Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Tuesday, November 13, 2012

Sakata la Kupindua Serikali za Vijiji lazidi kuchukua Sura Mpya: Kijiji kingine chauondoa Uongozi wa Kijiji

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa ukitaka demokrasia ya kweli nenda Mbulu, baada ya chama chake cha TANU pamoja na kukubalika nchi nzima kilipomsimamisha mgombea ambaye wananchi hawamkubali na kisha kumchagua mtu ambaye wanamkubali. Hiyo ilikuwa mmwaka 1961 lakini yakajirudia tena mwaka 1995 Karatu na 2010 likatokea tena katika jimbo la Mbulu ambako kote CCM iliwasimamisha wagombea wasiokubalika na wananchi bila ajizi wakawapiga chini.

Kwa wiki kadhaa sasa wananchi katika vijiji kadhaa tarafa ya Haydom wamefanya mapinduzi kwa kuwaondoa viongozi wao ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao kisheria. Baada ya kushuhudia panga hilo likiwapitia viongozi wa vijiji vya Gidarudagaw, Bisigeta, Getarer na Haydom, jana wananchi wa Kijiji cha Basonyagwe kilichopo nje kidogo ya mji wa Haydom nao wameuondoa uongozi wa kijiji chao wakiutuhumu kwa utendaji mbovu na kukisababishia hasara ya zaidi ya Shilingi milioni 50.


Akiongea na Ohayoda, mwananchi wa kijiji hicho Bwana Julius alisema kuwa pamoja na uongozi huo haujasoma taarifa ya mapato na matumizi kwa zaidi ya miezi 14 sasa, uongozi huo ulifanya uzembe na kusababisha hasara ya shilingi milioni 50 baada ya kukataa kumlipa mkandarasi aliyejenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya shule katika kijiji hicho.


"Mwenyekiti na serikali yake wamekuwa wakifanya mambo kimya kimya bila kuwataarifu wananchi, hawasomi taarifa wala hatukuwa tunajua mwenendo mzima wa kesi hadi juzi baada ya kupata amri ya mahakama ya kuuza shamba la kijiji" alisema mwananchi huyo mwenye hasira


Taarifa zinaeleza kuwa, mkandarasi huyo ambaye ni mkazi wa kijiji hicho alipewa tender ya ujenzi huo lakini alipomaliza hakulipwa fedha hizo na hata alipoenda mahakamani viongozi hao waliendelea kupuuza hadi hukumu ilipotolewa na mahakama kutoa amri ya kuuza mali za kijiji ili kumlipa mkandarasi huyo.


Ohayoda ilipowasiliana na mwenyekiti anayetuhumiwa Bwana Samuel Naman alizikana tuhuma hizo na kudai kuwa si kweli kuwa hajasoma taarifa kwa miezi hiyo bali alikiri kuwa mara ya mwisho alisoma taarifa mwezi Machi tofauti na sheria ya Serikali za mitaa inayotaka viongozi wa vijiji wasome taarifa kila baada ya miezi mitatu.

" Hao ni wapinzani wenye ajenda zao na wana maslahi binafsi kwenye jambo hili" alisema Samuel Naman ambaye ni maarufu kwa jina la Mainas anayefanya kazi katika Hospitali ya Kilutheri ya Haydom
Bwana Mainas aliendelea kueleza kuwa wao hawamtambui Mkandarasi huyo Bwana Bartholomayo  Bura kwa kuwa hawana mkataba na hakuna vielelezo kuwa yeye ndiye aliyejenga lakini Ohayoda ilipomwuliza kuwa je ni kweli amefanya ujenzi huo alikubali ila akasema "amejenga nje ya makubaliano" ambayo hakutaka kuyaeleza. Mwandishi alipozidi kuhoji iweje basi mahakama imtambue ilhali anadai hawana vielelezo alisema kuwa mahakama inataratibu zake na hawezi kuingilia taratibu hizo

Aidha Ohayoda ilivyohoji kuhusu amri ya mahakama na kwanini hakuhudhuria mahakamani kama inavyodaiwa alisema kuwa hawezi kulizungumzia hilo kwa sasa kwani huo ni uamuzi wa mahakama.


Taarifa zaidi zinasema kuwa, mara baada ya hukumu hiyo kutolewa viongozi hao walijaribu kukata rufaa lakini rufaa yao ikatupiliwa mbali kwani walikuwa nje ya muda unaoruhusiwa kufanya hivyo, na baada ya kugonga mwamba wakaamua kubadili umiliki wa shamba hilo la kijiji na kuwa mali ya Chama Cha Mapinduzi jambo ambalo limezua hasira za wananchi


"Kwanza huyu mkandarasi ni mwananchi wa hapa na alikubali tenda hii kwa bei ndogo ambayo makandarasi wengine waliikataa na akawa tayari kusubiri malipo, lakini viongozi hawa wanamruka kuwa hawamtambui" alisema mwanchi mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe


Katika mkutano wa wananchi wa kijiji hicho jana, wananchi hao waliuweka pembeni uongozi huo na kuuteua uongozi wa muda mpaka pale uchaguzi mwingine utakapotangazwa na mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kama ambavyo imefanyika katika kijiji cha Haydom wiki iliyopita na baadaye jioni watakutana ili kuamua hatma yao.


Wakati huo huo uchunguzi wa Ohayoda umebaini kuwa vuguvugu hilo linafukuta katika kijiji cha Ng'wandakw pamoja na kuwa lilizimwa hapo awali, pia katika vijiji vya Harar na Mewadan hali si shwari kwani muda wowote ule kinaweza kulipuka. Ni kijiji kimoja tu katika kata ya haydom cha Endaharghadatk ambacho kipo salama kwani viongozi wake wapo karibu sana na wananchi na wanatekeleza majukumu yao ipasavyo. Na taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa huko Dongobesh nako wananchi wameuondoa uongozi wa kijiji hicho


Vuguvugu hili linakuja miezi michache baada ya Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni Haydom 4CCP kuanza kutoa semina kwa viongozi wa serikali za vijiji na wananchi kuhusu Mfumo wa Ufuatiliaji wa fedha za Umma (Public Expenditure Tracking System PETS), na baada ya wananchi kujua wajibu wao wamekuwa wakali kwa viongozi ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.


Juhudi za Ohayoda kuongea na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ndugu Simoni Mayeye hazikuzaa matunda kwani namba yake ilikuwa inatumika. Lakini Ohayoda iliweza kuongea na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mh. Joseph Mandoo Guulo ambaye yupo Dodoma kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa CCM, alisema kuwa tatizo la Basonyagwe ni   la muda mrefu kwani shule hiyo ilijengwa wakati kijiji cha basonyagwe ni kitongoji katika kijiji cha Ng'wandakw hivyo deni hilo lilitakiwa kulipwa na Ng'wandakw lakini alimtupia mpira diwani wa Kata ya Haydom Mh. Nasaeli Sulle kuwa alitakiwa kusaidia kulitatua tatizo hilo ila akaongeza kuwa yawezekana kuna maslahi binafsi katika sakata la kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda