Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Wednesday, August 29, 2012

Salamu kutoka Haydom: Haturudi Nyuma Kamwe

 Na Amani Paul
Wakati naanza kuandika Ohayoda kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu, ilikuwa kama kuendesha gari usiku, huwezi kuona zaidi ya yadi 200 lakini unapozidi kusonga mbele kiza huzidi kusogea kwa yadi zingine 200 hadi unapofika uendako. Ndivyo Ohayoda ilivyokuwa pasipo kujua kifutacho ni nini safari ikasonga na kwa kudra zake aliye juu tutafika tunakokusudia kufika

Kwa wiki kadhaa majukumu ya kijamii yamenifanya niwe mbali nanyi, ambao mmekuwa sehemu ya maisha yangu toka tuanze, Watu Ambao mliipokea Ohayoda kwa mikono yote miwili na ambao wanajivunia kuwepo kwa Ohayoda. Katika kipindi hiki siwezi kuficha nimewamisi sana, nimemisi kuandika makala za SINTOFAHAMU, SHUJAA WETU na habari mbalimbali zinazojiri toka huku kwetu japo huwa nakumbana na vikwazo mbalimbali vikwemo vitisho na kukatishwa tamaa kwa namna nyingi lakini "haturudi nyuma kamwe". Huwa najisikia furaha sana kuona wadau mbalimbali wanafuatilia kwa kina yote yanayojiri toka pande hizi. Nichukue fusa hii kuwajuliha kuwa bado kitambo kidogo tu Ohayoda itarudi kwa kasi na vitu vipya kabisa vilivyosheheni.

Kwa miaka mingi nimekuwa na ndoto ya kufanya kitu cha tofauti kwa jamii ambayo nimetokea, jamii ambayo imekulia na pengine bila hiyo jamii nisingefika hapa nilipo. Ni kama sehemu ya shukrani yangu kwa jamii na pengine ndiyo maana hata Ohayoda toka imeanza ni kazi ya kujitolea na hata sasa niandikapo majira ya saa tano na nusu usiku baada ya purukushani za kutwa nzima, bado nina mzigo wa kufikisha ujumbe kwa njia hii.

Pengine msukumo mkubwa zaidi wa haya yote umetokana na mtu moja ambaye kwa sehemu kubwa sana amenifanya niwe hivi nilivyo leo hii, ambaye siku zote za uhai wake alifanya mambo mengi ambayo jamii pengine hata haiyatambui na yawezekana haitapata fursa ya kuyatambua, na pia yapo  mengi sana ambayo hakuweza kuyakamilisha katika uhai wake au kuyashuhudia yakikamilika wakati wa uhai wake. Kwa yale yote ambayo hakukamilisha, japo viatu vyake ni vikubwa mno ila kwa kadiri ya Mungu anavyonijalia najitahidi kuyakamilisha. Si kwa nguvu wala uwezo!

Kama nilivyosema awali, ni kweli nimeadimika katika siku mbili tatu zilizopita kiasi cha kushindwa kuwaletea habari, makala na matukio mbalimbali kama hapo awali lakini namshukuru Mungu kwani katika kipindi hiki nilikuwa jikoni napika Tamasha la kwanza kabisa kufanyika katika ukanda huu, tamasha ambalo siyo tu litatangaza ukanda huu ambao una urithi mkubwa wa utamaduni na Maliasili kedekede lakini umesahaulika hata kwa wadau ambao wametokea huku. Juzi niliwaza jinsi ukanda huu unavyoongoza kwa kutoa viongozi mashuhuri nchini lakini sina uhakika kama wanafanya yakutosha kuleta maendeleo huku.

Katika kipindi hiki nimekuwa nikitafuta washiriki pamoja na wadhamini kwa ajili ya Tamasha hili ikiwa ni pamoja na kuweka mchakato mzima katika mustakabali mzuri. Lengo ni kuwa tamasha hili lijiendeshe lenyewe bila kutegemea fedha kutoka kwa wahisani hasa wa nje kama ilivyozoeleka, tuoneshe kuwa hata sisi tunaweza na si lazima tutembeze bakuli hata kwa yale yaliyo katika uwezo wetu japo Si jambo rahisi sana kwani linafanyika kwa mara ya kwanza tena huku Haydom lakini kwa niaba ya timu nzima ya 4CCP nawashukuru sana Norwegian Church Aid, Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Manyara, Halmashauri za Wilaya za Mbulu, Mkalama/Iramba na Hanang, kampuni ya nishati ya jua ya Ensol Energy (T) Ltd kwa kukubali kuwa wadhamini wa shughuli hii, Best Food Market chini Isaac Awaki na Emmanuel Nuwas, Hospitali ya Kilutheri ya Haydom,Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Tarangire National Park, Bodi ya Utalii Tanzania kupitia Tanzania Cultural Tourism Programme, Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, na Goig Society, Haydom Vocational Training and Entrepreneurship Center,  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Manyara, Benki ya NMB tawi la Mbulu, Art in Tanzania, Taasisi ya Damu Salama, Mama Duncan wa Katesh, Garage ya HLH, Ofisi za vijiji hasa Haydom na Ng'wandakw, Ofisi ya Kata Haydom hasa Afisa Mtendaji wa Kata ndugu Damian Isaay, Kituo cha Polisi Haydom na wengineo ambao wameunga mkono jitihada hizi ambazo siyo tu yataukuza utamaduni wetu bali pia yatatangaza fursa mbalimbali huko duniani n kuvutia uwekezaji katika ukanda huu.

Bado hatujafikia siku ya ufunguzi wa tamasha na bado tunawakaribisha wadau mbalimbali ambao pamoja na majukumu waliyonayo wameamua kuja kutuunga mkono; Shukrani za pekee kwa Madaraka Nyerere kwa kuamua kuja kutoka Butiama hadi Haydom, Saphy na Dorothea kutoka Dar es Salaam, Adam Mayo, Augustino Namfua na Samuel kutoka Jambo Festivals Arusha, Felix na Peter wa Mpesa Babati. Lakini shukrani za dhati kwa Samuel Mshashi na Dr. Nuwas kwa kuitikia wito na kwa ushirikiano wa hali ya juu, komredi Nelson aka mekuu na wadau woooote ambao mara kadhaa tulipoonekana kukata tamaa walitunyanyua na kutupa nguvu ya kuendelea.

Pia niwashukuru wale wote walioonesha nia ya kushiriki lakini kutokana na sababu mbalimbali mwaka huu wameshindwa lakini wameahidi mwaka ujao watakwepo hasa SIMGAS na wengineo....Pengine watakwepo wengi zaidi wa kuwashukuru mara baada ya tamasha hili, lakini ningependa uchukua fursa hii kuwakaribisha watu woote wanaokaa maeneo ya Haydom na maeneo yaliyojirani kuanzia Karatu, Mbulu, Babati, Katesh, Basotu, Dongobesh, Kiomboi, Nduguti, Singida, Ilongero, Dareda hadi Meatu. Karibu uwe sehemu ya Historia hii muhimu sana.

Kwa ufupi tu, kutakuwa na maonesho na mashindano ya ngoma za asili kutoka makabila ya Wairaqw, Wanyiramba, Wanyisanzu, Wahadzabe na Wadatooga ambapo mshindi wa kwanza atajipatia TSH 100,000/=, wa pili 75,000/- na ngoma ya tatu ni 50,000/=. Pia kutakuwa na mashindano ya riadha ya KM 2 kwa wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 45 na mshindi wa kwanza atapata 50,000/=, wa pili 30,000/= na wa tatu 20,000/= ambazo zitaanzia uwanja wa CCM Haydom hadi Kituo cha Utamaduni Haydom na kwa vijana wa chini ya miaka 45 zawadi ni 50,000/=, wa pili 30,000/= na wa tatu 20,000/= zitakazoanzia kibao cha Harar hadi kwenye viwanja vya kituo cha Utamaduni.

Aidha, Mwalimu Nelson Faustine na Mwalimu Isaac Ara watatoa mafundisho ya kuwatia hamasa wanafunzi hasa wa shule za sekondari (Inspirational Talks) ya jinsi ya kujiwekea malengo ya kitaaluma na kimaisha na Taasisi ya Damu Salama itakuwa inaendesha zoezi la kuchangia damu kwa hiari kwa ajili ya benki ya damu ya Taifa na pia kwa ajili ya HLH. Wananchi wanaombwa kujitokeza kwa uwingi sana katika siku hizo tatu.

Kwa niaba ya timu nzima ya 4CCP niwakaribishe tena wote katika viwanja vya Kituo cha Utamaduni Haydom kuja kujionea mambo mbalimbali na upate kujifunza mengi zaidi ambayo yatakubali mtazamo wako.

NIPO KWA SABABU UPO.................I AM BECAUSE YOU ARE!


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda