Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, August 2, 2012

SINTOFAHAMU: Viongozi wanafaidika vipi na matatizo yetu?

Na Amani Paul, Endaharghadatk
Kimya kingi kina mshindo mkuu, baada ya kukosekana hewani kwa takriban zaidi ya mwezi SINTOFAHAMU imerudi kwa kishindo ikiwa imesheheni mambo mbalimbali mbali ambayo kwa namna moja au nyingine yatakugusa na kukufanya uchukue hatua stahiki, wewe, mimi, yule na mwingine kila mtu kwa nafasi yake.

Philip Marmo
Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikifanya tathmini ya hali ya mambo ilivyo katika sehemu mbalimbali nchini hususani huku kwetu, wakati hali ya maisha na utoaji wa huduma katika karibu kila sekta vikiwa duni kupita maelezo, viongozi wetu tuliowapa dhamana ya kutuongoza wakifaidika na wakiishi katika neema. Yaani ni sawa na kuanzisha biashara yako halafu ukamwajiri "Meneja" aiendeshe hiyo biashara lakini kinyume na matarajio yako, badala ya kukupa faida biashara hiyo siyo tu inakupa hasara kila kukicha lakini pia huyo meneja anageuka kuwa mfalme na wewe kuwa "kanyaboya" usiye na thamani na kukutumbukiza katika umaskini mkubwa. Ndivyo ilivyo, tumewaweka viongozi lakini wametusaliti na kutufanya kuwa watumwa ndani ya nchi yetu wenyewe.

Mifano ipo mingi kuanzia ng'azi ya kitaifa hadi vijijini, viongozi ni miungu watu, wasiotaka kuhojiwa wala kuwajibika kwa wananchi, kote inatumika vitisho, jazba na wamweka usiri mkubwa sana katika namna wanavyoendesha mambo katika ofisi hizo. Swali ni je, viongozi wetu hawa huwa wanapata raha gani pale wanapoona wananchi wanakuwa kwenye matatizo?
Wiki iliyopita bungeni kuliwaka moto baada ya kubainika kuwa mateso yote tuliyokuwa tunayapata watanzania kutokana na mgao wa umeme kumbe ni matatizo ya "kutengeneza", yaani hadi mkuu wa kaya anaingizwa mkenge na kuaminishwa kuwa tatizo ni uhaba wa maji kumbe wazandiki hao wanafaidika na mgao huo ili wao wauze majenereta na mafuta. Ni uwendawazimu mkubwa na ni kosa la uhaini kwani huku ni zaidi ya kuhujumu uchumi bali ni kuliua taifa kwa makusudi! Sintofahamu na haitokaa kuniingia akilini eti hata nguzo za umeme zinazovunwa Iringa zinasafirishwa hadi Mombasa na kurudishwa nchini na kuuziwa TANESCO kana kwamba zimetoka Afrika Kusini, hata kama Tanzania imekuwa shamba la bibi ila sasa yamezidi.

Hayo ni ya Tanesco na wizara ya nishati na madini ambayo yanatendwa na mapapa na manyangumi kunako bahari kuu, wahenga walisema avumaye baharini papa kumbe wengine wamo, tena wanatisha pengine kuliko hao mapapa wenyewe, hawa ni makambare ambao wanawanyanyasa dagaa huku ziwani ni kwenye mabwawa, hawa hawamulikwi hawaulizwi na wala hawashauriki, hata kama lina tija kwa manufaa ya wananchi waliowengi na yeye akiwa moja wao lakini anapoona na  "mbaya" wake anaweza kufaidika hawakawii kuweka vikwazo.

Sintihahamu nani anafaidika sana na matatizo ya maji Haydom, najaribu kuwaza na kuwazua lakini sipati jibu. Vyanzo vya maji vipo na inasemekana kuna wafadhili walitaka kuleta mradi wa maji mji wa Haydom lakini "siasa" ziliwafukuza, ningeelewa labda kama kuna moja wa hao wakubwa wanafanya biashara ya kuuza maji lakini sijaona. Watu wanashinda kwenye foleni kwa masaa mengi katika vioski vichache vinavyouza maji badala ya kufanya shughuli zingine za uzalishaji. Sintofahamu mradi au mamlaka ya maji (kama ipo) inawajibika kwa nani, nini malengo yake na inafanya kazi gani? Ninachoona inakusanya mapato, toka nakua mpaka leo sioni mabadiliko yoyote hakuna vioski vipya zaidi ni kauli za kisiasa kuwa sasa maji kuanza kusambazwa kwa wananchi manyumbani.....siasa...siasa ....siasa! Hakuna ripoti yoyote ya mapato na matumizi, swali kwa hawa ndugu zangu, ambao naamini nao wanapata machungu tuyapatayo maana nao ni sehemu ya jamii hii, wanafaidikaje na uhaba wa maji?

Huu ni mfano tu wa mengi na uozo na upunguani wa viongozi wetu nchini, wanakata tawi walilolikalia tena chini kukiwa na mamba wenye njaa. Ipo siku kama siyo wajukuu basi vitukuu vyenu vitafukua makaburi yenu wakitaka kupima kama kweli mlikuwa na akili timamu ama mapunguani kufanya maamuzi ya kipuuzi mliyoyafanya.
Yapo mengi sana, kutoa tenda hasa za ujenzi wa barabara kwa makandarasi wasiokidhi viwango wakati wote kama siyo yeye basi hata ndugu zake ni waathirika wa ubovu wa barabara. Kwenye elimu ndiyo usiseme, tunatengeneza taifa la "mbumbumbu" kwa ajili ya ubinafsi wa viongozi kwa kutoa elimu duni kwa watoto wa maskini waliowengi, sintofahamu wanafaidikaje viongozi hawa kama mtoto wa mzee Barabojick wa Gidmadoy anayesoma shule ya sekondari Endanachan akapata elimu bora akafaulu, hivi inamaana akifaulu Nsanganzelu inamzuia Endeko kufaulu! Ni upunguani tu kwani mshumaa haupotezi chochote kwa kuwasha mshumaa mwingine!

Biblia imesema kuhani atakula madhabahuni, sawa kabisa basi hata unapokula basi kula ukiwa umefanya la maana, siyo unakula mbegu zote! Hata ukitaka ng'ombe akupe maziwa lazima umpe majani, sasa wewe ndugu yangu unakamua tuuuuuuuuu hadi damu khaa unapata raha gani? 
Sintofahamu kuhusu huu ubinafsi wa hawa viongozi wetu! Pengine ni laana.... Mungu aepushie mbali tena kwenye sayari ya mbali zaidi ya Pluto! 
Akhamis Kareem!

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda