Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Tuesday, February 19, 2013

Gharama za Harusi za Kisasa na Maisha Bora kwa kila Mtanzania....2


Imeandikwa na;
Mathew Mndeme, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Ilipoishia Jumatatu 
Katika nchi yetu tunashuhudia harusi kila iitwapo leo hasa katika siku za mwisho wa wiki tena kwa wingi wa kutisha. Mara nyingine inakua ngumu kuamini kama hawa watu wote wanamaanisha wanachokifanya au ni maigizo fulani katika kuandaa filamu. Harusi hizi huwa ni za watu wa tamaduni na imani tofauti.  Nataka nitumie muda kidogo kuangalia harusi hizi kwa undani zaidi bila kuzungumzia taratibu zingine kama vile posa na mahari kwa undani. Nataka tuangalie kwa pamoja bila kuficha wala kupendelea nini faida, hasara na matokeo ya harusi hizi ambazo kadiri siku zinavyoendelea zinachukua sura nyingine bila jamii kuliona hili katika harakati za kuondoa umasikini na kuleta maisha bora kwa kila mtanzania.

ENDELEA........
Harusi za kisasa zimebadili picha ya harusi za kitanzania nilizotolea mfano katika sehemu ya kwanza ya makala hii na kubadilika kuwa miradi mikubwa inayohitaji wataalamu wa hali ya juu katika uandaaji, uendeshaji na ufanikishaji kama vile ilivyo kwa miradi ya MKUKUTA, MKURABITA na mingine inayofanana na hiyo.
Mandalizi haya yanaanza mara tu vijana wanaotaka kuoana kwa sababu yoyote ile waliyonayo. Ndugu na wazazi wa binti na wale wa kijana hukaa chini na kupanga taratibu zinazotakiwa kufuatwa kulingana na ustaarabu husika (nasema ustaarabu kwa vile wako wale wanaotaka taratibu za kabila fulani zifuatwe au wale waliokwenda shule na kuamua kutumia uzungu kama taratibu zao). Mara nyingine mambo yanakua mengi hapa na mafungu ya mahari huwekwa dhahiri na wahusika hutakiwa kuwajibika. Pale familia hizi zinapokua zimekwisha kuwekana sawa na kukubaliana katika mambo ya msingi, basi kijana anaruhusiwa kuomba kutoa siku ambayo angependa kuoa. Siku hii hujadiliwa katika majopo ya familia zote kuona kama inatoa nafasi ya kutosha kwa maandalizi ya msingi kufanyika. Mwisho wa siku harusi itapangwa na hapa maandalizi rasmi huanza. Huenda hadi hatua hii hakuna la ajabu sana zaidi ya mabishano na majadiliano katika taratibu na mahari ingawaje mara nyingine vijana hasa wa kiume huishia kulia kwa jinsi wanavyokamuliwa pesa ya mahari utadhani wanawekeza kwenye mgodi wa Buzwabi. Shida ninayotaka kuizungumzia mimi inaanzia hapa;

Siku hizi utaona kadi zinaandaliwa tena za bei kubwa kuwapelekea ndugu jamaa na marafiki kuwapa taarifa ya harusi na wajiandandae kuchangia aidha harusi au sendoff ya binti. Huenda ni miezi kama nane au hata mwaka kabla ya harusi taarifa hii ikitolewa. Muda si mwingi sana binti ataanza kuwa na majukumu lukuki akindaa kinachoitwa sherehe ya jikoni (kitchen party) na ile ya sendoff. Kijana pia ataanza harakati za miezi minne au zaidi kuanza maadalizi ya harusi. Hapa ngoma inakua nzito kusema ukweli. Kadi za michango zinataandaliwa na kusambazwa. Watu wataitwa kwenye vikao ambavyo havitofautiani sana na baraza la mawaziri au ile tume ya madini chini ya Jaji Bomani kwa jinsi vilivyo na mada zilizopangiliwa, ufuatiliaji makini na uongozi uliotukuka. Mara nyingine kama huna degree ni ngumu kuwa katibu au mwenyekiti wa kamati hizi.

Kwa wale tulio mijini, sio ajabu kusikia harusi Fulani itagharimu milioni kumi au kumi na tatu na zaidi ya hapo. Pesa hizi sio kua zimeandaliwa tayari bali zinatakiwa zipatikane kutoka kwa mifuko ya wahisani ambao ni ndugu, jamaa na marafiki. Ili kufanikisha hili kunahijika mpango mkakati na utaalamu wa kutafuta pesa toka kwa yeyote aliye na asiye tayari. Kule kwa binti utaambiwa sherehe ya jikoni itagharimu milioni tano na ile ya sendoff itakuwa sio kubwa sana hivyo itagharimu milioni tisa tu na itafanyikiwa ukumbi wa Ubungo Plaza au Impala hotel kama siyo kwa hotel dada ya Naura Spring. Hawa vijana wanaopanga au kupangiwa kufanya harusi ya aina hii ndio tu kwanza wameanza maisha na wanaishi kwa matumaini na uvumilivu wa mshahara mdogo, gharama kubwa za mafuta na nauli za daladala zisizo na huruma hata kwa watoto wa shule. Kijana anayeoa anaishi pale Tandale kwa Mtogole chumba cha kupanga ambapo mvua zikinyesha inabidi atafute daywaka (day worker) wa kumsaidia kuhamishia mafuriko kutoka ndani ya chumba chake. Kwa upande wake, binti hali sio mbaya sana kwani amefanikiwa kupanga pale Mburahati na sasa wanafikiria wakishaoana angalau wakatafute nyumba ya bei nafuu pale Manzese Mahakama ya Ndizi.

Kamati itaamua viwango vya chini watu wanavyotakiwa kuchangia ili kufikia malengo. Wachangiaji watapewa taarifa kabisa kuwa usipofikia kiwango hiki cha chini cha uchangiaji hasilani hutaruhusiwa kukanyaga eneo la ukumbi wa sherehe husika. Atatafutwa MC na muziki utakaolipiwa laki kadhaa, ukumbi ni wa milioni moja tu na gari la maharusi litapatikana kwa kamilioni pia kwani mtindo ni kukalia Limousine kama lile linalotumia na mtangazaji wa kikundi kimoja cha vichekesho katika kutangaza habari akijaribu kuonesha fahari ya pesa zake. Mambo mengine kama vile mapambo, nguo za harusi, fungate (honeymoon) na mengine , bajeti zao sio haba. Mwisho wa siku pesa hizi zinapatikana na harusi inafanyika.Ukumbuke kule kwa binti hadithi ni ileile na michango ni ileile. Kinachochanganya zaidi wahisani wanaotakiwa kufanikisha huu wingi wa sherehe za harusi za wapendanao ni walewale na hivyo kama utakua unafahamiana na watu wachache sana basi utajikuta kwa mwezi una kadi za kuchangia sherehe kama kumi hivi na tatu ni za harusi moja.

Hivi ni nani aliyesema huu ndio mtindo wa kuwaozesha vijana wetu? Hivi haya yote yanafanyika kwa faidia ya nani na kwa furaha ya nani?

Najaribu kufikiria kauli iliyojichukulia heshima katika medali ya kisiasa miaka ya karibuni iliyotelewa na Rais wetu ya Maisha bora kwa kila mtanzania ambayo itabidi tuifanyie marekebisho uchaguzi ujao iwe ‘maisha bora kwa kila mtanzania ANAYETAKA’  hasa kutokana na hali ya kimazingira nisiyopenda kuijadili hapa. Hivi hizi sherehe nzito za harusi na zinazogharimu pesa zinazotosha kukarabati yale majengo ya chuo kikuu cha nchi hii (Mlimani) vinasaidiaje hii kauli mbiu ya rais wetu? Tumeshawahi kufanya tathmini ya jambo hili na kuona lina faida au hasara gani kwa jamii yetu? Hivi huwa linawasaidiaje wale wanaoana kufikia lengo la ndoa yao?

Najua wako watakaojitokeza na kuweka upinzani mkubwa juu ya maswali ninayouliza na hata kuhoji usahihi wa mada hii. Lakini kwangu nitaona hayo ni mafanikio kwani nataka jamii ijitokeze na kuliona hili kuwa tatizo kama ilivyo kwa ugonjwa wa matende, UKIMWI na Malaria.

Hebu tungalie kile wachumi wanakiita Opportunity Cost katika hili. Tuangalie ni jinsi gani nyingine kwa vikao hivihivi na michango hiihii tungeweza kubadilia maisha yetu na maendelea kwa nchi yetu.

Hebu tufikirie muda tunaotumia kukaa vikao vya sendoff, kitchen part na harusi. Jaribu kufikiri miezi mitano ya vikao vya kila wiki au wiki mbili. Ni muda mwingi sana na tena ni wa muhimu sana kwa maendeleo yetu. Hebu changanya na gharama kuanzia za vikao hadi sherehe zenyewe. Mara nyingine inamgharimu mtu kutoka Mbagala kwenda kikao Tegeta changanya na muda wa usafiri njiani.  Ingekuwaje kama tungetumia pesa hizi na vikao hivi kusomesha familia na jimii zetu ili tuwe na kizazi cha wasomi? Ingekuwaje kama tungejadili jinsi ya kujenga nyumba bora na kuanzisha mitaji mikubwa kama ile ya NICOL itakayoendeshwa na watanzania na kuwa na uwezo wa kununua mashiraka ya umma yanayouzwa kwa wageni kwa bei chee? Ingekuwaje kama tungetumia rasilimali muda na pesa hizi kuona jinsi tunaweza somesha waalimu wengi zaidi kusaidia zile shule zetu za kata zenye waalimu waliosmea Kiswahili na Historia lakini wanaofundisha Fizikia na Hisabati?

Viongozi wa dini kama wachungaji, maaskofu, mashehe na weingine, bado hamujaliona hili kua mingoni mwa mambo ya kukemea na kutafutiwa ufumbuzi kama tunavyofanya kwa mambo mengine yenye maslahi kitaifa? Bado hatujaona kuwa ndoa zinatolewa kwenye misingi yake na kuumbiwa mapambo yasiyo lazima na yanayopotosha umaana wa tendo hili muhimu katika maisha ya mwanadamu na uhusiano wake na Mungu? Bado hatuoni athari zake katika nyumba zetu za ibada? Bado hatujaona hili kuwa haliwasaidii wanandoa kuishi kwa furaha na amani na mara nyingine maandalizi haya yameharibu ndoa? Ni kweli hata makanisa imefika mahali harusi hizi zimekua deal la kupata pesa kwa watu kulipia makanisa hasa yale mazuri wanapotaka kufungia ndoa?

Itaendelea Ijumaa

Mathew Mndeme ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliandika makala haya miaka 4 iliyopita katika gazeti la Raia Mwema. Makala haya yatakujia kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa. Unaweza kutoa maoni yako kwa kuacha comment hapa chini

2 comments:

 1. kuna uhusiano wa harusi..nikimaaanisha sherehe kubwa za kisasa na any biblical view,kuna mwongozo wowote wa kibiblia kuhusu ufanyikaji wa harusi..halafu kwa kuwa moja ya vitu vinavyohitajika ni pete,je ina ulazima maana naona kwa baadhi ya madhehebu haipo(nimezungumzia ukristo)

  ReplyDelete
 2. Hakuna mwongozo wa kufanya harusi au sherehe za harusi ndani ya Biblia kwa maana ya logistics, ukbwa na gharama. Ila nadhani Biblia unatufundisha mengi yanayoweza kutusaidia jinsi ya kufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na harusi. Kwa mfano Biblia inatufundisha unyenyekevu na kutojikweza. Inatufundisha kufanya mambo kwa kiasi. Inatufundisha kutokupenda anasa. Biblia inatufundisha kutopenda mashindano yasiyo na utukufu wa Mungu

  Hivyo mambo kama hayo na mengine mengi yanaweza kukusaidia kuamua vyema jinsi unataka kupangilia harusi yako. Ukiepenuka hayo hapo juu ni wazi huwezi kuteseka kutaka kufanya harusi kwa maana ya show-up na kutesa watu ili tu uonekane nawe upo. Utazingatia kuwa sio sahihi kutumia gharama kubwa kwa ajili ya masaa machache wakati kua mambo mengi ya msingi katika maisha.

  Lakini pia kwa uhalisi wake, harusi ni jambo la kifamilia. Familia inatakiwa iandae harusi na kualika marafiki zao kwa uwezo wao kuja kufurahi pamoja nao. Sio kama sasa inafanywa kibiashara na kuonekana ni mtaji wa ukusanyaji fedha na mali. Familia inatakiwa iandae harusi ya ndugu yao (wale watu wa karibu katika familia na hata marafiki lakini wale wa ndani kabisa sawa na ndugu). Waandae kulingana na uwezo wao halafu waamue nani wa kumualika kuja kula na kufurahi pamoja nao. Na sio kulazimisha watu wakufanyie harusi baada ya wewe kuwasetia viwango.

  MM (Mwandishi)

  ReplyDelete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda