Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, September 26, 2013

Barua ya Wazi kwa Mustapha Akonaay: Miaka mitatu chini, bado tupo vile vile!

Kwako mheshimiwa mbunge! Naandika waraka huu nikiwa sina uhakika kama ujumbe huu utakufikia ama la, lakini ninaimani wapambe wako wapo kila kona, hata huko "mjengoni" watakufikishia haya machache yaliyojaa moyoni mwangu.

Wakati naandika, akili yangu ilinipeleka nyuma, mwaka 2005 wakati wa Uchaguzi mkuu, hasa kauli ya aliyekuwa mbunge wetu wakati ule, ambaye aliutangazia umma kuwa "angeng'atuka" pale tu atakapoamua yeye na si tutakapoamua wapiga kura. Mheshimiwa, haraka akili inanipeleka mwaka 2010, ambapo wananchi hao walichoshwa na mtangulizi wako, wakadhamiria kuwa hata kama angegombea na
"jiwe" watu wangechagua jiwe. Ilikuwa kauli ya watu waliochoka na kutaka mabadiliko kwa namna yoyote ile.

Ndugu Mheshimiwa, nikiri kuwa, wapiga kura hao katu hawajutii kukuchagua uingie mjengoni ili ufaidi "mema ya nchi" kwani wakati wanafanya hivyo walikuwa wanataka mabadiliko. Hawakuwa na matarajio yoyote kwako na hata sasa wamebaki wanasubiri mwaka 2015.

Ndugu mheshimiwa, hata kama hawakuwa na matarajio yoyote kwako, lakini liwaahidi
mengi sana na pengine kwa hali ya kawaida yapo ambayo yangetekelezwa japo kwa usimamizi wako "mdogo", matokeo ambayo yangeleta tofauti na mtangulizi wako. Miaka mitatu baadaye, bado tupo palepale! Hakuna jipya. Barabara zetu bado ni mbovu sana hazimithiliki, bado wananchi hawana maji na huduma nyingine za jamii ni duni sana. Inasikitisha sana kuwa sasa wananchi wanatamani kurudi "Misri".

Nikukumbushe tu moja ya ahadi zako ambazo uliahidi ni lazima utimize, nalo ni kuhakikisha jimbo limegawanywa. Ninajua hilo si jukumu lako kiutendaji lakini
kwa kuwa uliahidi mwaka 2010,tunatarajia hilo linatekelezwa, naomba nikukumbushie tu, imebaki miaka miwili tu na usisahauuchaguzi wa serikali za mitaa ni mwakani, Ahadi ni deni

Ndugu Mheshimiwa sana, ukiwa unakaa mjengoni na “kufaidi kodi zetu wavuja jasho”, tunaomba ufahamu kuwa Haydom hakuna mahakama na ya kuwa inabidi kufuata huduma hiyo muhimu mpaka Dongobesh kilomita zaidi ya 50. Wewe ni mwanasheria,
sihitaji kukuambia umuhimu wa chombo hicho muhimu, kwa kifupi wananchi wa Haydom wanataka Mahakama!

Ndugu Mheshimiwa, hata jimbo lisipogawanywa, ukiwezesha kwa ushawishi wako kuhakikisha huduma za kibenki zinapatikana Haydom na Dongobesh hakika wafanyakazi na wafanyabiashara wa maeneo haya hawatakaa wakusahau. Inasikitisha sana, mwalimu wa Shule ya Msingi Semonyandi kata ya Hayderer,
ambaye juzi kati serikali iliongeza mshahara wake kwa shilingi 30,000/= anatumia zaidi ya kiasi hicho kwenda kufuata mshahara wake Mbulu, baada ya kufundisha
katika mazingira magumu!

Ndugu mheshimiwa, kwa sisi wapenda michezo, tumefarijika kuwa umeanzisha mashindano ya soka ya Kombe lako mheshimiwa. Tunaomba mashindano haya yawe ya wilaya nzima na yasiishie Mbulu mjini tu. Tunatarajia kupitia michezo hii, vipaji kutoka Gwandu Mehhi na vile vya kule Endamasak na Qaloda vitapata nafasi ya kuibuliwa. Pia mwakani hayo mashindano yasiishie kwenye soka tu, bali yaguse michezo kama Riadha na kurusha mkuki, michezo hii ndiyo iliyoijengea jamii yetu heshima kitaifa na kimataifa!

Ndugu mheshimiwa, katika "enzi yako" elimu imeshuka sana, japo hili ni janga la kitaifa lakini hali imekuwa mbaya zaidi katika miaka mitatu iliyopita. Ukiachilia
mbali ufaulu kushuka, lakini hata ile kasi ya ujenzi wa shule umeshuka sana. Je unajua kuna shule ngapi za serikali na binafsi zenye kidato cha tano na sita katika
jimbo lako? Usinipe jibu bali utafakari kwa kina.

Ndugu mheshimiwa sana uketiye mjengoni, uliahidi kuboresha viwanja vya ndege hasa wa Haydom na Mbulu. Ni kweli huduma hiyo ni muhimu lakini kwa “wateule wachache”. Wananchi wengi hawahitaji huduma hiyo, wanataka usafiri wa kuaminika,
wamechoka kuamka alfajiri huku wakihatarisha maisha yao ili wasafiri kwenda Mbulu au Babati na Arusha. Kifupi wanataka barabara nzuri.

Kuna mtu aliniambia kuna tofauti ya barabara ya lami na ile ya kiwango cha lami, baba mheshimiwa sana, tunaomba hata kamahalitatekelezwa hivi karibuni lakini
itatutia matumaini hata ile kusikia tu kuwa siku moja nasi tutakuwa na barabara ya lami ikikatiza katika wilaya yetu. Inawezekana hautambui umuhimu wa hili kwa kuwa muda mwingi upo Arusha, lakini hii ni ndoto ya wananchi ambayo wameacha kuiota.

Mheshimiwa sana, kwa utafiti wangu mdogo niliofanya nimebaini kuwa wananchi wa Wilaya ya Mbulu wanapoteza zaidi ya Shilingi milioni tatu kila siku kutokana na ubovu wa barabara, sawa na shilingi milioni 90 kwa mwezi au bilioni 1.08 kwa mwaka
ambazo ni sawa na bilioni 12.9 kwa miaka mitano . Hizi ni hela wananchi wanazopoteza moja kwa moja kama nauli achilia mbali uchakavu wa magari unaowakumba wamiliki wa magari. Hizi ni karibu nusu ya bajeti ya Halmashauri yetu kwa mwaka moja!

Usishangae mheshimiwa, ni hisabati rahisi sana kulitambua hili, kutokana na ubovu wa barabara, nauli huwa kubwa sana pengine hata mara mbili ya bei ya wanaoserereka kwenye mkeka”. Kutokana na ubovu huo, bei za bidhaa huwa juu sana na kupelekea ugumu wa maisha kwa wapigakura wako. Tunajua maamuzimengi ya nchi yetu yanafanyika kwa "ushawishi" na siyo kipaumbele, ndiyo maana kiranja mkuu
alipopewa rungu, alihakikisha kule kwao Katavi lami inafika. Usipopiga kelele unasahaulika mheshimiwa, hata sisi tunataka watoto wetu waione lami huku
"Marcopolo" na "Yutong" zikipishana mitaa ya Mbulu, Bashay na hata Dongobesh.
Mwisho mheshimiwa, ninaomba uwe karibu nasi wapiga kura wako kwani umekuwa mbali nasi, na hata unapokuja unaibuka tu bila taarifa na hata pale tunapokupa
kero zetu, unazichukua bila kuzifanyia kazi.

Tunakusihi pamoja na majukumu mengi ya “kamati ya bunge” uliyonayo japo siyo majukumu tuliyokutuma, ujitahidi kuhudhuria vikao vya Baraza la Madiwani ili kuisimamia pia Halmashauri yetu.

Ni hayo kwa leo mheshimiwa, nikipata nauli nitakufuata mjengoni nikueleze mengine mengi yanayotukumba hapa kijiji kwetu

Wako Mtiifu
Mpiga kura wako!

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda