Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, November 8, 2012

Haydom is the Pride of Africa-Balozi wa Namibia nchini

Balozi wa Namibia nchini Tanzania mheshimiwa Japhet Isaack amesema kuwa amefurahishwa sana na aliyoyaona na kujifunza katika ziara yake ya siku mbili aliyoifanya Haydom kuanzia tarehe 7 Novemba hadi tarehe 8 Novemba 2012, na kusema kuwa urithi wa Utamaduni uliopo Haydom na jitihada zinazofanywa na kituo cha Utamaduni Haydom katika kuhifadhi na kuutangaza utamaduni wa jamii za Haydom ni fahari kwa bara zima la Afrika.
Balozi wa Namibia Japhet Isaack akisaini kitabu cha wageni kwenye Ofisi ya Kijiji cha Mongo wa Mono
Balozi Isaack ambaye pia anaiwakilisha nchi yake katika nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda na pia ni mwakilishi wa nchi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, UNEP na UN HABITAT, aliandamana na mke wake katika ziara hiyo yenye lengo la kuwafahamu vizuri kabila dogo la Wahadzabe ambao wanafanana na jamii za KhoiSans walioko kusini mwa Afrika.

Tofauti na makabila mengine ambayo yalihamia Tanzania yakitokea Magharibi (Wabantu) na Kaskazini (Wakushi na Wanailotiki) mwa Afrika, Wahadzabe na Wasandawe ndio wenyeji halisi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwani wamekuwepo kwa zaidi ya miaka 10,000 iliyopita, na jamii za Khoi Sans zilizopo kusini mwa Afrika katika nchi za Namibia, Botswana, Afrika Kusini, Zimbabwe na Angola zilihamia kusini mwa Afrika wakitokea Afrika Mashariki. Jamii zote hizi pamoja na Wahadzabe na Wasandawe huongea lugha yenye sauti za "Klik" (Clicking sound) na inasemekana kuwa kuna baadhi ya maneno hufanana.
Balozi Japhet Isaack, akirusha mshale alipowatembelea Wahdzabe katika kijiji cha Mongo wa Mono, Yaeda Chini

"Sisi tunajua kuwa tumetokea huku, tumekuja kujionea maisha ya ndugu zetu na hii siyo mara ya mwisho kwani tunataka kujenga uhusiana wa muda mrefu" alisema balozi Isaack wakati akiongea na Wahadzabe wa kijiji cha Mongo wa Mono.

Kabla ya kufika Mongo wa Mono, Balozi Isaack alishiriki katika shughuli ya Ufunguzi wa Wodi mpya ya akina mama ya haydom Lutheran Hospital, shughulin iliyohudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu ndugu Anatoly Choya, Askofu Zebedayo Daudi wa KKKT Dayosisi ya Mbulu, viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mwenyekiti wa Bodi ya HLH Mch. John Nade na wajumbe wa bodi ya HLH.

Akizungumza katika ufunguzi huo, mke wa Balozi Isaack ambaye kwa taaluma ni muuguzi mkunga, alisema kuwa kazi ya uuguzi hasa ukunga ni muhimu sana kwa kuwa inahusu kuleta maisha mapya duniani

"Unapokuwa mkunga unahudumia mama na mtoto, na hapa muuguzi anahusika kwa saa 24. Nimefanya kazi ya uuguzi kabla ya kutekwa nyara" Alisema mama balozi akimaanisha kabla hajaolewa.

Baada ya kukutana na wahadzabe jana na kushuhudia shughuli mbalimbali za wahadzabe ikiwemo uwindaji, michezo mbalimbali, ngoma na vyakula vya asili, leo balozi Isaack alitembelea kituo cha Utamaduni Haydom 4CCP na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo hicho.

Haydom ni sehemu pekee katika bara la Afrika ambako makundi manne ya lugha za bara la Afrika huishi pamoja, huwezi kupata sehemu yoyote ile. Haydom kuna makabila ya kibantu (wanyiramba na Wanyisanzu), Wahdzabe (Khoi Sans), Wakushi (Wairaqw) na Wadatooga ambao ni wanailotiki.

"Hili ni jambo la pekee sana, sijawahi kuliona popote Afrika na tunapaswa kujivunia jambo hili"
"Mnafanya kazi nzuri sana ya kuhifadhi utamaduni wa jamii hizi, nawaahidi huu ni mwanzo wa ushirikiano baina yetu na ninyi na juhudi hizi mziendeleze" Alisema Balozi Isaack wakati akiwa katika kituo cha utamaduni Haydom.
Balozi Isaack akitoa maelezo kabla ya kuondoka Mongo wa mono
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbulu ndugu Anatoly Choya alimshukuru Balozi huyo kwa kuja kutembelea sehemu katika wilaya yake na kuwa ni jambo la kujivunia kuwa sasa vivutio vya utalii hasa wa kiutamaduni vilivyopo wilayani Mbulu vinaanza kufahamika na kuipongeza 4CCP kwa juhudi wanazozifanya na kuahidi kutoa ushirikiano pale wanapomhitaji.

Ziara ya Balozi wa Namibia inakuja miezi miwili baada ya kufanyika tamasha la kwanza la utamaduni hapa Haydom ambalo liliwahusisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na kuwakutanisha na makabila ya huku. Ziara hii ni matunda ya tamasha hilo ambalo tunaamini litazidi kufungua milango na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo huku kwa dunia.


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda