Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, November 1, 2012

Breaking News: Wananchi Haydom wapindua Serikali ya Kijiji


  • Ni Baada ya kutokupata taarifa ya mapato na matumizi kwa miezi 13
  • Wahoji mwenyekiti kujenga miradi ya TASAF kwenye eneo lake
  • Mch. Fissoo wa Full Gospel ateuliwa mwenyekiti wa muda na Godlove Mushi awa Katibu

Katika kile kinachoonesha kuwa sasa wananchi wamechoshwa na utendaji wa serikali na kutambua haki zao kisheria, leo wamefanya kile ambacho kilikuwa kikionekana kuwa hakiwezekani baada ya kuuondoa uongozi wa kijiji cha Haydom uliokuwa chini ya mwenyekiti Bryson Emanuel, chini ya miaka 3 toka uingie madarakani mwaka 2009.

Wananchi hao bila kujali itikadi za vyama vyao kwa pamoja waliamua "kumtolea uvivu" mwenyekiti huyo baada ya kuchoshwa na danadana wanazopigwa kila mara na kutoitishwa kwa mkutano mkuu wa kijiji kwa zaidi ya miezi 13 kinyume na sheria inayomtaka kufanya hivyo kila baada ya miezi 3.

Wakiongea katika mkutano huo ambao uliitishwa kwa ajili ya kupata taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji, lakini kabla haujafunguliwa wananchi hao walimtaka mwenyekiti na baraza lake lote wakae pembeni na kisha kuuchagua uongozi wa muda, jambo lililozua "tafrani" kwa takribani saa zima kabla ya busara kutoka kwa baadhi ya viongozi akiwemo mjumbe wa serikali hiyo ndugu John Massay kuamua kukaa pembeni na kisha wajumbe wote na mwenyekiti kuamua kukaa pembeni kuwapisha Mchungaji Emmanuel Fissoo na Godlove Mushi kuongoza mkutano huo.

Katika kile kinachoonekana kuwa wananchi hao walikuwa na dhamira moja tu ya kuuondoa Uongozi, baada  ya kuanza mkutano huo Agenda kuu ilikuwa ni kujadili kero zao dhidi ya Uongozi huo ambao waliutuhumu kushindwa kutekeleza majukumu yao na kuwajibika kisheria.

Shutuma zilizoelekezwa kwa mwenyekiti huyo ni pamoja na kutokusoma taarifa ya mapato na matumizi kwa zaidi ya miezi 13, na hata iliyosomwa Novemba 2011 ilikuwa na mapungufu na haikupitishwa na mkutano mkuu na kutakiwa kuja na taarifa kamili lakini wakatokomea mpaka sasa.
"Kisheria kwa kitendo cha kutokutoa taarifa wala kuitisha mkutano mara tatu mfululizo kunamwondoa katika nafasi yake" alisema mwananchi mmoja huku akishangiliwa "Siyo sisi bali amejifukuzisha mwenyewe" 
 
Tuhuma zingine ni pamoja na mwenyekiti huyo kujenga mradi wa TASAF wa mashine ya kusaga nafaka karibu na nyumbani kwake (katika eneo lake), mradi huo ulitolewa kwa ajili ya waathirika wa UKIMWI lakini wananchi hao wanamtuhumu kuwa ni mwaka wa pili sasa mradi huo haufanyi kazi ilihali aliwakodishia waathirika hao eneo kwa muda wa miaka 3.

Mengine ni pamoja na kuikodisha Godown (Ghala) la mazao la kijiji kwa wawekezaji wawili ambao ni TANESCO na Bajuta International bila kuwashirikisha wananchi na mapato na matumizi ya fedha hizo hazijulikani. Hii ni pamoja na mapato kutokana na ushuru wa soko, gulio, faini mbalimbali na ruzuku kutoka serikalini ambazo hazijulikani
"Sisi ndio tunaoumia, ndio tuliowaweka madarakani na ni sisi ndio tumeamua kuwaondoa, huyu mwenyekiti tumemwomba sana atupe taarifa lakini badala yake tumekamatwa na kuwekwa ndani, malalamiko yetu yapo kwa mtendaji wa kata, diwani, DC na Mkurugenzi wa Wilaya, ni zaidi ya siku miezi 2 na hayafanyiwi kazi" alisema Elisamehe huku akiungwa mkono na wananchi karibu wote.

Wananchi hao walikuwa wanaonekana wamejipanga kwani walikuwa wamesimamia vifungu vya sheria na katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, hawakuwa na mjadala zaidi ya kufikia azimio la kuuondoa uongozi madarakani na kumtaka Afisa mtendaji wa Kijiji kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Wilaya ndani ya siku 7 ili aitishe uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
 
Katika mkutano huo, wananchi hao hawakutaka mwenyekiti huyo kujibu chochote na kumtaka asiingie tena ofisini, hata na hivyo Ohayoda ilipata fursa ya kufanya mahojiano naye ambapo alikana tuhuma hizo zote.

"Ni kweli taarifa haijasomwa kwa muda mrefu lakini kulikuwa na sababu zilizonje ya uwezo wangu" alisema Bryson
Ohayoda ilipomtaka kutoa sababu hizo alisema kuwa "vitabu vilichukuliwa toka Februari na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na havijarudishwa hivyo kushindwa kuandaa taarifa"
Lakini Ohayoda ilipomwuliza kama hivyo vitabu havijarejeshwa mpaka leo imekuwaje leo wakajiandaa kusoma taarifa hiyo na kama kama vitabu vya risiti vilichukuliwa wamepokea vipi fedha kwa ajili ya michango na malipo mbalimbali katika kipindi chote hiki alishindwa kujibu swali hilo badala yake alimtaka mwandishi aende ofisini ataoneshwa makbrasha, japo wakati huo ofisi "ilikwishatekwa"

Mapinduzi haya ni muendelezo wa mapinduzi yanayofanywa na wananchi katika vijiji mbalimbali katika Tarafa ya Haydom ambapo hivi karibuni wananchi wa vijiji vya Gidurudagaw na Getarer waliuondoa uongozi madarakani kwa kutumia nguvu ya umma na katika kijiji cha Ng'wandakw mapinduzi kama hayo yalizimwa japo bado kwafukuta.No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda