Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, July 26, 2012

Kutoka Ukerewe hadi Iramba: Historia, Maisha na Tabia za Wanyiramba na Wanyisanzu.....Sehemu ya Kwanza

Na Amani Paul, Haydom
Uleyleani! Wajuzi wa hiyo salamu tayari wamekwisha kujibu "izaa uduu".
Katika siku zilizopita tumekuwa na mfululizo wa makala mbalimbali yanayotupa fursa kujua kuhusu Historia, Maisha na Tabia za makabila mbalimbali hususani huku kwetu katika mikoa ya Manyara, Singida, Arusha na Shinyanga pamoja na mikoa jirani na hii. Tuliweza kuangazia utamaduni wa Wairaqw na Wadatoga na leo tutamulika kuhusu Wanyiramba na Wanyisanza wanaopatikana katika wilaya ya Iramba (Sasa ni Iramba na Mkalama) mkoani Singida.....Kanyaga twende...
Kama zilivyo kwa jamii zingine za kibantu barani Afrika ambao walihamia Mashariki na Kusini mwa Afrika wakitokea Afrika Maghariki hususani nchi za Kameruni, Naijeria na Ghana wakipita misitu ya Kongo, Wanyiramba na Wanyisanzu walikuwa katika kundi mojawapo lililoelekea mashariki hadi maeneo ya Ziwa Nyanza (Victoria) hadi katika kisiwa cha Ukerewe kilichopo katika ziwa hilo kubwa zaidi barani Afrika. Japo haijulikani sababu hasa, kundi moja liliondoka kutoka katika kisiwa cha Ukerewe hadi Kisiwa cha Uzinza na kutoka hapo wakahama hadi maeneo ya Tabora ambako waligawanyiaka kundi moja likielekea kusini na inasemekana ndio waliokuja kuwa Wagogo na Wanyaturu huku kundi lingine likiendelea kuelekea Mashariki kupitia mlima Sekenke hadi Kisiriri.

Walipoanza kuitwa Wanyiramba na Wanyisanzu/Waihanzu
Wakaishi hapo Kisiriri kwa muda mrefu kabla ya kutokea ukame mkubwa sana uliosababisha njaa katika eneo hilo. Ili kukabiliana na tatizo hilo la njaa, watu hao walitumia mboa za majani za mlenda uliokaushwa zijulikanazo kama "ndalu" kama chakula kikuu. Kutokana na kula "ndalu" kwa mtindo wa kulamba, watu wa makabila mengine ya kibantu walivyowaona wakawaita "wenye kulamba" na baadaye likabadilika hadi kuwa "wenyilamba" hadi "Wanyiramba".
Ikumbukwe kuwa hadi hapo Wanyisanzu na Wanyiramba walikuwa kabila moja na wote walifahamika kama Wanyiramba baada ya njaa hiyo.

Wanyisanzu/Waihanzu wahamia pori la Mkalama
Kundi moja likaamua kuondoka hapo Kisiriri hadi pori la Mkalama wakiwa na mifugo yao na familia zao na walipofika katika pori hilo ili kujilinda na wanyama wakali wakajenga nyumba na kuzungushia maboma ya miba maarufu kama "masanzu/mahanzu". Baadaye baadhi ya Wanyiramba waliobaki Kisiriri nao waliamua kuondoka hapo na walipofika Mkalama wakawakuta wenzao wamezungushia nyumba zao kwa Maboma ya "masanzu/mahanzu"  ndipo walipoanza kuwaita hawa ni wanyisanzu au waihanzu.

Wanyiramba na Wanyisanzu japo wanahistoria inayofanana na kwa mtu mgeni anaweza kudhani kuwa hakuna tofauti baina yao, lakini ukweli ni kuwa kuna tofauti kubwa sana baina yao.

Koo zao na Wanapopatikana 
Wanyiramba
Hizi ni koo tano za Wanyiramba na wanapopatikana

  • Kinampanda: Wanaishi sehemu za milimani hasa huko Kinampanda
  • Anagimbu:     Wapo Iramba Mashariki
  • Waiambi/waiyambi: Wanaishi Nkungi na Iambi
  • Anishai: Wanapatikana Kinandili na
  • Akimbu: Hawa wapo mpakani mwa Iramba na Tabora
Kwa upande wa Wanyisanzu, wao wana Koo nne tu
  • Mnyakilumi: Wapo maeneo ya Kilumi/Kirumi
  • Mnyatumbili: Wanaishi Ikolo
  • Mnyadintima: Hawa wanapatikana Mwangeza na
  • Mnyasoha: Waishio Mkalama
Ndugu msomaji wa Ohayoda, yapo mengi sana usiyoyafahamu kuhusu makabila haya mawili yenye historia inayofanana na japo wanaishi pamoja na watu wengi kudhani ni kabila moja, wanatofauti kubwa sana hasa za tabia na mambo mengine kedekede. Katika Makala zijazo tutakujuza mengi hasa Lugha, Mofolojia/miili (Morphology), mavazi, tabia, miiko, matambiko, umiliki wa mali na chakula.

Usikose kufuatilia makala hii na zingine kuhusu mambo ya Utamaduni kila siku za Jumanne, Alhamisi na Jumamosi hapa hapa katika libeneke boooooora zaidi linalokujuza  habari kemkem hasa za jamii halisi za Kitanganyika.

Kama una maoni, maswali au ushauri usisite kuwasiliana nasi au kuacha maoni yako hapo chini nasi tutayafanyika kazi ili kuboresha jamvi letu hili liwe na manufaa kwa wote.

Songela saana!

2 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda