Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Friday, February 1, 2013

Sakata la Kugawanywa Jimbo la Mbulu: Akonaay awapiga wananchi "Changa la Macho"

 • Mustapha awasaliti wapiga kura
 • Jimbo kugawanywa bado ni ndoto
 • Mwenyekiti CHADEMA alia na wajumbe

Mwanasheria wa wilaya ya Mbulu ndugu Deogratius
 Mathiya akitoa ufafanuzi wakati wa mgogoro wa uongozi
Haydom. Inadaiwa kuwa mheshimiwa Mbunge
amekuwa mbali sana na  wananchi wakati 

walipomhitaji na hivyo kuonekana kuwasaliti
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, moja ya ahadi ambazo alizitoa Mheshimiwa Mustapha Akonaay ilikuwa akiingia bungeni moja ya vipau mbele vyake vikuu ni kuhakikisha kuwa siyo tu jimbo la Mbulu linagawanywa bali pia ikiwezekana wilaya hiyo kongwe zaidi katika mkoa wa Manyara nayo unagawanywa ili kusogeza huduma muhimu karibu zaidi kwa Wananchi.
Licha ya Mustapha Akonaay kushinda siyo kwa sababu ya ahadi hiyo bali ukweli ni kuwa wananchi walikuwa wamemchoka aliyekuwa mbunge wa Mbulu ndugu Philip Marmo, lakini ni ukweli kuwa kwa muda mrefu Marmo alikuwa hataki jimbo jigawanywe kwa kuwa alikuwa akiungwa mkono zaidi na ukanda wa kusini mwa jimbo hasa maeneo ya kata za Haydom, Maghang na Maretadu. 
Mwezi Mei mwaka jana (2012) Ohayoda ilifanya mahojiano maalum na mheshimiwa Mustapha ikimkubusha ahadi yake ya kugawanya jimbo ambapo alikiri kuwa jambo hilo amelishughulikia na sasa jimbo la Mbulu litagawanywa, kauli ambayo siyo tu iliwafurahisha wapiga kura wake lakini pia ilileta ahueni hasa katika ukanda wa Kusini mwa jimbo la Mbulu ambako tokea Uhuru haijawahi kutoa mwakilishi bungeni isipokuwa Mheshimiwa Martha Umbulla, Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa manyara.
Jana Ohayoda ilifanya mahojiano na mwekiti wa CHADEMA wilaya ya Mbulu ndugu Ernest Martin na kutaka kujua uetekelezaji wa ahadi alizozitoa mbunge. Bwana Ernest alilieleza Ohayoda kuwa imekuwa vigumu sana kutekeleza ahadi mbalimbali hasa kwa kuwa Mbunge mara nyingi hayupo na hata katika vikao vya ndani ya Chama wajumbe wengi hawalipi umuhimu hili suala la kugawanya jimbo na imefika wakati yeye kama mwenyekiti anakosa nguvu ya kulisukuma kwa kuwa wajumbe wengine wanamwona kama anaajenda binafsi.
"Kwa kweli hili suala limekuwa gumu sana, kama wajumbe wanaotoka Haydom, Dongobeh na Maghang wangekuwa wanalipa msukumo ndani ya chama, tungekuwa na ubavu wa kumbana Mbunge atupe majibu ya kueleweka, lakini mimi kama mwenyekiti siwezi kulisukuma bila wajumbe kulileta, vinginevyo nitanekana nina ajenda binafsi" alisema Bwana Ernest, alipokuwa akiongea na mwandishi wa Ohayoda mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Halmashauri kuu ya CHADEMA taifa uliofanyika Ubungo jijini Dar es Salaam
Aidha Bwana Ernest aliongeza kuwa kuna mabadiliko makubwa ndani ya CHADEMA katika Wilaya ya Mbulu yanakuja ikiwa ni pamoja na kuweka viongozi makini wanaokubalika kwa wananchi.
"Tulipoteza kiti cha udiwani Haydom kwa kuwa hatukusimamisha mtu anayekubalika na watu pamoja na kuwa watu waliichoka CCM, chama ndio kilikiwa kinaingia maeneo mengi hivyo tulikuwa hatufahamiani vizuri, lakini sasa tunawafahamu watu makini na pia tunajitahidi kuwahamasisha wadau mbalimbali wenye mapenzi mema na nchi yetu wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama katika uchaguzi mkuu wa chama mwaka huu"
Aidha mheshimiwa mbunge amekuwa akilalamikiwa na wananchi kuwa mbali nao hasa walipomhitaji sana wakati wa vuguvugu la kuwawajibisha viongozi wa vijiji ambapo mara nyingi mbunge huyo alijitetea yupo "bungeni" ilhali wapiga kura wake wakilalamikia kutokumwona jimboni mara kwa mara mbunge huyo ambaye pia ni "katibu mkuu" wa Chama cha Wamiliki wa Makampuni ya Waongoza Watalli Tanzania (TATO) chenye makao yake makuu mjini Arusha!

Wakati huo huo, uchunguzi wa Ohayoda umebaini kuwa, katika kuelekea uchaguzi mkuu 2015, jimbo la Mbulu kwa sehemu kubwa litakuwa na mchuano mkali sana kutokana na Mbunge wa sasa Mheshimiwa Mustapha Akonaay kwa nyakati tofauti kukiri kuwa hana mpango wa kugombea tena kiti hicho, kitendo kinachotoa nafasi kwa watu mbalimbali "kutokwa na mate" wakitamani kurithi nafasi hiyo ya "kuingia mjengoni"
Kati ya majina yanayotajwatajwa ni pamoja na aliyegombea na kushindwa na Marmo ndani ya CCM ndugu Michael Lorry, aliyekuwa afisa tawala wa Hospitali ya Kilutheri ya Haydom bwana Samwel Mshashi, mwalimu na mjasiriamali maarufu Isack Awaki, aliyekuwa mwenyekiti wa H/W Mbulu ndugu ambaye pia ni diwani wa kata ya Gehandu ndugu Isack Bayo na Mbunge wa viti maalum (CCM) mheshimiwa Martha Umbulla.
Aidha wachunguzi wa mambo wanadai kuwa, pamoja na kauli ya mheshimiwa Mustapha juu ya kutokugombea, kunauwezekano mkubwa akabadilisha kauli yake japo kwa kiasi kikubwa umaarufu wake umeshuka hasa asipotekeleza zoezi la kugawanywa kwa jimbo.
Kwa vyoyote vile, uchaguzi mkuu ujao katika wilaya ya Mbulu hautakuwa mrahisi sana hasa kwa CHADEMA kutetea jimbo hilo, na habari za kuaminika kutoka ndani ya chama zinasema kuwa CHADEMA kinahaha kumtafuta mtu makini atakayeuzika kwa urahisi kwa wananchi hasa baada ya Mustapha kupoteza umaarufu na kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa CCM kulitwaa tena jimbo hilo. Kati ya majina yanayopigiwa sana chapuo ni Michael Lorry lakini changamoto kubwa ni kumshawishi atoke CCM na kuhamia CHADEMA huku akihofia kibarua chake "serikalini" endapo hatashinda.

2 comments:

 1. mwandishi naona umekaa kikanda zaidi!

  ReplyDelete
  Replies
  1. Sijakuelewa unaposema mwandishi yupo kikanda zaidi, maana sijaona kama kaandika lolote lililokaa kikanda. labda wewe ni moja wa wasiotaka jimbo ligawanywe?

   Delete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda