Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Monday, March 11, 2013

Uzalendo na Uhalisia wake kwa Watanzania........ Sehemu ya Kwanza

 Na Mathew Mndeme
Wiki kadhaa zilizopita nilialikwa kwenye kipindi cha radio kwenye mojawapo ya vituo vilivyoko Dar es Salaam chenye malengo ya kutoa changamoto kwa watanzania kubadilisha jinsi tunavyofikiri na kufanya shughuli zetu ambazo ndizo haswa huchangia ujenzi wa Taifa letu katika kuleta maendeleo kwa kila mtanzania na Tanzania kwa ujumla. Mada ya mjadala wa kipindi nilichoalikwa ilikua ni swala zima la uzalendo kwa watanzania. Nilipata mwaliko wa kipindi hiki siku moja kabla ya kipindi chenyewe na ilinipa shida kidogo kukubali mwaliko. Kubwa kwangu lilikua ni nini hasa ningekwenda kuongea na maelfu ya wasikilizaji toka kila kona ya nchi yetu au nini haswa kilitakiwa na kutegemewa toka kwangu..

Wakati natafakari hoja ya uzalendo, nilijiwa na mambo kadhaa. Moja niliwaza kuwa hadi imefikia waandaaji wa kipindi kuleta mada hii radioni kwa wiki ya pili mfululizo, ni wazi kuwa kuna tatizo la uzalendo katika nchi yetu. Kuna kitu wameona hakijakaa sawa kwa maana ya uzalendo. Pili niliwaza, ni nini haswa maana ya uzalendo? Uzalendo ni nini na nini kiashirio cha mtu kuwa mzalendo au sio mzalendo? Tatu nikajiuliza ni kwa nini watanzania twakosa uzalendo? Tumekosea wapi au kwenye nini na lini au tangu lini? Nne nikajiuliza iwapo ni kweli tumekosea na kusababisha hali ya kutokua na uzalendo inayoonekana katika jamii yetu, je tunatakiwa kufanya nini ili kurekebisha jambo hili? Au twatakiwa kutokufanya nini ili uzalendo usiendelee kuwa tatizo? Nani afanye nini na lini?

Katika makala yangu hii, ningependa niongelee kidogo kuhusu mada ya uzalendo na kile nilichojikita kukiongelea kwa dakaika chache tulizokua nazo kwenye kituo cha radio na hasa kwa kujaribu kujibu maswali ya msingi yaliyonijia baada ya kupokea mwaliko.

Uzalendo ni nini?
Waandaji wa kipindi waliwaulizwa swali hili kwenye ukurasa wao wa facebook na kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu wakitaka watu watoe maoni ya uelewa wao juu ya uzalendo ni nini. Katika maoni mengi yaliyotolewa, watu walijikita katika kutoa tafsiri nyingi sana za nini maana ya uzalendo huku wengine wakijikita kutoa matukio yanayoashiria uzalendo na wengine wakitaja matendo yanayoonekana kama ishara ya uzalendo. Yako maoni mengine yalikua yanachekesha sana kama lile lililotolewa na moja alipowema umbea sio uzalendo huku mwingine akieleza ni jinsi gani anavyoguswa na uzalendo wa wanajeshi na walinzi wa usalama kwa jinsi wanavyojitoa kuhakikisha tuko salama. Kwa ujumla watu wengi walikubaliana na ukweli kuwa uzalendo ni hali ya mtu kuipenda sana nchi yake na kuwa tayari kujitoa kwa ajili yake.

Nakubaliana kabisa na tafisri hii lakini nataka niongeze au kuweka msisitizo kidogo juu ya tafisri ya uzalendo. Kwa mtazamo wangu, naona kama uzalendo ni neno pana na limebeba vitu vingi kidogo. Naungalia uzalendo kama kiashiria muhim sana cha tamaduni, mila, desturi na taratibu mtu anazokua amezibeba katika ujumla wa maisha yake ikiwa ni utambulisho wa jamii anayotoka au aliyoko. Nautazama uzalendo kama nadharia yenye nguvu kubwa na ninaweza kuifananisha na imani ya kidini. Sote twajua nguvu za imani katika kile mtu anachokiamini pamoja na kundi analoshirikiana nalo. Tunajua ni jinsi gani imani za watu zimekua utambulisho wao mkubwa katika vitu vingi ikiwa ni pamoja na matendo yao; mwenendo wao; maneno yao; aina ya marafiki zao; malezi yao; mitazamo yao; mikra zao, na mengi mengine. Ninapouangalia uzalendo kama imani, namaanisha kuwa uzalendo lazima uwe na sehemu kubwa katika kumwelezea mtu na jamii yake. Uzalendo uhusike katika kuweka mipango, kuchagua nini cha kufanya au kutokufanya, pamoja na kuwa na mambo ya msingi ambayo kwayo ujumla wa mtu unasimamia.

Nakumbuka tukiwa pale studio, msikilizaji mmoja alisema uzalendo haufai kufananishwa na mahusiano ya kimapenzi kama mke na mume bali unafanana na mahusiano au mapenzi kati ya mama na mtoto. Mimi nilioa shida kidogo katika tafisiri yake kwani kama ilivyo kwa mapenzi ya watu wazima, uzalendo lazima uwe na kujitoa kwa mtu (commitment). Mtoto na mama hawana maagano yoyote bali mahusinao na yao yanatokana tu na asili ya mfumo wa kuzaliana na kimajukumu zaidi. Nautazama uzalendo kama mahusiano ya kimapenzi ya hali ya juu kabisa ambayo ni mapenzi ya ndoa pale ambapo mtu unajitoa kumkubali mwenzako kama alivyo na kuishi naye katika hali zote ukiwa tayari kumlinda, kumtunza, kumsaidia, na kumuona kama sehemu ya wewe ulivyo. Uzalendo ni mapenzi ya kweli, ya dhati, ya kujitoa kati ya mtu na nchi yake na mengine yote yanatakiwa yawe matokeo tu ya mapenzi haya.

Mzalendo ni Nani?
Tunapoongelea uzalendo ni ngumu sana kusema nani ni mzalendo kuliko mwingine. Kama vile ilivyo katika imani kua ni ngumu kusema nani anamwamini Mungu kuliko mwingine, uzalendo nao hali kadhalika. Kwa kiwango gani tunamwamini Mungu itaoenekana kwenye mwenendo wetu; kauli zetu; matendo yetu na mawazo yetu. Matunda ndio yatatutambulisha kuwa sisi tunaamini na kusimama katika nini na sio kwa sisi kusema au kujinadi kuwa tuna imani kubwa kuliko wengine. Katika hali hiyohiyo, uzalendo hauji kwa kujinadi wala huwezi kujisifu kuwa wewe ni mzalendo kuliko mwenzako kwa sababu tu hujafanya au umefanya hili wala lile. Nguvu ya uzalendo haiko katika matendo tu maana mtu yeyote anaweza kutenda lolote hata lile ambalo halikutegemewa. Nguvu ya uzalendo iko katika ujumla wa mfumo wa maisha.

Ila pia niseme uzalendo hauna nguvu katika umwenyewe bali una nguvu katika umoja. Uzalendo unaonekana pale ambao uelewa wa uzalendo huo umekua wazi na dhahiri katika jamii husika na kukubalika kama mfumo wa maisha wa pamoja. Kuna mwimbaji fulani aliwahi kuimba na kusema, “Mimi Maasai bana; nadumisha mila ile wengine naacha”. Hakusema yeye maasai kwa kua anavaa rubega ya kimasai. Hapana; bali kwa sababu anadumisha mila zinazoutambulisha umasai. Rafiki yangu mmoja wa kimasai aliniambia katika mila za kimasai, iwapo hujapitia mafunzo ya jando na tohara ile wanayofanyiwa vijana wa kimasai kwa kukatwa maungo yao bila ganzi huku wakitazama na kutotakiwa kulia; basi wewe huwezi kujihesabu kama kijana wa kimaasai na hutakubalika. Akaenda mbali na kusema hata kama umepata tohara ya kisasa hospitalini, ukitaka uhesabiwe katika kundi ya wanaume wa kimasai lazima upitie ile tohara yao kwa mara ya pili ili kuthibitisha uimara na ujasiri wako. Uzalendo ni kujulikana wewe na mila/taratibu/tamaduni/ tabia na misingi unayosimamia.

Tumekosema wapi katika kudumisha uzalendo wetu?Makundi ya kiimani au kidini yanakua na nguvu pale yanapoelewaka yanaamini nini katika jamii ambayo kwayo wanaishi. Huwa na nguvu pale ambapo kundi husika linasimama kwa pamoja kutambulisha kile wanachoamini na kukisimamia katika umoja wao. Makundi ya imani yana vitu wanaita mafundisho ya msingi au misingi ya imani (Fundamental Doctrines) ambayo kwayo imani yao imejikita na kujitambulisha. Mafundisho hayo yanakua “very specific” kwenye nini wanaamini na nini hawaamini na unapotamka jina lao moja kwa moja mtu anapa picha ya aina ya kundi unalolizungumzia. Hutambulika kwa viongozi wao; majengo yao; kazi/majukumu yao na michango yao kijamii; na hutambulika kwa historia yao. Mtu mmoja aliniambi, kuna baadhi ya watu inapofika kwa mambo ya imani, wala hawataki kutumia tena akili bali huendeshwa na misisimko na miheuko ya ndani ambayo ni ngumu sana kuielewa.
Hali kadhalika, unapozungumzia uzalendo katika taifa ni lazima kuwa na mambo ya msingi tuliyokubaliana (Fundamental Principles) ambayo kwayo twayasimamia kama taifa. Mambo hayo ndiyo yatatutambulisha kuwa sisi ni watu wa aina gani. Unapozungumzia jamii kwa mfano za Kihindi, haijalishi yuko wapi au nchi gani, utaifa wao na utambulihso wake uko dhahiri. Wanajitambulisha kwa imani zao, wanajitambulisha kwa mavazi yao; wanajitambulisha kwa vyakula vyao; wanajitambulisha kwa tabia yao ya kupenda kukaa mijini; wanajitambulisha kwa tabia ya kuishi na kufungamana kifamilia zaidi; wanajitambulisha kwa bidii yao katika kufanya kazi na kujitafutia pesa “kwa njia yeyote ile”; wanajitambulisha kwa lugha yao, na kwa mengi mengine. Wana mambo ya msingi ambayo kwayo wanayasimamia na kujitambulisha na wanahakikisha wanayarithisha kizazi hadi kizazi.

1 comment:

  1. SAMAHAN, MM KAMA MM NIMESHINDWA KUSOMA HILI GAZETI MAANA NI REFU SANA HUWAZI KUSUMMARISE LABDA.LINACHOSHA KWAKWEL KWA WALE WATU WAVIVU KAMA MM NI NGUMU SANA.NI HAYO TU KWA LEO

    JARIDA.

    ReplyDelete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda