Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, June 14, 2012

SINTOFAHAMU: 20% ya mapato ya Halmashauri yanayotakiwa kurejeshwa vijijini inaenda wapi?

Na mwandishi Maalum
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri (W) Mbulu ndugu Joseph Guulo Mandoo
Kwa mujibu wa sheria na taratibu, 20% ya mapato ya ndani ya halmashauri za wilaya nchini inatakiwa irudi moja kwa moja kwa vijiji husika ambako mapato hayo yamekusanywa. Mapato ya ndani ya halmashauri ni yale ambayo hayalipwi kwa TRA bali hulipwa kwa halmashauri husika mfano ushuru wa minada, masoko, leseni za biashara, ushuru wa mazao, mifugo n.k ambazo hukusanywa na halmashauri husika moja kwa moja. Lakini Sintofahamu ni kwa nini fedha hizo hazirudishwi vijijini kama inavyotakiwa bali zote huingia katika mfuko wa halmashauri.
Uchunguzi mdogo uliofanywa na ohayoda umebaini kuwa viongozi wengi wa vijiji hasa wenyeviti wa vijiji kutokuelewa au kutokufahamu kabisa juu ya uwepo wa utaratibu huu na wale wanaofahamu hasa maafisa watendaji wa vijiji huogopa kuuliza kwani wanaogopa kutia "mchanga kitumbua" chao kwa mwajiri wao ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri.
"Wenyeviti ndio wanapaswa kuwabana madiwani lakini hawafanyi hivyo, sisi watendaji tukijaribu kufuatilia unatishia kazi yako kwani unaweza ukahamishwa na kupelekwa vijiji vya pembezoni na pengine hata kufanyiwa fitna na kuondolewa katika kazi yako" alisema moja wa maafisa watendaji wa vijiji waliohudhuria semina ya PETS iliyokuwa na lengo la kuwawezesha wananchi kufuatilia matumizi ya fedha za umma kuanzia ngazi ya chini
Kutokurudishwa kwa fedha hizo vijijini kunawaongezea mzigo mkubwa wananchi wa vijijini ambapo pamoja na kodi mbalimbali wanazotozwa na TRA, halmashauri huwakamua fedha na bado shughuli za maendeleo za vijiji huwamaliza pumzi. Mwenyekiti wa kijiji cha Endaharghadatk ndugu Martini Akko alidai kuwa mzigo wa michango kwa wananchi wake ni mkubwa kwani japo halmashauri hukusanya ushuru mkubwa sana kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika hapo kijijini lakini hawafaidiki na chochote na bado wanachi wanamzigo mkubwa wa kuchangia ujenzi wa shule ya msingi, sekondari, zahanati na ofisi ya kijiji.
"Kijiji chetu kinamnada mkubwa sana unaofanyika mara 2 kwa mwezi ambapo halmashauri hukusanya zaidi ya shilingi milioni 2 kwa kila mnada lakini hatujawahi kupokea hata senti tano zaidi baada ya mnada wanatuachia uchafu na hawafanyi chochote kuboresha mazingira. Wakati Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) imetukabidhi huu mnada ilipendekeza kuwa 40% ya mapato yatokanayo na mnada yabaki katika serikali ya kijiji ili tuweze kufanyia majengo na miundombinu mbalimbali mnadani ukarafati lakini siyo 40% bali hata 20% haijawahi kutolewa, majengo na miundombinu inazidi kuharibika huku halmashauri ikiweka kipaumbele kukusanya ushuru tu." alisema Akko
"Sasa hivi kila kaya inachangia zaidi ya 80,000/= kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari (Mama Kari) tu na bado kuna ujenzi wa ofisi ya kijiji, zahanati, nyumba za walimu na gharama za kuendesha ofisi, kama tungekuwa tunapata hizo 20% wananchi wasingetwikwa mzigo mzito kiasi hiki"
Naye makamu mwenyekiti wa hakmashauri ya wilaya ya Mbulu ambaye pia ni diwani wa kata ya Dinamu ndugu Joseph Guulo Mandoo alisema kuwa ni kweli utaratibu huo upo lakini umekuwa hautekelezwi katika wilaya ya Mbulu na kuongeza kuwa "inategemea na ushapu wa diwani wako katika kufuatilia"
"Mimi huwa nawapeleka wenyeviti wa vijiji vya kata yangu katika vikao vya halmashauri na huwa nafuatilia haki za wananchi ninaowawakilisha" alisema diwani huyu machachari maarufu kwa jina la Guulo, jibu ambalo lilizua hisia tofauti miongoni mwa viongozi wa vijiji ambao waliwaona madiwani wao kama wasaliti na wasiofuatilia mambo.
Sintofahamu kwa nini fedha hizo hazirudishwi kama inavtotakiwa kwa mujibu wa taratibu ambazo zimewekwa. Wakati hali ikiwa mbaya vijijini, taarifa zinasema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 wilaya ya Mbulu ilipewa jumla ya shilingi Bilioni 19 lakini mpaka mwisho wa mwaka wa fedha shilingi bilioni 2 zilirudishwa hazina kwa kutokutumika. Sintofahanu inakuwaje serikali na hasa halmashauri kila kukicha inalia kuwa haina pesa wakati bilioni 2 katika wilaya moja zinashindwa kutumika. Sintofahamu kama kweli hata hizo walizotumia zimetumika inavyotakikana au hata hizo zilizobaki ni wamekosa namna ya kujichotea.
Kwa leo ni hayo tu, naamini sasa wahusika hasa viongozi wa vijiji na madiwani watalifuatilia kwa makini suala hili ili kuwapunguzia wananchi mzigo mzito wa umaskini unaowakabili.
"Haki huinua Taifa bali dhambi nia aibu kwa watu wake!"

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda