia pekee ya kutambua vipaji vya watoto mapema, kwa kuwa kwa nchi changa kama yetu ni vigumu kuwa na shule za michezo (sport academy). 

Ikiwa hilo halitoshi, kumekuwa na hulka za kuwa na watu wenye uwezo mdogo wa uelewa na taaluma ya michezo kushika nafasi za juu kwenye vyama vya michezo. Hii imepelekea kuwa na migogoro isiyoisha kwenye vyama hivyo hali inayosababisha gurudumu la michezo kuzidi kurudi nyuma. 

Kuthibitisha hali mbaya hii iliyopo hapa nchini katika nyanja ya michezo, angalia matokeo ya Tanzania tunaposhiriki mashindano kadha wa kadha ya kimataifa. Ni jambo la wazi kabisa kuwa hatufanyi vizuri. Kwa mfano ukichukulia mpira wa miguu ni kwa mara ya mwisho mwanzoni mwa miaka ya 1980 ndio tulishiriki kombe la mataifa ya Afrika na hadi leo hatujaweza tena ukiachilia mbali kombe jipya la mataifa ya Afrika linaloshirikisha wachezaji wa ndani (CHAN) ambapo tulishiriki mara moja na hatukufua dafu na hata hivyo hatujapata tena nafasi ya kushiriki. 

Kwa upande wa riadha hasa mbio ndefu ambapo wadau wengi na wasomaji wa gazeti hili mtakuwa mashahidi kuwa ukanda huu wa Arusha na Manyara umekuwa ukitoa wakimbiaji bora kabisa wa mbio ndefu kwa miaka mingi hapo awali ila kwa sasa ni kama kumedorora. Hii yote ni kwasababu hakuna maandalizi ya kuvifahamu vipaji na kuviendeleza ili viweze kuwa nyota itakayong’aa kitaifa na kimataifa. 

Kuendelea kuiacha hali iwe hivi hivi bila kuchukua hatua za haraka na madhubuti ni kukubali kwamba sisi sote kama watanzania hatutaki tena kushiriki michezo bali tumejiweka kwenye kundi la mashabiki na kuendelea kujivunia kuvaa fulana za timu za huko ughaibuni ilihali timu zetu za hapa ndani hazina tena mafanikio. Katika zama hizi za kibiashara ni muhimu sana kutambua na kukuza vipaji kwakuwa sio tu vitaleta sifa kwa nchi yetu bali ni njia nyingine muhimu ya kuinua uchumi wan chi kupitia biashara hii ya kuuza wachezaji wa michezo mbali mbali na sio tu mpira wa miguu kama wengi wanavyodhani. Vipo vipaji vingi sana vimepotea kwa kutokuendelezwa katika umri unaofaa.

Hii kwanza ni jukumu la moja kwa moja la wizara husika, pili lije kwa watu binafsi nikiwa na maana ya wadau wengine wote wa nyanja hii ya michezo. Tufufue michezo na itakuwa msaada mmojawapo muhimu katika kuimarisha uchumi wan chi kwa siku za usoni.
Jina: Jackson Wilson Makala
Simu: 0767-884328/ 0783-784328
Barua Pepe: jacksonmakala@yahoo.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda