Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Wednesday, June 6, 2012

Mchungaji KKKT Endasak ampa kichapo Muumini

 •  Ni mwalimu wa Chekechea ya Kanisa

 • Ni baada ya kumchapa mtoto nyumbani

 • Amfukuza kazi na kumsimamisha kanisani

 • Mchungaji akiri "Kweli nilimchapa lakini kama mwanangu"

  Mchungaji Marko Shauri wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania Usharika wa Endasak, Dayosisi ya Mbulu ambaye pia ni mkuu wa jimbo la Hanang la kanisa hilo amedaiwa kumpa kipigo muumini wa kanisa hilo ambaye pia ni mwalimu wa shule ya chekechea iliyo chini ya kanisa hilo.Akiongea na Ohayoda, muumini huyo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe hewani alisema kuwa mnamo mwezi Aprili mwaka huu (baada ya pasaka) alimchapa mtoto wa kaka yake anayekaa naye nyumbani kwake huko Endasak baada ya kufanya makosa ya kawaida lakini akakiri kuwa mtoto huyo alikuwa ameumia mkono kabla ya tukio hilo na hivyo wakati anamchapa alimtonesha tena. Mwalimu huyo ambaye alikuwa akiongea huku machozi yakimtoka alisema kuwa baada ya tukio hilo, majirani zake wawili (majina yamehifadhiwa) walienda kumshitaki kwa mwenyekiti wa kitongoji ambaye alikuja na kumshambulia kisha kuchukua huyo mtoto na kumpeleka mahakamani ambapo taratibu zote za kisheria zilifuatwa na kulimaliza tatizo hilo.
  Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 32 mwenyeji wa kijiji cha Hayderer kata ya Maretadu wilayani Mbulu aliongeza kuwa majirani hao hawakuridhika kwani walienda hadi kwa mchungaji na kumweleza tukio hilo na ambaye aliamua kumsimamisha kazi tarehe 21 Aprili 2012 na kisha kumsimamisha kanisani tarehe 13 Mei mwaka huu
  Alizindi kuongeza kuwa baada ya kusimamishwa kazi alirudi nyumbani Hayderer na kumaliza tatizo hili kifamilia kwani kaka (baba wa mtoto) alikiri kuwa mtoto huyo mwenye miaka 5 alikuwa amevunjika mkono kabla hajaenda kuishi na shangazi yake mwezi Januari mwaka huu na kuwa hakuwa amepona vizuri na kama familia walimaliza hilo suala, lakini aliporudi Endasak wale majirani zake waliendelea kumsakama na kumtaka aondoke hapo na kuongeza kuwa walienda tena kwa mwenyekiti wa kitongoji amwondoe lakini mwenyekiti huyo hakuona kosa lake hivyo kutokutekeleza matakwa yao na hivyo kurudi kwa mchungaji ambaye alimsimamisha huduma zote kanisani tarehe 13 Mei 2012.
  Apewa kichapo na Mchungaji
  "Siku ya jumamosi tarehe 2 June 2012 nilikwepo kwenye semina ya waimbaji kanisani, mchungaji akanitoa hapo na kunichapa vibao kisha kunipeleka kwake na kunifungia ndani na kunipiga akitumia mkanda wa suruali" alisema
  Aliongeza kuwa anashindwa kuelewa kwa nini mchungaji huyo apeleke mambo ya kifamilia hadi kazini na hata kanisani, kwani ni wazazi wangapi wanawachapa watoto wao?
  Aidha alizidi kubainisha kuwa majirani hao wamekuwa wakimwandama kwa sababu ya kumwonea wivu kutokana na kazi anayoifanya na pia mwenye nyumba wanayoishi kumpa chumba kikubwa jambo ambalo liliwachukiza kwa kuwa wao wanafamilia kubwa na hatimaye kuamua kumchomea kwa Mchungaji, ambaye pasipo kufanya uchunguzi wa kina aliamua "kumkatili"
  "Huu ukatili inabidi utokomezwa hasa dhidi ya wanawake" alisema mwalimu huyo
  Alipoulizwa kama yupo tayari kurudi kazini alisema kuwa "hata kama nimedhalilishwa nipo tayari kurudi kazini lakini pia kama hawataki haina shida kwani nitapata kazi kwingine" na kuongeza kuwa hakutaka kwenda polisi baada ya kupigwa ili asimdhalilishe mchungaji huyo

  Mchungaji aongea na Ohayoda

  Ohayoda ilimtafuta mchungaji Marko Shauri kwa njia ya simu ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo
  "Ni kweli hayo yalitokea na nilimchapa kama mwanangu baada ya kukaidi agizo la "kusimamishwa kanisani" na kudharau kwani pamoja na kusimamishwa aliendelea kuja kanisani na kuendelea na shughuli, na hata katika semina hiyo alikuwa anaimbisha mapambio"
  Ohayoda ilipomwuliza kuwa kama makosa aliyoyafanya yanastahili kusimamishwa kazi ikizingatiwa kuwa hayajatokea katika eneo la kazi alijibu kwa kifupi kuwa "kama kanisa ulitaka ningefanyeje? Hii shule si yake ni ya kanisa na ameonesha dharau hata baada ya kusimamishwa"  Na alipoulizwa kama mwalimu huyo amesimamishwa kazi na uumini kwa kosa la kumchapa huyo mtoto kaka yake inakuwaje tena na yeye amchape huyo dada na kutenda kosa hilo hilo analomhukumu alijibu kuwa "nilichapa kwa kunionesha madharau na mimi kama baba sikuwa na la kufanya zaidi ya kumchapa" jibu ambalo linazua mjadala kwani ni sawa na "kukomalia" kibanzi kilichopo kwenye jicho la mwenzio wakati wewe unaboriti kwenye jicho lako kama alivyosema Yesu.
  Aidha Ohayoda ilipotaka kujua kama kweli alimfungia ndani na kumpiga kwa kutumia mkanda, alikaa kimya na kisha kukata simu.
  Naye msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mbulu (KKKT) Mchungaji Nsanganzelu alipoulizwa na ohayoda kwa njia ya simu alisema yupo safarini Dodoma toka wiki iliyopita na kuwa hajapata taarifa zozote kuhusu tukio hilo
  "Nipo safarini Dodoma sijapata hizo habari labda umtafute Askofu au katibu Mkuu" alisema mchungaji Nsanganzelu huku akionesha kushangazwa na tukio hilo.
  Yawezekana matukio kama haya ni mengi sana katika maeneo mengi hasa vijijini ambapo viongozi wengi hasa wa dini kujichukulia sheria na kuwapa vipigo waumini wao au watu wanaowaongoza kinyume cha sheria na habari hizi hazisikiki kutokana na kufumbiwa macho na jamii na waathirika hao kutokujua haki zao. Suala la huyu dada lilishafika katika vyombo vya sheria na kupatiwa ufumbuzi na kitendo cha mchungaji huyu kumshambulia ni kosa la jinai na lafaa kukemewa kwa nguvu zote kwani ni unyanyasaji wa kijinsia na haiyumkiniki kama angekuwa mwanaume kama angempiga!
  Ohayoda inatoa wito kwa vyombo vyote husika (kanisa hilo na serikali) kuchukua hatua stahili kwani hata taratibu za kisheria hazikufuatwa kumsimamisha kazi kwa mambo ya kifamilia hata kama shule hiyo ni ya kanisa na inaendeshwa kwa taratibu za kanisa lakini hakuna aliyejuu ya sheria hata kama ni kanisa.
  Aidha tunaomba vyombo husika na taasisi zinazojihusisha na maswala ya kijamii hasa haki za wanawake kumpatia dada hyu msaada wa kisheria kwani inawezekana kafukuzwa kazi bila kupewa haki zake kama mwajiriwa na haijuilkani kama atazipa na pia Uongozi wa Kanisa uchukue hatua zinazostahili na kunusuru taswira ya kanisa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda