Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Monday, February 25, 2013

4CCP, Mkombozi Group-Lushoto watoa mafunzo ya utengenezaji mkaa mbadala kwa shule 3 Haydom

Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni Haydom (4CCP) kwa kushirikiana na kikundi cha VICOBA cha Mkombozi Group-Lushoto kilicho chini ya (Inter Religious VICOBA) kimeendesha mafunzo ya siku 5 kwa wanafunzi wa shule mbili za sekondari na moja ya msingi katika kata ya Haydom mkoani Manyara.

Mafunzo hayo ya utengenezaji wa mkaa mbadala ambao unatengenezwa kwa kutumia makaratasi, maboksi, majani ya miti, vumbi la mbao (maranda), mabaki ya mkaa (chenga za mkaa) na udongo (wa kichuguu, mfinyanzi na hata udongo mwekundu) yalihusisha shule za Sekondari za Mama Kari na Haydom na shule ya msingi Haydom ambapo wanafunzi walifundishwa nadharia na vitendo ambapo baada ya mafunzo hayo waliweza kutengeneza mkaa huo na kuutumia.

Akizungumza na Ohayoda mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, mwakilishi wa 4CCP ambaye pia alikuwa mratibu wa mafunzo hayo alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanafunzi kupata ufahamu hasa juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi na kutoa njia mbadala ya kuzuia mabadiliko ya tabia ya nchi na kupunguza matumizi ya mkaa ambao huchangia katika uharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa hewa ya ukaa (Carbon Emission).
"Lengo ni kuwawezesha wanafunzi kuelewa kwa nini tuwe na mkaa mbadala, mali ghafi zinazohitajika na jinsi ya kuziandaa, namna ya kutumia mashine na namna ya kutumia mkaa huo kupikia. Pamoja na hayo, wanafunzi wameweza kujua jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na pia kuwapa wanafunzi ujuzi ambao unaweza kuwapatia ajira hata pale wanaposhindwa kuendelea na masomo" alisema Bwana Faustin ambaye ni maarufu kama "Meku".

Nao Bi. Zaujia Ally Hizza na Bi. Marietha Kusaga ambao ndio walikuwa wakufunzi kutoka Mkombozi Group-Lushoto alieleza kufurahishwa kwao na mafunzo haya kwani ni mara yao ya kwanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi pamoja na kuwa wametoa mafuzo sehemu mbalimbali nchini.
"Kwa kweli tumefurahi na ni mara yetu ya kwanza kuwafundisha wanafunzi japo tumetoa mafunzo katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Arusha, Moshi, Tanga, Dodoma, Mwanza, Morogoro, Manyara na pia tumepokea wakurufunzi kutoka Botswana lakini kote tumefundishwa watu wazima ambao ni wazito kuelewa tofauti na wanafunzi ambao pia ni wabunifu" alisema Bi. Zaujia Hizza

Naye Bi, Marietha Kusaga alisema kuwa kikundi chao kina jumla ya wanachama 28 ambapo pamoja na kutengeneza mkaa mbadala, wanatengeneza sabuni, usindikaji matunda na kuzalisha miche ya matunda lakini ni mkaa mbadala huo ambao umewapatia mafanikio makubwa tok kikundi hicho kianzishwe mwaka 2007
 Naye Mkuu wa Shule ya Haydom Bw. Vicent Gelangi akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo shuleni kwake alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa kwa wanafunzi wake kwani itawasaidia kuepukana na matumizi ya kuni wakati wa kupikia na pia wameweza kujifunza mambo mbalimbali kwa vitendo na pia kutoa fursa ya ujasiriamali

"Tunawashukuru 4CCP na wawezeshaji kutoka Lushoto kwa kutupa elimu hii muhimu sana. Pamoja na kutunza mazingira lakini ni fursa nzuri kwa wanafunzi ambapo hata wasipofaulu baada ya kumaliza elimu ya sekondari sasa wanaweza kujiajiri kwa kutengeneza mkaa huu na kuuza kwa akina mama Lishe na hata familia, kufeli siyo mwisho wa maisha na elimu hii ni ya msingi sana" Alisema Bw. Gelangi

Mkaa huo mbadala ambao hautoi moshi wala kutoa masizi, ni rafiki wa mazingira nagharama nafuu sana kuliko nishati ya mkaa wa kawaida kwani kwa kutumia makaratasi ambayo mara nyingi huchomwa au kutupwa au vumbi la mbao, makapi ya alizeti, magunzi, udongo wa mfinyanzi au kichuguu na hata majani makavu kama mali ghafi ambapo udongo au makaratasi hutumika kama gundi kushikilia malighafi hasa majani makavu au vumbi la mbao au hata vumbi la mkaa na moto wake huwaka kwa muda mrefu na kutosha kupika chakula cha familia

Naye Janeth John kutoka 4CCP alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na mafanikio makubwa sana na 4CCP itahakikisha kuwa inaanza kuzalisha mkaa huo mbadala kama sehemu ya kuhamasiha jamii kutunza mazingira na pia kama moja ya vyanzo vya mapato
"tutahakikisha na sisi tunazalisha mkaa huo na kuhakikisha kuwa kikundi chetu cha VICOBA nacho kinashiriki katika utunzaji wa mazingira" Alisema Janeth ambaye ni mara yake ya pili kupata mafunzo haya.

Ohayoda ilishuhudia baada ya utengenezaji wa mkaa huo, mabonge matatu maarufu kama "bricketes" vikitosha kupika chakula cha familia ya watu sita, mboga na kuchemsha maji na gharama yake ikiwa ndogo sana ambapo kwa mujibu wa wataalamu hao walisema wao huuza brickets tatu kwa shilingi 200 tu.

Huu ni mwanzo mzuri katika harakati za 4CCP na washirika wake wakuu Norwegian Church Aid-Tanzania (NCA) katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo kama zoezi hili litafanikiwa, litapunguza kama si kumaliza kabisa matumzi ya mkaa na kuni hasa vijijini ambapo wanawake huhangaika umbali mrefu kutafuta kuni. Zaidi pia, litaboresha maisha ya jamii kwa kutoa ajira mbadala kwa vijana na wanawake hasa wakijiunga na vikundi vya VICOBA ambapo kikundi cha Mkombozi kimepata mafanikio makubwa sana kwani wameweza kujenga Ofisi yao, ukumbi ambao wanaukodisha na stoo ya kuhifadhi bidhaa zao.

Aidha kama unataka kuwasiliana na Mombozi Group na namna ya kupata mashine hizi ambazo ni rahisi kuzitumia unaweza kuwasiliana nao moja kwa moja kupitia namba hizi 0787956245 na 0784604397 au barua pepe marietazaujia@yahoo.com

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda