Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, September 26, 2013

ZAKAYO MALEKWA: Msomi na Nahodha wa Tanzania Olimpiki 1988 aliyegeukia Uchungaji


Na Gift Thadey
Jina la Zakayo Malekwa ni maarufu katika mikoa ya Manyara, Singida na Arusha kama mchungaji na muhubiri maarufu katika ukanda huu. Lakini Malekwa alikuwa mwanamichezo aliyeiletea nchi yetu sifa katika mchezo wa kurusha mkuki.
Malekwa ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu Usharika wa Hariabi na Bashai,anasema kuwa anajivunia mafanikio makubwa aliyoyapata katika mchezo huo ambao kwa sasa umepoteza umaarufu kabisa nchini, lakini ameamua kumtumikia Mungu.
“Hivi sasa namtumikia Mungu maana kama vile polisi wanavyofanya doria ya kulinda raia na mali zao, mimi nafanya doria ya kulinda mioyo ya watu hivyo tumegawana majukumu tofauti,” alisema Malekwa.
Malekwa anatoa wito kwa Wizara inayohusika na michezo kutambua matatizo yaliyopo, kuwatambua wanamichezo na kutafuta eneo la mafunzo kwenye eneo la Babati au eneo la Mamaisara wilayani Mbulu kwani pana mwinuko mzuri
Aliiasa wizara hiyo inayohusika na michezo kuwajali waasisi na kutowapuuza waliotangulia kwani kuna vitu wanajua na watumie rasilimali za kitaaluma zilizopo kama wataalam ambao ni wanamichezo wa miaka iliyopita kwani unapoacha kutumia rasilima unakosa maendeleo.
“Lazima tujipange ili tuweze kutoa wanamichezo wazuri kama miaka iliyopita ambapo tulikuwa na wanamichezo mbalimbali wakiwemo kina Malekwa, John Bura, Gidamisi Shahanga, John Akhwari, Filbert Bayi na wengineo” alisema Malekwa.
Alisema anajivunia mwanafunzi wake, Elizabeth Emmanuel, ambaye ni mzaliwa wa kata ya Dongobesh, ambaye ni mrusha mkuki mzuri na hivi sasa yupo kwenye jeshi la Magereza Arusha na anaongoza hivi sasa Tanzania kwa kurusha mkuki.
Aliwaasa wanamichezo kuwa na nidhamu kwenye michezo kwani michezo inahitaji kujituma tangu ukiwa mdogo na haitakiwa kujiingiza kwenye uvutaji sigara,ulevi na kushiriki uasherati.
Histori yake.
Mchungaji Malekwa ambaye ni mwanamichezo maarufu mstaafu wa kutupa mkuki alizaliwa mwaka 1952 kwenye kijii cha Kambi ya Nyoka wilayani Karatu na akakulia kijiji cha Dirim, katika kata ya Dongobesh Wilayani Mbulu.
Mwaka 1960 hadi mwaka 1966 alisoma katika shule ya msingi Dirim na mwaka 1967 hadi mwaka 1970 akasoma shule ya sekondari Endamasika na mwaka 1970 akajiunga na Jeshi la kujenga Taifa JKT Mafinga mkoani Iringa na mwaka 1974 akahamishiwa Jitegemee JKT Jijini Dar es salaam.
Mwaka 1978 Malekwa ajiliunga na chuo cha michezo cha Peiking China, mwaka 1980 akajiunga Oklahoma Marekani na mwaka 1983 hadi 1987 akajiunga na chuo cha Junior College Texas Marekani, kusomea stashahada ya sayansi.
Mwaka 1987 hadi mwaka 1989 akajiunga na chuo cha Plain View Texas cha Walden Pabtist University, kuchukua shahada ya sayansi ya jamii katika saikolojia ya michezo.
Mwaka 1990-1991 akajiunga na Texas Lutheran College Bale kusomea shahada ya sanaa na mwishoni mwa 1991 hadi 1993 akajiunga na chuo cha theolojia cha Whatbug Aiwa, Marekani kisha akarudi nyumbani Tanzania.
Rekodi alizoweka michezoni kwa kurusha mkuki.
Mwaka 1974, Zakayo Malekwa alianza kurusha mkuki na alivunja rekodi ya Taifa mwaka 1976 jijini Dar es salaam, kwenye michezo ya Taifa kwa kurusha mita 66.
Mwaka 1977, Peiking China, alivunja rekodi ya dunia
kwenye mashindano ya kurusha mkuki mita 74 na mwaka mwaka huo huo, alivunja rekodi kwa kuru
sha mita 68 kwenye mashindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika nchini Somalia.
Mwaka 1978 alishiriki mashindano ya All Africa Games nchini Algeria akawa mtu wa pili kwa kurusha mita 71 na mwaka 1979 alishiriki mashindano ya All Africa Games nchini Misri na akarudi nchini na medali ya fedha.
Mwaka 1978 alishiriki mashindano ya Jumuiya ya madola yaliyofanyika Edmunto Canada na akawa wa pili kwa kurusha mita 76 na mwaka 1979 alishiriki kwenye michuano ya Olimpiki ndogo iliyofanyika Mosco nchini Urusi na akawa mtu wa pili kwa kurusha mita 70.
Mwaka 1983 alisema Marekani kusomea michezo kwani aliona bila elimu siyo jambo zuri na kwa sababu
alikuwa na wito wa kuwa mchungaji akaamua kujiunga na masomo ya Theolojia.
Mwaka 1987 akavunja rekodi ya Afrika kwa kurusha mita 87 katika mashindano ya vyuo,Plain View Texas Marekani na pia akawa mtu wa tisa kwa kurusha mkuki mita 76 kwenye mashindano ya vyuo vikuu duniani Helsinki nchini Finland.
Malekwa kwa mwaka huo wa 1987 aliweza kukutana na Baba Mtakatifu Papa Yohana Paul wa pili na akazungumza naye kwa muda wa dakika 15, kwenye mashindano ya dunia yaliyofanyika nchini Italia, ambapo alikuwa mtu wa 12 kwa kurusha mkuki mita 78.
Pia, mwaka huo wa 1987 alishiriki kwenye mashindano ya Afrika mashariki mjini Nairobi nchini Kenya akawa wa pili kwa kurusha mita 78 na mwaka 1988 akabeba bendera ya Taifa kwa kuwa nahonda wa timu ya Tanzania katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mjini Seoul Korea Kusini.
Katika mashindano hayo ambayo Malekwa alikuwa nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, ilishiriki katika mashindano mbalimbali ikiwemo kurusha mkuki, riadha ya mbio fupi na mbio ndefu, ngumi, kuogelea na kuruka.
Baada ya hapo akaachana na michezo na kurudi tena darasani kwa ajili ya kuongeza elimu ya theolojia hadi mwaka 1993 akarudi nchini na hadi leo anaendelea kumtumikia Mungu akiwa mchungaji wa KKKT Dayosisi ya Mbulu Usharika wa Hariabi.
Anasema ana wito wa kulea, anahudumia waumini, anatangaza mikutano ya Injili na mwezi Oktoba mwaka huu, anatarajia kwenda Jamhuri ya Czech, kuhutubia mkutano mkubwa wa Injili na anangoja kwenda mbinguni.
Tanzania hususani mikoa ya Arusha, Manyara na Singida inahazina kubwa sana ya wanamichezo ambao waliiletea nchi yetu sifa, lakini jambo la kusikitisha ni kuwa, licha ya kutokuenziwa na kupewa heshima wanayostahili kwa kuitumikia nchi yetu, hata historia zao zimefutika. Wiki iliyopita tuliona jinsi John Steven Akhwari alivyoiletea nchi yetu heshima na jinsi Renata Kawala anavyofanya vyema nchini New Zealand lakini je tunautambua mchango wao?
Malekwa ni moja tu ya hazina hiyo, CV na rekodi zake zinazungumza zenyewe na hatumiwi ipasavyo. Tuchukue hatua, hatujachelewa

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda