Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Sunday, February 17, 2013

Gharama za Harusi za Kisasa na Maisha Bora kwa kila Mtanzania....1


Imeandikwa na;
Mathew Mndeme, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaan

Ninaandika makala hii nikijua wazi kuwa inaweza  kuleta mjadala mgumu na miongoni mwa wengi watakaoisoma. Kuna uwezekano wa kuwepo watu watakaoona inawaharibia na haiwatendei haki. Lakini kwa upande wangu, naona huu ni wakati wa matengenezo kwa nchi yetu na matengenezo haya hayawezi kutokea kama tutaogopa kuambiana ukweli hasa katika yale mambo ambayo ni ya msingi na yanayogusa ustaarabu wa maisha yetu ya kila siku.  
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoneemeka kua na utajiri mkubwa. Utajiri huu hauko katika wingi wa mali asili pekee, ukubwa wa nchi na wingi wa watu, bali pia utajiri katika watu waliogawanyika katika makabila na tamaduni mbalimbali. Inasemekana Tanzania ina makabila zaidi ya 120 yanayozungumza lugha mbalimbali na tamaduni zinazotofautiana hata kama sio katika mambo mengi sana.
Sio lengo la makala hii kuongelea kwa undani juu ya utajiri wa utamaduni ambao ama kwa hakika ni wa kujivunia pamoja na ukweli kua kwa sasa unakutana na wakati mgumu  wa  changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknologia. Hata hivyo nataka niongelee kwa uchache juu ya kipengele kimoja katika utamaduni wetu kinachohusu ndoa na sherehe zake yaani harusi.

Ndoa ni eneo mojawapo katika tamaduni zetu ambalo limekua likipewa uzito mkubwa na maandalizi yake yamekua yakianza mapema sana katika malezi na makuzi ya watoto na vijana. Kuna sababu nyingi kwayo kupewa uzito huu lakini kubwa ni kuwa ili dunia iendelee kuwepo na kuendelea ni lazima mwanadamu aitikie mwito wa asili katika kuendeleza uzao. Hii ndio sababu kulikua na mafunzo maalum wakati wa tohara na unyago kwa wavulana na wasichana, pamoja na mambo mengine yakiwaandaa kuwa wanandoa watakaoweza kuishi vema na kutimiza wajibu katika familia na jamii katika ujumla wake. Kuna baadhi ya makabila bado yanaendeleza utamaduni huu. Taratibu za makabila mbalimbali zinaonesha ni jinsi gani sherehe za ndoa zilivyokua zinapewa umuhimu mkubwa na maandalizi yake kufuata utaratibu unaoeleweka kwa kila mwanajamii hata kama kwa tafsiri na mitazamo ya kisasa hazitakubalika katika ujumla wake. Jamii nyingi zilihakikisha ndoa zinafanyika wakati wa mavuno ya mazao ya mashamba ili kuwe na uwezo wa kutosha kifedha na kwa chakula kwa ajili ya kufanikisha mpango mzima huku suala la kuwazawadia maharusi likipewa umuhimu na nafasi ya kutosha ili kuwawezesha kuanza maisha mapya kwa furaha na bila shida.

Katika jamii zetu sherehe za ndoa ilichukuliwa ni jukumu la kila mmoja hasa kule vijijini. Nakumbuka wakati wa utoto wangu kule wilayani Arumeru mkoa wa Arusha ambapo ndipo nilizaliwa na kulelewa, harusi ilikua ni ya kijiji kizima bila kujali anayeoa au kuolewa ni wa kundi, dhehebu au dini gani.  Ilifahamika na viongozi wa dini, viongozi wa kijiji na wakuu wa koo. Wazazi wa kijana aliyekuwa anaoa na wale wa binti anayeolewa walishirikiana kwa karibu katika kuandaa harusi ikiwa ni pamoja na kuzunguka kijiji kizima na hata cha jirani, nyumba hadi nyumba, wakiomba ushirikiaano kwa tendo hili kubwa. Hapakua na michango ya harusi wala kadi za mialiko. Hapakua na bajeti ya watu 400 au 500 ambao watatosha ukumbi fulani. Harusi ilikua ni ya kila anayeweza kuhudhuria na ilifanyika katika maeneo ya wazi kama vile katika viwanja vya kanisa, shule ya msingi au shamba lililofyekwa vizuri kuwa kiwanja kwa vile haukua wakati wa mazao. Hapakua na michango ya sherehe za sendoff tunanazoziona leo kwani kijiji kizima hasa vijana wa kike na wa kiume walitambua fika kua usiku unaoamkia sherehe ya harusi familia ilitakiwa kwenda kuchukua sanduku la bibi harusi na kulileta kwa kijana kama ishara ya kuagwa kwake na kuondoka kwao. Hapakutakiwa chakula wala viywaji kufanikisha hili kwani watu walijitokeza wakiwa wameshiba na wenye nguvu za kuimba na kurukaruka hadi muda sanduku litakapofika linapopelekwa tena kwa miguu inapokua sio lazima kutumia gari.

Siku ya harusi watu walileta zawadi si kwa maharusi tu bali na kwa wazazi wao pia. Tuliwaona wamama wakimletea mama mwenzao (mama wa bwana harusi) vyakula mbalimbali ambavyo vingepikwa na kuandaliwa siku hivyo kwa waalikwa kama vile ndizi, mahindi yaliyokobolewa, maharage, mchele, sukari, na hata vilivyokwisha andaliwa kama vile Loshoroo (makande yaliyochemshwa vema kisha yakachanganywa na ndizi laini na kupekechwa pamoja na wingi wa maziwa mabichi na yaliyochacha). Wengine walishirikiana kuhakikisha maji ya kutosha yanaletwa toka chemchem na vyombo vinakusanywa kwa majirani kijiji kizima vitavyotosha kupikia na kupakulia chakula kwa ajili ya wageni wote na itakapotokea havitatosha basi palikatwa majani ya mgomba kwa ajili ya kusudi hili.  Wazee walitoa ng’ombe, mbuzi na kondoo kama zawadi. Vijana walijitolea nguvu zao katika kupamba, kufanya kazi ngumu, kupika na kugawanya vyakula. Wanawake walitoa zawadi ya vyombo mbalimbali ili mradi tu kila mmoja amehusika na amewajibika katika jambo hili muhim lililohusu kila mwana jamii.

Wakati wa harusi ulikua ni wakati wa undugu na mahusiano kujengwa na kuimarishwa. Ulikua ni wakati wa kufahamiana kwa undani na ilipotokea anayeoa na anayeolewa wametoka katika vijiji tofauti, basi undugu na umoja miongoni mwa vijiji hivi ulianzia hapo na vijiji hivi viliendeleza undugu huu katika shida na raha zote. Haya yote yanajaribu tu kuelezea ni nafasi gani ndoa ilipewa katika jamii na familia zetu. Nina hakika picha hii ya jinsi harusi zilivyofanyika miongoni mwa jamii za watu wa Arumeru ambao wengi wao walikua ni wameru, hautofautiani sana na jinsi ilivyofanyika katika jamii zingine za kitanzania hasa katika yale mambo ya msingi.

Kwa jinsi siku zinavyozidi kwenda ni dhahiri kabisa kuwa tamaduni nyingi za kitanzania zinazidi kupotea au kubadilishwa katika uhalisi na kimaana. Ni hakika waataalamu wa mambo ya jamii na tamaduni wataniunga mkono katika hili. Ziko sababu nyingi zinazopelekea hali hii lakini kubwa ni hili la mabadiliko ya kimaendeleo na ushindani wa kifikra katika umuhimu wa mambo. Jamii yetu inatoka au inahamishwa kutoka kwenye kufanya mambo kwa sababu yana maana fulani na yanaongeza uthamani na uhai wa tamaduni zetu, kwenda kwenye kufanya mambo kwa sababu ndivyo dunia inavyokwenda na ndivyo kila mtu afanyavyo. Jambo hili halitofautiani sana na zile kauli tulizokuwa tunaambiwa kule mashuleni hasa katika maswala ya migomo kuwa usifuate mob psychology, ikiwa na maana kua usifanye mambo tu kwa vile wenzako au fulani anafanya bila kuhesabu faida na hasara zake kwako kama mtu binafsi. Hali hii ni mbaya sana kwani inapoteza uhalisi wa mambo mengi na kuichanganya jamii zaidi ya kuisadia katika kupambana na mabadiliko yaliyoko. Tumefika mahali hatuelewi tamaduni zetu ni zipi na zisizo zetu ni zipi na kwa sehemu gani. Naomba nisieleweke vibaya hapa kua napinga mabadiliko, la hasha! Kwa sehemu nimebahatika kusoma kwa undani nadharia ya menejimenti ya mabadiliko (Change Management concepts) pamoja na utekelezaji wake kwa vitendo katika jamii. Kwa vile sio lengo la mada hii, sintaelezea dhana hii ya menemejimenti ya mabadiliko katika jamii kwani ni mjadala ni mada inayojitosheleza kutoka na umuhi wake unaoonesha kwa nini mambo au vitu viko kama vilivyo.

Labda niulize swali rahisi hapa; utamaduni wa Mtazania katika sherehe za harusi hasa kwa wale tulioko mijini ni upi? Ninapotaka kumwalika rafiki yangu aliyeko Dubai, au ukanda wa Gaza au Kashmiri au Texas kule nyumbani kwa Richmond, kua aje kuangalia harusi yangu itakayofungwa kwa utamaduni wa kitanzania, ninatakiwa niiandae kwa utaratibu upi? Je tamaduni zetu zinaelezaje maandalizi ya harusi na zinasema nini juu ya gaharama? Pamoja na tamaduni zetu, hali halisi ya maisha inatusaidiaje katika kuamua kwa usahihi na kufanya mambo kwa faida zaidi?

Wenzetu kwenye nchi kama Uganda na Malawi walio kwenye imani ya dini za Kikristo , Kiislam na hata zingine, bado wana kitu kinaitwa ndoa za kimila (Traditional Marriage). Na mara nyingine utaratibu huu wa ndoa za kimila hufanyika kisha kufuatwa na taratibu za kanisani au msikitini au kwingineko kwa kufuata taratibu husika. Mtanzania ambaye amekulia Manzese Kambi ya Fisi au yule wa Mbagala Rangitatu kwa Fundi viatu anapotaka kufunga ndoa, harusi yake inafuata utamaduni gani? Utambulisho (Identity) yake ni ipi?

Katika nchi yetu tunashuhudia harusi kila iitwapo leo hasa katika siku za mwisho wa wiki tena kwa wingi wa kutisha. Mara nyingine inakua ngumu kuamini kama hawa watu wote wanamaanisha wanachokifanya ua ni maigizo fulani katika kuandaa filamu. Harusi hizi huwa ni za watu wa tamaduni na imani tofauti.  Nataka nitumie muda kidogo kuangalia harusi hizi kwa undani zaidi bila kuzungumzia taratibu zingine kama vile posa na mahari kwa undani. Nataka tuangalie kwa pamoja bila kuficha wala kupendelea nini faida, hasara na matokeo ya harusi hizi ambazo kadiri siku zinavyoendelea zinachukua sura nyingine bila jamii kuliona hili katika harakati za kuondoa umasikini na kuleta maisha bora kwa kila mtanzania.

Itaendelea Jumatano

Mathew Mndeme ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliandika makala haya miaka 4 iliyopita katika gazeti la Raia Mwema. Makala haya yatakujia kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa. Unaweza kutoa maoni yako kwa kuacha comment hapa chini

1 comment:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda