Katibu wa chama cha walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Singida Saidi Mselem akitoa nasaha zake kwenye mkutano wa kuhamasisha walimu kushiriki mgomo wa kuishinikiza serikali kuwalipa walimu stahili zao ikiwemo nyongeza ya asilimia 100 ya mshahara.Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya msingi Kiomboi.
Mwenyekiti wa CWT mkoa wa Singida,Aran Jumbe akizungumza kwenye mkutano maalum wa kuhamasishana kwa lengo la kuishinikiza serikali kilipa stahili za walimu,ikwemo nyongeza ya aslimia mia.Kushoto ni mwenyekiti wa CWT wilaya ya Iramba,Josephat Gunda na kulia ni mjumbe wa CWT mkoa wa Singida kwa upande wa walemavu,mwalimu John.
 Baadhi ya walimu waliohudhuria mkutano maalum wa kuhamasishana ushiriki wa mgomo unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao kwa ajili ya kuishinikiza serekali,kulipa madai yao ya msingi.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Kukiwa hakuna dalili zozote za madaktari mkoani Singida kuungana na wenzao katika kushiriki mgomo wenye lengo la kuishinikiza serikali kutimiza madai yao, walimu mkoani Singida wanaendelea na mikutano ya kuhamasishana kujiandaa kushiriki mgomo unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao.
Walimu mkoani Singida wameendelea kuhamasishana na kuondoana woga na wasi wasi, kupitia mikutano ambayo imekuwa ikiandaliwa na kuratibiwa na chama cha walimu Tanzania (CWT) mkoa.
Chama hicho kimewataka wanachama wake na walimu kwa ujumla kuwa tayari kushiriki mgomo iwapo serikali haitakuwa tayari kutekeleza maombi yao.
Madai yao kwa serikali ni pamoja na nyongeza ya mishahara kwa asilimia 100, posho ya kufundisha asilimia 55, walimu wa sayansi 50, walimu wa sanaa 30 na posho ya mazingira magumu asilimia 30.
Akizungumza na walimu wa wilaya ya Iramba,Mwenyekiti wa CWT mkoa wa Singida Aran Jumbe, amesema lengo la kuhamasisha ni kuunga mkono mgogoro dhidi ya serikali kwa lengo la kuishinikiza kulipa madai yao.
Amesema walimu wamekuwa wavumilivu sana, wakati wote wa kutekeleza majukumu yao ya kuelimisha jamii, bila kujali kutotekelezwa kwa madai yao kwa muda mrefu.
Akifafanua, Jumbe amesema serikali kwa muda mrefu imekuwa haitekelezi matakwa yao kwa vitendo, bali imeweka mbele nadharia tu.
Mwenyekiti huyo amesema kutokana na dharau hiyo ya serikali kwa walimu, baraza la taifa la walimu linatarajia kufanya kikao chake Julai 5 mwaka huu, kutoa maamuzi ya mgomo wa walimu nchi nzima, endapo serikali haitayafanyia kazi madai yao.
Jumbe amesema endapo mwanachama wa CWT au asiye mwanachama atajitenga na kuacha kushiriki mgomo huo, chama hicho kitamshughulikia kwa mujibu wa sheria.

Source: www.dewjiblog.com