Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Wednesday, March 6, 2013

JICHO LA MZALENDO:TUMEDHULUMIWA KAMA NCHI, SASA SERIKALI IMEAMUA KUDHULUMU WANANCHI.

Na Joel Nanauka
Mwandishi Maalum-Ohayoda


“Katika miradi mikubwa kama ile ya ujenzi wa chuo kikuu cha Dodoma serikali inadaiwa shilingi trilioni 1.2 na mifuko ya jamii nchini. Pia Serikali ilitumia kiasi cha fedha zaidi ya trilioni 3 kulipa mafao ya wastaafu ambao hawakuchangia kabisa katika mifuko ya pensheni. Mikopo hii ni fedha za wananchi na hakuna mkataba wowote”

Kwa sasa nchi yetu ina kilio kikubwa kinachotokana na mikataba mbalimbali ambayo imeleta hasara kubwa katika maslahi ya umma,ikiwemo kuliingiza Taifa katika hasara kubwa.Wakati Mh.Zitto kabwe alipowasilisha hoja binafsi kuhusu mkataba wa buzwagi bungeni.
Jambo la kwanza alilolihoji ni sababu za kusainiwa kwa Mkataba mpya wa wa Madini wa mgodi (mradi) wa Buzwagi kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick na sababu za mkataba huo kusainiwa nje ya    nchi,London Uingereza.

Vile vile alihoji kwa nini mkataba huo umesainiwa wakati bado serikali inafanya durusu (review) ya mikataba kufuatana na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Kuondolewa kwa kipengele katika Sheria ya Kodi ya mapato ya mwaka 1973 kuhusiana na asilimia 15% ya Capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure bila ya kibali cha Bunge lako Tukufu.

Hoja hii iliibua mambo mengi ikiwemo kuanika uzembe wa wenye dhamana katika serikalini na kupotea kwa mapato mengi katika sekta ya madini nchini.Hoja hii ilizaa matunda kwani viongozi waliohusishwa waliwajibika kwa kujiuzulu na ilipelekea marekebisho ya sheria ya madini ya mrahaba kutoka 3% hadi 4% ambayo ni faida kubwa kwa Taifa.

Tatizo la mikataba ndilo limeifikisha Tanesco hapa ilipo leo, kuanzia IPTL, Richmond hadi Dowans. Kwa kulitambua hili mara tu baada ya waziri Sospeter Muhongo kuteuliwa kuwa waziri wa Nishati na Madini pamoja na mambo mengine aliitaka bodi mpya ya Tanesco kuipitia upya mikataba 26 ambayo imeingiwa katika shirika hilo. Hadi mwishoni mwa mwaka jana ilionekana kuwa ni mikataba minne tu ndiyo ambayo imeweza kupitiwa, mikataba 22 bado haijamalizwa.

Hadi sasa katika eneo la mikataba, TPDC ina kesi 5 mahakamani na TANESCO ina kesi 200 mahakamani zinazohusiana na masuala ya mikataba. Kabla mikataba hii ishirini na sita haijakamilika bado kuna mikataba mingine mikubwa kadhaa tayari imeshasainiwa hivi karibuni ukiwemo ule wa kupata trilioni 1.2 kutoka Exim benki ya China za ujenzi wa bomba la gesi kutoka mkoani Mtwara. Swala ni je? umakini unaojitosheleza umezingatiwa katika kusaini mikataba hii ili kutorudia makosa? Hali hii ya kuendelea kusainiwa upya mikataba wakati bado mingine inapitiwa haina tofauti sana na kile kilichojitokeza wakati wa sakata la Buzwagi.

Kwa miaka mingi nchi yetu imejipambanua katika kuwa na wataalamu bora wa elimu katika sheria ukizingatia kuwa katika Afrika Mashariki Tanzania ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuanza kutoa elimu ya kisheria  tangu katika miaka ya 1950’s. Inakuwaje masuala ya mikataba yatusumbue kuliko majirani zetu?

Hivi karibuni pia suala la mikataba sasa likaibuliwa katika mikataba ya ndani kati ya serikali na mashirika ya mifuko ya hifadhi ya jamii. Kamati ya bunge iliyovunjwa ambayo ilikuwa na dhamana ya kusimamia mashirika ya umma(POAC) iliibua jambo nyeti kuwa serikali imekuwa ikikopa katika mashirika haya bila kuwa na mikataba yoyote ile.

Nia ya mifuko hii ya pensheni ni kuwekeza kwenye maeneo yenye kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuongeza thamani ya pensheni. Lakini kwa hivi sasa asilimia 70 ya mali za mifuko ya jamii ambazo ni sawa na shilingi trilioni 4.7 ni dhamana ya serikali, asilimia 22 imewekezwa kwenye majengo na asilimia nane zimenunuliwa hisa katika makampuni mbalimbali.

Katika miradi mikubwa kama ile ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma serikali inadaiwa shilingi trilioni 1.2 na mifuko ya jamii nchini.Pia Serikali ilitumia kiasi cha fedha zaidi ya trilioni 3 kulipa mafao ya wastaafu ambao hawakuchangia kabisa katika mifuko ya pensheni. Mikopo hii ni fedha za wananchi na hakuna mkataba wowote!

Kwa upande wake mkurugenzi wa LAPF, Eliudi Sanga anasema mfuko wake umeikopesha serikali bilioni 34 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Dodoma. Hii nayo haina mikataba!

Fedha za mifuko ya hifadhi za jamii ni michango ya wanachama ambao ni wananchi. Pamoja na kuwa hufanya hivyo kujiwekea akiba ya hapo baadaye lakini pia nia ya mifuko hii ni kuwa na uwekezaji unaojitosheleza ili kuongeza ajira na mzunguko wa kifedha kwa wananchi na pia kuwekeza katika huduma za jamii.

Kitendo cha serikali kuchukua fedha hizi bila kuwa na mikataba ni kuhatarisha usalama wa fedha za wananchi. Kwa upande mwingine ni aibu kubwa kwa serikali inayosifika kuwa inazingatia utawala bora na sheria (kama ripoti iliyotolewa na kamisheni ya kujitathmini ya afrika inavyosema) kuvunja sheria zake zenyewe na kukiuka jamabo hili la msingi. Yako maswali ya msingi ambayo ni pamoja na; kwa nini serikali iliamua kukopa pesa hizi bila kuwa na mikataba? tatizo si kukopa, tatizo ni kwa nini serikali inayotakiwa kusimamia sheria iamua kuvunja sheria?

Jambo lingine la kujiuliza ni kwa nini wasimamizi wa mifuko hii yote hakuna hata mmoja ambaye alijitokeza kulisema jambo hili? ni hofu ya kufukuzwa kwa sababu wanateuliwa?. Imefika wakati watanzania kuwa wajasiri katika kutekeleza majukumu yao bila kuwa na hofu ya kunyang’anywa nafasi zao, huu ndio uzalendo.

Tangu jambo hili liibuliwe bado hakuna tamko rasmi lilotolewa na serikali hadi sasa, nadhani tumeshaumia kama nchi katika mikataba ya nje, tusiumie tena katika mikataba ya ndani. Serikali ionyeshe njia kwa kuzingatia kanuni na sheria.

Joel .A. Nanauka
jnanauka@gmail.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda