Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, February 21, 2013

Gharama za Harusi za Kisasa na Maisha Bora kwa kila Mtanzania....3 (Mwisho)

Imeandikwa na;
Mathew Mndeme, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Ilipoishia Jumatano
Bado hatujaona kuwa ndoa zinatolewa kwenye misingi yake na kuumbiwa mapambo yasiyo lazima na yanayopotosha umaana wa tendo hili muhimu katika maisha ya mwanadamu na uhusiano wake na Mungu? Bado hatuoni athari zake katika nyumba zetu za ibada? Bado hatujaona hili kuwa haliwasaidii wanandoa kuishi kwa furaha na amani na mara nyingine maandalizi haya yameharibu ndoa? Ni kweli hata makanisa imefika mahali harusi hizi zimekua deal la kupata pesa kwa watu kulipia makanisa hasa yale mazuri wanapotaka kufungia ndoa?
Ungana na Mwandishi katika sehemu hii ya mwisho ya makala hii....
Wanasiasa mnnaopigania maendeleo; bado hamujaona hili ni jambo linalohitaji elimu kwa munaowaongoza? Hamujaona kuwa linazuia watu kuwa na uwezo kuchangia madarasa, afya, kulipa ada na shughuli zingine za maendeleo? Hatujaona kua pesa nyingi sana zinatumika kwa kula tena siku moja na kwa watu wachache na wakiondoka hapo wanalaumiana kuwa kuku hawakuwa wa tamu kama wale wa sendoff? Ni hadi liwe ufisadi ndio tutaanza kulikemea?

Labda niangalize mambo kadhaa hapa;
Mosi; ninaona kuwa taswira hii ya harusi za kisasa zinawafaya baadhi ya vijana wa kike na wa kiume kuogopa kuoana kwa kufuata taratibu njema za kifamilia na kiimani. Watu wanapata uoga kuona kuwa hawataweza kukusanya mamilioni haya kwani sio wote wenye mtandao wa watu wenye fedha wanaoweza kuwachangia kwa kiwango hiki. Binafsi hawana uwezo hata wa kujikimu maisha yao achilia mbali wakusanye kwa ajili ya harusi. Baadhi ya vijana wa kiume wameogopa kuoa kwa sababu mahari za laki kadhaa au vimilioni kwao ni tatizo kubwa wasiloweza tafutia ufumbuzi.

Pili; kwa wale tuliosoma sayansi tunakumbuka vitu tunaita vipimo (SI UnitS) ambavyo hutumiwa kupiwa vingi au ukubwa wa vitu mbalimbali. Imefika mahali vijana wanaona harusi za wenzao ndio vipimo vya jinsi kila mmoja anapaswa kuoa au kuolewa. Wasichana hawawataki vijana ambao hawataweza kuwafanyia harusi kubwa kama ya Fulani na hawako radhi kukubaliana na ndugu zao ambao hawataweza kuwafanyia sendoff ya kishindo. Vijana hawataki tena kwenda kuoana vijijini ili ndugu zao na jamii iliyowalea ifurahi pamoja nao. Wnataka kuoa mijini ili waweze kupata michango na watu watakaoweza kufikia viwango ambavyo wanadhani ndio kipimo chao. Hawataki ndugu wa vijijini wawaaibishe sababu hawajastaarabika na hivyo kuharibu picha zao za mnato na za video.

Tatu; mbwembwe nyingi tunazotumia kuandaa hizi harusi hazijawasaidia vijana kuishi kwenye ndoa kwa malengo yake. Mara nyingine inasigitisha kuona hawa vijana hata hawajui ndoa ni nini na ni mambo gani yatakayowakabili na hakuna anayeliona hilo kwani mtazamo ni kuwasaidia kuwa na harusi ya nguvu. Wanapoagwa pale ukumbini na kubwaga hotelini wanajikuta wameachwa katika ulimwengu walisioufahamu na mashindano ambayo sio tu hawajajiandaa kwayo bali hawajawahi kuyasikia na hivyo kuonana maadau wasiweza kuishi pamoja. Ndoa nyingi tunazozishuhudia hudumu kwa kitambo sana ingawa zilichangiwa mamilioni yaliyoleta uamsiki kwa baadhi ya ndugu ambao walilazimika kujikamua.

Nne, kuna msemo kwa kingereza unasema “For every mistake/failure/problem caused by one person there is an opportunity for the other”. Tunawatengenezea watu nafasi za ujasiriamali zisizo stahili. Walio kwenye ujasiriamali wa mambo ya harusi mutanisamehe lakini naona kua kwa ujinga/kutofahamu/upotoshaji wa makusudi wa jamii kwa habari ya maana halisi ya harusi, wameibuka watu wanaokula bila jasho kwa sababu tu wanaweka muziki tena kwa CD sizizo nakala halisi na kushika kipaza sauti. Watu wanajitwalia mamilioni kwa sababu tu wanatandika mashuka ya pink na blue, wanapuliza matarumbeta , wanatuchemshia matoke, na wengine wengi wanaofanana na hao. Sisemi haya ni mabaya ila kwa asili na maana ya harusi zetu haya tungetakiwa kuyapata bila ngarama na pesa nyingi ambazo tunazihitaji sana kwa maendeleo ya jamii na familia zetu. Nakumbuka nilikua kwenye mji mmoja kwenye mkutano na watu kutoka nchi tofautitofauti za Africa. Mshiriki kutoka Nigeria na mwingine kutoka Madagascar waliposikia sauti za matarumbeta walichungulia toka ghorofani wakidhani ni vikosi vya jeshi vinapita. Hawakuamini tulipowambia ni harusi za kitanzania na mmoja alitamani akairudie yake iwe ya mtindo huo.

Tano; hii milolongo ya muda na pesa isiyo lazima katika maandalizi ya ndoa, inafanya vijana wetu wanachoka na kuona kuoa ni mateso. Inafika mahali wanawekeana visasi kwa ajili ya maumivu waliyosababishiana wao au ndugu zao wakati wa maandalizi ya harusi. Wakati mwingine wanachoka na wanaamua kuanza kufaidi matunda ya ndoa kabla ya harusi na inapofikia wakati wa harusi inakua tunafanya mambo kwa kujionesha tu na hakuna jipya kwa maharusi hao. Wengine hua wameshatoa mimba au wana mimba kubwa wakati wa harusi lakini jamii inawafanya walazimike kuigiza kuwa ndio wanaanza maisha. Wanajidangaya wao wenyewe, watuwadanganya wanaowatizama na Mungu wanayekwenda kuapa mbele zake na kumwambia wanamwomba awaunganishe wakati walishajiunga kitambo

Sita; jamii na hasa walio kwenye nafasi wasipopiga kelele kurudisha mambo kwenye mstari, kuna hatari kubwa ya kujenga kizazi kilichoacha mambo ya msingi na kukimbilia yasiyo na msingi na hivyo kupoteza mwelekeo. Tunajenga kizazi kinachoshindana kuvaa suti za Italia na Taiwan, magauni ya bei kubwa, kusheherekea kwenye kumbi za gharama na kutumia magari ya kifahari wakati kesho yake wanaingilia dirishani kwenye daladla za Mbagala. Tunajenga kizazi kinachoogopa ndoa kama UKIMWI kwa sababu ya gharama zisizobebeka na makwazo yasiyovumilika. Tunajenga kizazi kinachofanya kazi January hadi December kuapata pesa za kuchangia sherehe za ndugu,  jamaa na marafiki kwa sababu hakuna jinsi tunaweza watupa watu wetu. Tunajenga kizazi cha kuangalia nani alinichangia kiasi gani na mimi natakiwa kulipa fadhila kiasi gani leo.

Saba; Mimi nadhani kuna umuhimu mkubwa tukaachana na ushamba huu wa kisasa wa kuwezekeza kwenye sherehe za harusi. Tunaweza kubadili mwelekeo huu wa rasilimali watu, muda na pesa, ukaenda mahali ambapo matunda yake yanaweza kuwa wazi kwa watu wote na kwa vizazi vingi vijavyo. Tunaweza kuwafanya vijana wakaona kwa kufuata taratibu za imani na jamii zao bila kupotoka wala uoga. Tunaweza kuwasaidia kuona ndoa sio pesa wala haiwalazimu kuteseka ili waweze kuoa na kuolewa. Tunaweza tukaacha kupoteza muda mwingi kwenye vikao vya kupanga jinsi ya kula na tukavitumia kwa kuzijenga familia, jamii na nchi yetu katika mambo ya msingi. Nadhani tunaweza tukaepuka kuchekwa na wenzetu weupe wanaotushangaa tunapotumia mapesa mengi kwasherehekea huku tukiishi maisha magumu na tusiyoweza kupata mahitaji ya msingi (kama sio wewe unayeoa/olewa basi familia na ndugu zako kule kijijini). Tunaweza kuwaambia waumini makanisani, misikitini na kwingineko kuwa kutumia pesa nyingi na sherehe kubwa kwenye harusi sio lazima wala muhimu hasa kama mtu hana uwezo. Tutumie muda mdogo na rasilimali chache tulizonazo kufanya mambo yatakayotusaidia kubasilisha maisha yetu na kuleta maisha bora kwa kila mtanzania na sio vinginevyo.

Ninadhani kuna umuhimu wa kuanza kubadilika na tuache kutumia muda na rasilimani kufanya yale yasiyo ya msingi huku ya msingi yakidumaa na kutoweka katika jamii yetu. Tunahitaji ufunuo wa wakati (Timely Revelation) ili utusaidie kuwa na mtizamo sahihi wa hali ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania Anayetaka.

MWISHO.

Mathew Mndeme ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliandika makala haya miaka 4 iliyopita katika gazeti la Raia Mwema. Usikose makala ziingine ya Mathew Mndeme itakayokujia hivi karibuni kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa hapa hapa Ohayoda

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda