Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Friday, March 15, 2013

PCCB NAO WANAHITAJI KULETEWA “CIA”.


“Mtandao wa wikileaks wa Julius Assange ulivujisha mazungumzo ya Dr.Hosea na afisa wa kidiplomasia wa marekani(2007)ukieleza kuwa Dr.Hosea alikuwa anahofia uhai wake kwa kuwa alikuwa anashughulika na wala rushwa wenye nafasi kubwa serikalini na wanasiasa pia.Na alinukuliwa akisema kuwa Rais Kikwete ana hofu ya kuacha sheria ichukue mkondo wake”

Hivi karibuni Rais Kikwete alitangaza azma ya serikali ya kuwahusisha shirika la kijasusi la kimarekani CIA katika kushughulikia swala la mauaji ya padre lililotokea huko Zanzibar.Hili si jambo baya,ingawa linaleta tafsiri tofauti ikiwemo  ya vyombo vyetu vya usalama kushindwa kulisimamia hilo.
Uchumi wetu pia una wauaji wengi ambao chombo tulichokipa mamlaka kuwashughulikia wauaji hao bado hakijafanikiwa inavyotakiwa,nadhani nao wanahitaji “CIA” kutoka nje kuwasaidia kushughulika na Rushwa.
Juhudi za kupambana na rushwa zilianza tangu miaka hiyo wakati wa ukoloni wa uingereza.Mwaka 1938 na mwaka 1945 yalitolewa matamko ya kupingana na rushwa kabla ya sheria yakupingana na rushwa the Prevention of Corruption Ordinance (PCO) ilipoanzishwa Tanganyika.Mara baada ya uhuru 1961,Tanganyika iliendelea na sheria hii katika serikali ya wazalendo.
Ilipofika mwaka 1974 kikaanzishwa kikosi maalumu cha kupambana na Rushwa(Ant-corrupution squad-ACP) kabla ya kupitisha sheria mpya ya kupambana na rushwa iliyopelekea kuanzishwa kwa Taasisi ya kupambana na Rushwa(PCB) Mwaka 1991,baada ya kufanikiwa kuanzisha ofisi mbalimbali katika ngazi za wilaya,tarehe 1 july 2007 sheria mpya iliipa mamlaka ya kujiendesha yenyewe kama chombo huru na ndipo jina likabadilishwa na kuitwa taasisi ya Kupambana na Kuzuia rushwa Tanzania(PCCB).
Katika ripoti iliyozinduliwa mwaka jana mwishoni na Transparency International(TI) nchini Uganda imeonyesha Tanzania kushika nafasi ya pili katika Afrika mashariki kwa Rushwa kwa asilimia 40.7 ikilinganishwa na Rwanda yenye kiwango cha chini kabisa cha asilimia 2.5(Kama inavyoonekana katika jedwali hapo chini).Si ajabu Rwanda inapiga hatua kwa kasi sana kimaendeleo ukilinganisha na Tanzania kwa sasa.Nafasi tuliyopo kwa sasa ni mbaya zaidi ikilinganishwa matokeo kama hayo yaliyofanywa na taasisi ya Mo Ibrahimu katika kipengele cha Coruption Index(CI) kilichotuweka chini ya Kenya na Uganda.
Picture: Comparison of the countries by aggregate likelihood of bribery demand
Katika bajeti chache zilizopita wafadhili wanaochangia bajeti ya Tanzania kupitia GBS walitishia kutochangia bajeti ya Tanzania kwa sababu ya Rushwa.Kwa utafiti uliofanyika inaonekana bajeti ya Tanzania kwa asilimia 33 inapotea katika rushwa kwa sasa.Inakadiriwa asilimia 40 ya mapato ya kila mtanzania hupotea kwa sababu ya rushwa,hasa katika taasisi za polisi,mahakama,ardhi na TRA.
Mwaka 2006 Norway waligundua upotevu wa fedha takribani Usd Milioni 30 ambazo ni nusu ya fedha wanazotoa katika wizara ya utalii.Lakini baada ya kutishiwa kutosaidiwa bajeti zijazo Serikali ya Tanzania iliirudisha pesa Norway,na wakaamua kutusaidia tena Usd milioni 100 katika wizara ya Maliasili na utalii kwa mpango wa miaka mitano.
 Katika bajeti ya Tanzania ya mwaka 2011/2012 wafadhili waligoma kutoa kiasi cha shilingi 453 bilioni na sababu zilikuwa wazi;ni kutoshughulikiwa kwa kesi kubwa za rushwa nchini(Grand corruption scandal).Wameendelea kupunguza kwa kukosekana uwajibikaji na matokeo yake serikali imejitosa katika kukopa nje na ndani na kulifikisha deni la Taifa trilioni 22 kwa sasa.
Nchini Tanzania viongozi hawaogopi rushwa tena,wanajua watatajwa kidogo kisha watasahaulika;skendo kadhaa zimeitafuna nchi bila hatua za kuridhishwa kuchukuliwa;
  • TShs. 179 bilioni zilizopotea na sakata la Richmond,zingeweza kujenga nyumba 19,211 za walimu.
  • Shilingi 70 bilioni za skendo ya radar na BAE zingeweza kujenga angalau maabara 2,412
  • Msamaha wa kodi wa kifisadi waliopewa kampuni ya ukaguzi wa dhahabu ya Uingereza(Alex Stewart Assayers) zilitosha kutujengea vyoo 7,777 mashuleni,
  • Kashfa  ya majengo mawili ya BOT  ingeweza pia kutujengea madarasa 31,57.
Taasisi ya kupambana na Rushwa(PCCB) imewekwa ili kupambana na rushwa lakini cha ajabu sana imekuwa ikishutumiwa kila mara na hakuna hatua yoyote hadi sasa imechukuliwa.
Kati ya Mapendekezo 16 yaliyototewa na kamati iliyoongozwa na Dr.Harrsion mwakyembe katika sakata la Richmond,ilitaka uongozi wa juu wa PCCB kuondolewa.Hii ilitokana na sababu kuwa ni taasisi hiyo ndiyo iliyopitia swala la Richmond kabla halijafika mbali na kusafisha mchakato mzima kwa kusema kuwa haukukuwa na shaka yoyote ile.Hii inafanana na kumsafisha Chenge katika sakata la uuzwaji wa Rada na fedha kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1.5 alizoficha huko marekani katika kisiwa cha jersey.
 Kwenye mwaka wa uchaguzi 2005,BOT ziliibiwa takribani ya shilingi bilioni 40 kupitia kampuni isiyokuwa na kichwa wala miguu-Kagoda Agriculture(tena inasemekana documents zinaonyesha ilisajiliwa mei mosi siku ya mapumziko),kelele zimepigwa katika hili na hadi sasa serikali haijakanusha wala hakuna aliyechukuliwa hatua kuhusika na hili pia.
Tuhuma za viongozi waandamizi wa serikali kuficha zaidi ya bilioni 300 nchini uswisi,waziri mkuu alisema anayewajua wapeleke majina.Kama wananchi wanatakiwa kufanya kazi ya PCCB,tunahiitaji PCCB kwa kazi gani?Huwa inaamka wakati wa uchaguzi tu na kujisifia kukamata watoa rushwa kama ilivyofanya kwa Fredrick mwakelebela iringa na kumshitaki kwa kutoa laki moja wajumbe wagawane.Hawa wa uswisi nao vipi?
Mkurugenzi wa taasisi hii ya kuzuia na kupambana na rushwa,Dr.Edward Hosea ameshawahi kutuhumiwa kwa mambo kadhaa yanayomnyima hadhi kuiongoza taasisi hiyo kwa sasa.
 Skendo ya kuingizwa kwa sukari na Mohammedi enterprises iliyoghushiwa kuwa ni ya DRC kumbe ni ya Tanzania ilimuhusisha pia,baada ya mvutano wa muda mrefu habari zilivuja kuwa zilitolewa zaidi ya shilingi milioni 500 kuhonga PCCB na TRA ili kulifunika jambo hili,kashfa hii ni nzito pia.Kwa Mkurugenzi mkuu wa Taasisi hii ya kupambana na rushwa kumiliki kampuni ya uwakili tena inayojishughulisha kuwatetea walioshtakiwa na PCCB ni mgongano wa kimaslahi pia.
Kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2011 PCCB imeweza kurejesha bilioni 93 tu zilizokuwa zimeibiwa kwa rushwa katika maeneo mbalimbali.Lakini kati ya mwaka 2001 na 2008 Tanzania imepoteza trilioni 1.6,hii ni zaidi ya bajeti ya elimu kwa sasa.
Hivi karibuni raia wa uingereza kwa jina la Sarah amenukuliwa na gazeti la raia mwema la tarehe 28/feb alivyoandika facebook akisema ;Kikwete kuitaka PCCB ichunguze baraza la mawaziri ni sawa na kutaka KIKUNDI CHA WEZI kichunguze KIKUNDI kingine cha MAJAMBAZI.
Nadhani yafuatayo yanatakiwa yafanyike kwa haraka;
  • Kutekeleza mapendekezo ya tume ya Dr.mwakyembe kwa kufanya mabadiliko ya haraka katika nafasi za juu za PCCB.
  • Kuwa na sheria na utaratibu wa uwazi katika tuhuma,kama nchi za skandnavia zinavyochapisha majina ya wakwepa kodi nasi pia tuweke utamaduni wa transparency katika kuwataja wahusika wa rushwa.
  • Viongozi wanaohusishwa na rushwa walioko madarakani wanahitaji kuachia ngazi na kukaa pembeni ili kupisha utaratibu wa kufuatiliwa kwa tuhuma zao.
  • Uteuzi wa kiongozi wa Taasisi ya rushwa uwe wa uwazi kwa watu kushindanishwa kwa uadilifu(integrity) wao,na zoezi zima la usahili wao lazima ufanyike kwa uwazi.
Nadhani kama tulivyohitaji CIA kusaidia usalama wa Taifa na polisi kuchunguza mauaji ya Padre,tunahitaji pia “CIA” ya kifedha kutafuta Wauaji wa uchumi wetu.

Joel Nanauka

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda