Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Tuesday, February 26, 2013

JICHO LA MZALENDO: Tatizo la Elimu Nchini;Mfumo wa Usimamizi Unachangia


Na Joel Nanauka
Wapenzi wasomaji wa Ohayoda, kila Jumatano Mwandishi wetu Joel Nanauka atakuwa akituletea makala maalum ya JICHO LA MZALENDO, makala ambayo itakuwa ikijadili masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya nchi yetu na mwelekeo wake kwa ujumla. Leo Joel Nanauka anakuja na Mada inayosema; Tatizo la Elimu Nchini;Mfumo wa Usimamizi Unachangia

Hivi karibuni Taifa la Tanzania lilishuhudia kwa mara nyingine likipata aibu ya aina yake baada ya kutolewa kwa matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana ambapo wanafunzi zaidi ya 240,000 ya waliofanya mtihani walipata sifuri. Ingawa ukweli ni kuwa ufaulu wa wanafunzi watahiniwa katika ngazi ya kidato cha nne umekuwa ukishuka takribani miaka 4 mfululizo, jambo hili halikuonekana kupewa uzito wa juu sana kwa kuwa na muono wa mbali kama ilivyo kawaida ya wengi waliopewa dhamana ya kusimamia sekta mbalimbali nchini.

Pamoja na  changamoto nyingi zinazoikabili sekta hii kuanzia motisha ya walimu kushuka, idadi ya walimu kuwa ndogo (Unesco wanapendekeza uwiano wa 1:32, Tanzania ni 1:51), ukosefu wa vitabu na vifaa vya maabara na mengineyo, ningependa katika makala hii nizungumzie udhaifu wa sekta ya usimamizi wa elimu nchini Tanzania.

Imekuwa kawaida sasa kwa wasimamizi na viongozi wenye dhamana katika ngazi mbalimbali kutumia aina ya uongozi ya “reactive” badala ya “initiative”. Katika aina ya reactive, viongozi husubiri kutatua matatizo hasa baada ya tatizo kuwa kubwa na mara nyingi baada ya kuanza kulaumiwa na kuwataka kuwajibika kwa vitendo, kama tulivyoona kuundwa kwa tume ya kuchunguza matokeo haya. Katika aina ya  pili ya initiative viongozi hutumia uwezo wa kuona mbali kabla ya tatizo halijawa kubwa na kujaribu kulitatua kwa njia mbalimbali na kushirikisha wadau husika katika sekta hiyo.

Mfumo wa initiative leadership ungewezesha kuliona tatizo hili kwa mbali hata kabla halijafikia kiwango hiki cha leo. Kwa kuangalia matokeo haya 2009-26.46% sawa na idadi ya 65,708 walipata sifuri, mwaka 2010-49.60% sawa na 174,407 walipata sifuri, mwaka 2011-46.41% sawa na 156,085 walipata sifuri na mwaka 2012-60.1% sawa na 240,000 walipata sifuri. Hii ni kusema kwa miaka hii minne kuna wanafunzi wapatao 637,103 wamepata sifuri, wako wapi? wanafanya nini? si jibu rahisi kwa sasa. Na hili ndilo hasa linalopigiwa kelele na wadau kumtaka waziri Kawambwa kuwajibika kwani akiwa kiongozi anatakiwa kuona mbali na kuchukua hatuamadhubuti.

Kwa upande mwingine, idadi ya wanafunzi wa daraja wa kwanza kwa miaka minne iliyopita imeshuka kutoka 1.76% mwaka 2009 hadi 0.4% kwa mwaka 2012. Hii ni kusema kuwa kila mwaka idadi ya wanaopata daraja la kwanza inashuka na wengi wanajazana kati ya daraja la nne na sifuri. Hapo ni kutengeneza kizazi cha baadaye chenye uwezo mdogo sana katika kukabiliana na changamoto za maisha kwani kiwango cha ufaulu unaelezea ubora wa elimu waliyoipata.

Ili kujua tatizo halisi nadhani pia tuangalie mfumo wa usimamizi wa elimu yetu ambao hasa ndio unaoelezea nani anatakiwa kufanya nini na kwa wakati gani, akisimamiwa na nani na kwa muongozo upi. Hapa nchini vipo vyombo na taasisi mbalimbali ambazo husimamia elimu yetu katika ngazi mbalimbali kama vile, Wizara ya elimu, Taasisi ya Elimu Tanzania, Baraza la mitihani Tanzania na hata Kitengo cha huduma za walimu ofisi ya Rais utumishi wa umma.

Kwenye tamko la serikali namba 494 la tarehe 17 desemba 2010 wakati Raisi alipounda Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi stadi wizara ilipewa majukumu ya kuandaa, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa sera za elimu nchini, kufundisha walimu, uandikishwaji wa shule, ukaguzi wa huduma za elimu na miundo mbinu na huduma za kimaktaba.

Kwa upande mwingine usimamizi wa kiutawala wa shule za msingi na sekondari hauko tena kwenye Wizara ya Elimu bali sasa umehamishiwa katika Halmashauri zilizoko katika wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI). Baada ya mwalimu kuwa amefundishwa na wizara sawasawa na majukumu yake kulingana na viwango vilivyowekwa, anakabidhiwa kwa mamlaka nyingine (Halmashauri za Miji/Manispaa) ambayo ni Wizara nyingine kupangiwa vituo vyao vya kazi.

Wakishapangiwa shule za kufundisha idara ya ukaguzi inatakiwa kufanya kazi kwa niaba ya Wizara ya elimu kuhakikisha yale yanayotarajiwa kutoka kwa mwalimu huyu yanafanyika. Lakini hivi leo idara hii imedhoofika, magari yake yamechoka katika wilaya nyingi na uwezo wa kifedha wa kutembelea shule hizo umepungua sana. Hii inasababisha ubora wa elimu kutoangaliwa kwa wakati(monitoring) hivyo kujikuta mshtuko unatokea baada ya matokeo kutoka. Kama huwezi kufuatilia ubora wa elimu mara kwa mara unategemeaje kutoa elimu bora? usimamizi wa bunge kwa serikali ni sawa kabisa na usimamizi wa idara hii ya ukaguzi kwa shule zetu. Shule zinapokaa bila ukaguzi ni sawa na kuwa na serikali bila bunge la kuisimamia.

Ukweli ni kwamba idara hizi kwa sasa hazina fungu la kutosha na vitendea kazi vya  kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Na hapa tatizo si umaskini bali tatizo ni umakini. Kama huko nyuma idara hii iliwezeshwa na kusimamiwa ufanisi wake, inashindikanaje leo kufanyiwa hivyo. Kupuuziwa kwa udhaifu wa idara hii kumechangia kuharibu ubora huo wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi wa shule pia.

Kwa upande mwingine kuna kitengo katika wilaya kinachoitwa Teachers Sevice Department(Kitengo cha huduma cha walimu-TSD). Kitengo hiki hakiko chini ya wizara ya elimu wala TAMISEMI ,kitengo hiki kiko katika Wizara ya Utumishi wa Umma ambayo iko chini ya ofisi ya Rais. Pamoja na mambo mengine mwakilishi wa kitengo naye hutakiwa kutembelea shule zilizoko katika eneo lake na kufanya tathmini na mapendekezo mbalimbali.

Ni kitengo hiki TSD hutakiwa pia kushughulika na nidhamu ya walimu na kufanya vikao mbalimbali vya kupendekeza upandishwaji wa madaraja ya walimu mbalimbali. Kitengo hiki nacho kiko hoi, kasma wanayopewa kutekeleza majukumu yao mara nyingi ni laki 4 na ikizidi ni laki 6 kwa mwezi. Hiki bado ni kiwango kidogo sana ukilinganisha na uhitaji halisi na ukubwa wa kazi yao. Kwa mfano katika wilaya ya kinondoni Dar Es Salaam kuna walimu wasiopungua 5000 lakini idadi ya maofisa wa TSD wako 3 tu, huu ni mzigo mzito kuutekeleza.

Udhaifu wa kitengo hiki ndo hasa umepelekea kukua kwa deni la walimu kwani tathmini ya upandishwaji vyeo imekuwa haifanyiki kwa wakati. Matokeo yake pale inapofanyika inagundulika maelfu ya walimu muda wao wa kupandishwa vyeo umepita miaka kadhaa huko nyuma. Ili kutenda haki walimu hawa hupandishwa vyeo tangu ule mwaka waliotakiwa kufanyiwa hivyo ikimaanisha mabadiliko ya mshahara pia, na hii hupelekea sasa kuanza kuidai serikali malimbikizo yao. Kama utathmini huu ungekuwa unafanyika kwa wakati, madai haya yasingejilundika kama ilivyo sasa.

Kwa upande mwingine taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) inayosimamia uandaaji na utengenezaji wa mitaala kazi hufanya kazi hiyo kisha kuipeleka katika Wizara ya Elimu kwa ajili ya utekelezaji mashuleni. Katika utafiti wake William A. L. Anangisye (Phd) alieleza jinsi ambavyo utafiti wake katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa na Mbeya ulivyobaini kuwa kwa miaka 7 mtaala mpya umekuwa hautumiki. Katika kufuatilia akaelezwa kuwa Taasisi ya Elimu walishakabidhi kwa Wizara kuanza matumizi tangu mwaka 2003.

Kwa upande mwingine Chama cha Walimu Tanzania(CWT) kimeendelea kuwa na nguvu za ushawishsi kwa walimu kuliko serikali. Hii si kwa sababu ya kutetea maslahi ya walimu tu bali pia uwezo wake wa kifedha unaozidi kukua.Walimu ni 53% ya watumishi wa umma na uchangiaji wao katika Chama cha Walimu ni walazima na hukatwa moja kwa moja katika mishahara yao. Hii hufanya CWT kuwa moja ya taasisi zenye fedha nyingi za watumishi wa umma, hivyo wanao uwezo na nguvu ya kufanya utafiti pia na kueleza kilichoisibu elimu yetu hivi leo.

Ili kupata jibu la uhakika na lenye suluhisho la kudumu nadhani kamati itakayoundwa na Waziri Mkuu haina budi kujumuisha Taasisi hizi zote kwani kwa namna moja au nyingine zinahusika katika kutufikisha hapo tulipo. Kwa hili hatakiwi kuwajibika mtu mmoja, wako wengi wanatakiwa kuwajibishwa!!!!!

Joel .A. Nanauka
0688-677968
Mchambuzi wa masuala ya Jamii.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda