Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Tuesday, July 31, 2012

Kutoka Ukerewe hadi Iramba: Historia, Maisha na Tabia za Wanyiramba na Wanyisanzu.....Sehemu ya Tatu

Na Amani Paul, Mwangeza
Kama tulivyoona katika makala mbili za awali kuhusu Historia, Maisha na Tabia za Wanyiramba na Wanyisanzu, leo tunaendelea na sehemu nyingine ambayo tutaangazia Mavazi na matambiko katika jamii hizi ambazo zinapatikana huku kwetu. Yapo mengi ya kujifunza na ambayo sisi tunajivunia kuwa na utajiri mkubwa wa utamaduni.

MAVAZI NA MAPAMBO
 • Kabla ya wakoloni kuja, wanyiramba na wanyisanzu walivaa mavazi ya ngozi za wanyama ambapo wanaume walivaa kama lubega na wanawake kujifunga kiunoni na sehemu ya mbele hufungwa shanga nyingi zilizoshonwa kwa ustadi ili kuficha utupu. Ngozi hizo hushonwa kwa uzi wa miti ya mwandu au migumo, ngozi ya mbuzi ilitosha vazi la mtu mzima.
 • Katika kujipamba husuka nywele nyuzi ndogondogo na kuweka shanga, kutoga masikio juu na chini na kuweka mpini na kisha kuninginiza ushanga
 • Kuweka chale usoni alama ya mshale au alama ya =
 • Wanachonga meno ya juu alama ya V inayoelekea chini
 • Wanavaa shanga shingoni, kiunoni, mikononi na miguuni.
 • Kwa viatu walikuwa wanatumia ngozi ya ng'ombe dume hasa sehemu ya chini ya shingo maarufu kama dagala
 • Wanaume hutembea na fimbo, upinde, mkuki, visu na sime
MATAMBIKO
Wanyiramba na Wanyisanzu wanathamini sana matambiko. Kuna matambiko ya mtu binafsi, familia, ukoo au jamii nzima. Kwa ajili ya matambiko, hutumia ng├Žombe mweusi aliyezaliwa usiku, mbuzi mweupe, kondoo mweusi, pombe na hori
Matambiko haya hufanyika kwenye mapango na makaburi na huwa kuna maeneo maalum ya kufanyia matambiko hasa kule Mwandu kwa Wanyiramba na kwa Wanyisanzu hufanyia matambiko yao kule Kirumi.

Wanyiramba na Wanyisanzu ni watumiaji wazuri w tumbaku hasa ugoro.

Pamoja na hayo niliyoyaeleza hapo juu, Wanyiramba na Wanyisanzu wamepoteza utamaduni wao kwa kiasi kikubwa sana hasa kutokana na mabadiliko ya maisha. Mambo mengi yamebadilika mfano
 • Lugha ya Kiswahili kuzimeza Kinyiramba na Kinyisanzu
 • Dini (Ukristo na Uislamu) umefanya mambo ya matamiko yatoweke
 • Miiko mbalimbali imepuuzwa na kupingwa
UMILIKI WA MALI KATIKA
Ikumbukwe kuwa pamoja na kuwa Wanyiramba na Wanyisanzu wanahistoria inayofanana na tamaduni zao ni karibu sawa, lakini wanyisanzu wanautofauti pengine tofauti hii inawafanya wawe wa pekee zaidi yaani wanawake wananguvu zaidi ya wanaume (Matrilinear society). Kuna mali zinazomilikiwa na wanaume, wanawake, ukoo na jamii nzima.

 1. Mali zinazomilikiwa na Wanaume : Mifugo yote, mazao yote, zana za vita, mashamba na ardhi, watoto na kupokea mahari
 2. Mali zinazomilikiwa na wanawake: Vyombo vyote vya mapishi na vifaa vya kutayarisha mapishi na vyakula vyote vilivyopikwa
 3. Mali inayomilikiwa na Ukoo: Matambiko, ndoa, mirathi na usuluhishi wa migogoro
 4. Mali inayomilikiwa na jamii: Miti na maeneo ya matambiko na vyanzo vya maji
Wanyiramba na Wanyisanzu wanasema kuwa "uzao ni kwa baba lakini ukoo ni kwa mama" wakimaanisha kuwa mwanaume anapooa ni sharti ahamie na kuishi kwa wake zake. Wakwe hawa wanawajibika kuwatunza pamoja na watoto wao kwa kuwapa chakula, shamba la kulima lakini hana haki na mapato yatokanayo na shamba hilo na kujengewa nyumba. Mwanaume huyo anapofariki urithi huenda kwa mjomba wake. 
Siku hizi hali hii imebadilika kwa kiasi kikubwa na wanaume hawataki kwenda kuishi kwa wakwe ili kuondokana na dhana ya kuwa "ameolewa"

USHIRIKIANO NA JAMII NYINGINE
Wanyiramba na Wanyisanzu wamepakana na Wanyaturu kwa kusini, wasukuma upande wa magharibi, wahadzabe upande wa kaskazini na kwa upande wa mashariki wanapakana na Wairaqw na Wadatooga, ambao wamekuwa wakishirikiana katika nyanja mbalimbali kama ifuatavyo;
WANACHOPATA KUTOKA KWA
WANACHOTOA KWA
1. Wairaqw: Chakula, punda na ng’ombe
1. Wairaqw: Mtama, mikuki, visu, tumbaku na ushanga na vibarua (wafanyakazi)
2. Wanyaturu: Watumwa (atugwa) kama malipo ya uganga wa mvua
2. Wanyaturu: Mtama, mikuki, visu, tumbaku na uganga wa mvua
3. Wahdzabe: Asali, Nyama, madawa ya asili na kuoleana
3. Wahadzabe: mtama, ushanga, tumbaku na kuoleana
4. Wasukuma: ng’ombe, uganga na kuoleana
4, Wasukuma: Ardhi, kibarua (nguvu kazi) na kuoleana
5. Wadatooga: mafuta, maziwa, ng’ombe na punda
5. Wadatooga: Tumbaku, ardhi na vibarua


Mpenzi msomaji, ninaamini umeweza kujua kwa kiasi kikubwa kuhusu ndugu zetu hawa na yumkini ungependa kujua zaidi, kama una uswali, ushauri au maoni usisite kuwasiliana nasi. Nasi tutayafanyia kazi maoni yako au tutayajibu maswali yako hasa yanayohusu tamaduni za jamii mbalimbali.
Wasiliana nasi kwa kuacha maoni yako hapa chini au tuandikie barua pepe kupitia amanipaulit@gmail.com au nipigie kwa 0784238225!

Nikuache na utani wa huku Iramba kuwa "Iramba mukulu Tanzania kanino"

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda