Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Tuesday, June 19, 2012

Bung`eda: Mazishi ya Kidatoga yanayochukua hadi miezi tisa

Buneida! Gibeseiyuu!
Niliahidi kuwaletea mambo mbalimbali ya jamii ya Wadatooga ambapo katika makala mbili za awali tuliangalia historia yao kama jamii na kisha ndoa za kidatooga zinakuwaje. Leo tunaendea na sehemu ya tatu ambapo tutaangalia shughuli nzima za mazishi ya jamii hii ya kinailotiki inayopatikana katika ukanda wa juu wa kaskazini wa Tanzania!
Bung`eda kwa kifupi linamaanisha Kaburi na kaburi huwa la mviringo tofauti na makaburi ya jamii zingine.

Bung`eda ni mazishi ya heshima sana na lazima iandaliwe na watoto wa kiume wa marehemu ambao huwaalika watu (ndugu) mbali mbali katika mchakato mzima unaochukua miezi takribani 9 ambayo ni sawa na muda wa kubeba mimba kwa mwanamke hadi kujifungua na katika mwezi wa mwisho ndugu hao huanza kuwasili katika nyumba ya marehemu na kuanza kujenga nyumba watakazoishi katika kipindi hicho kulingana na ukubwa wa familia husika na wageni walionao.
Ikumbukwe kuwa, ndugu hutoka sehemu mbalimbali na kila familia iliyoalikwa huja na kujitegemea kwa chakula chao na ndugu waliowaalika wao, yaani msosi unakwepo kwa waalikwa tu tena katika nyumba za familia zilizowaalika tu.

Kuna aina mbili za bung`eda

 1. Bung`eda isiyo na mwendelezo: Baada ya mtu kufariki anazikwa na hakuna shughuli zozote zinazoendelea baada ya hapo. Haya ni kama mazishi ya kawaida  na hufanywa kwa mtu yeyote na wa jinsia yeyote
 2. Bung`eda yenye muendelezo: Baada ya marehemu kuzikwa kunakuwa na shughuli mbalimbali (kama sherehe) ambazo huchukua miezi tisa au zaidi na siku ya kuhitimisha ndipo hufanyika sherehe kubwa sana ambayo watu wengi huiita bung`eda.
Pamoja na aina hizo mbili za mazishi lakini bung`eda yenye muendelezo imekuwa ikichukuliwa kama bung`eda na hivyo tunapozungumzia bung`eda tutakuwa tunamaanisha bung`eda yenye muendelezo na huwa haibagui jinsia

SIFA ZA MTU KUFANYIWA BUNG`EDA
 • Awe na umri wa zaidi ya miaka 60 wakati anafariki (mwanaume au mwanamke)
 • Awe na uwezo wa mali (ng`ombe), kama wewe ni maskini ujue ukifa hautafanyiwa bung`eda
 • Awe na angalau mtoto moja wa kiume
 • Awe na mtoto wa kike ambaye ameolewa
MAMBO YANAYOZUIA MTU KUFANYIWA BUNG`EDA
 • Mikono yenye damu: Kama marehemu alishawahi kumwua mtu hawezi kufanyiwa bung`eda
 • Kama marehemu alishawahi kuhara damu, (bung`eda ataisikia kwa marehemu wenzake teh teh)
 • Kama hana watoto
 • Kama ni maskini yaani hana mali (Ng`ombe)
 • Kama marehemu alishawahi kuwapiga wazazi wake
 • Endapo watoto wa kiume wa marehemu watakataa kufanya bung`eda
Marehemu anapofariki inapobainika kuwa atafanyiwa bung`eda hufungwa kwa kukalishwa kwa takribani siku 2 ili aweze kuzikwa vizuri kwa kukalishwa na ndipo kaburi lake huanza kujengewa hatua kwa hatua huku wakiweka tundu kwa nyuma (upande alikoegemea alipokalishwa) kwa ajili ya "kumlisha" marehemu kwa kumpelekea maziwa, tumbaku, asali n.k.
Wakati huohuo, sehemu inachagualia ambapo majani (lelechanda) hupandwa yakiwa yanawakilisha nywele za huyo anayefanyiwa bung`eda na siku ya mwisho hupandishwa juu ya bung`eda na kuwekwa hapo. 
Katika kipindi chocte hicho cha miezi tisa, mambo mbalimbali hufanyika na katika kila hatua idadi ya watu huongezeka na hadi siky ya kilele idadi ya watu huweza kufikia hata watu 20,000 ambao hutoka sehemu mbalimbali na katika miaka ya karibuni bung`eda imevutia wadatooga wengine ambao hawajaalikwa huhudhuria na kujigharimikia chakula na pia watu kutoka makabila ya jirani hasa Wairaqw nao hawakosi kujichanganya humo na kufanya shughuli hiyo kuwa ya aina yake.
Hatua za bung`eda
 1. Mulgwega Madeda: Kuweka magogo ya kwanza, baada ya marehemu kuzikwa, miti (magogo) yenye urefu wa futi mbili husimika katika duara dogo katikati ya kaburi na kisha kufukiwa
 2. Mulgwegaba Iyenya: Magogo ya pili yenye urefu wa futi tatu huwekwa kuzunguka yale ya awali na kisha kufukiwa
 3. Eshta Bung`eda: Katika hatua hii pombe ya asali (gesuda) inaandaliwa na kisha bung`eda hukandikwa na kusilibwa (neno la kidatooga Eshta linaama ya kupaka yaani kupaka bung`eda)
 4. Geng`andita: Hatua hii ni kuweka harufu nzuri kwenye bung`eda kwa kuandaa pombe tu, hakuna chochote kinachofanyika kwenye bung`eda zaidi ya kunywa pombe na kuimba
 5. Rarischota: Kuweka miti mirefu zaidi na kukandika, urefu wa miti unategemea jinsia, ya mwanaume huwa mirefu zaidi ya mwanamke
 6. Ghedawu: Hii ni hatua ya mwisho kabisa ambapo siku ya kilele, majani (lelechanda) hupandishwa juu/kileleni mwa bung`eda na watoto wa kiume wa marehemu
Katika kipindi chote hicho cha miezi tisa au zaidi, marehemu hupewa maziwa kila siku na pia wageni au ndugu wengine huleta tumbaku na asali kupitia tundu maalum.
Baada ya siku ya mwisho, hilo boma linaachwa (wanahama na kuacha hame) hapo na hakuna mtu anayeruhusiwa kujenga wala kukata miti katika eneo linalofikia kipenyo cha mita 100 ndani ya eneo hilo.

1 comment:

 1. Hili ni kabila langu (Wamang'ati). Asante sana Amani Paul Gaseri kwa kunifungua macho kwa mengi nisiyoyajua. Naona nimeshakuwa "foreigner" kwelikweli!

  SWALI KWA WANASOMAJI WA OHAYODA
  Je, kwa mwendo huu wa Bung'eda www.gongalimodel.org itaweza kutimiza malengo ya kuondoa umaskini by 2025?

  ReplyDelete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda