Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, May 3, 2012

SINTOFAHAMU-Kwa nini Mashamba ya Ngano ya NAFCO ya Hanang yalikufa?

"Kwetu ni pwani, nimezoea kuona bahari ya maji lakini leo nimeona bahari ya ngano"
Haya yalikuwa maneno ya rais mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania ndugu Alli Hassan Mwinyi alipotembelea mashamba ya ngano ya NAFCO wailayani Hanang katika miaka ya mwishoni ya 1980. Rais huyo mstaafu alijionea ukubwa wa mashamba hayo yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 70,000 alipotembezwa kwa kutumia ndege.
Mashamba ya ngano ya Hanang yalikuwa chini ya Shirika la Taifa la Chakula (NAFCO) yakifadhiliwa na shirika la misaada la misaada la Canada. Kwa zaidi ya miongo miwili mashamba haya yalikuwa na mafanikio sana kwani asilimia zaidi ya 90 ya ngano inayozalishwa nchini ilitoka Hanang wakitumia vifaa na teknolojia ya kisasa zaidi ya kilimo kwa wakati huo.
Mlima Hanang, Mlima wa tatu kwa urefu Tanzania, 3418m


Je nini hasa kilitokea mpaka mashamba haya yakafa katika miaka ya mwanzo ya 2000?
Ni hali ya SINTOFAHAMU kwa watu wengi na mengi yanasemwa na wadau mbalimbali. Kulikuwa na jumla ya mashamba 7 ambayo ni Mulbadaw, Setchet, Warreta, Basotu Plantation, Gawal, Murujanda na Gidagamowd yenye ukubwa wa hekta 10,0000 kila moja. Ohayoda ilipata kuongea na wadau mbalimbali kujua wanasemaje kuhusu mashamba haya kufa?

1. Mkumbo wa kufa kwa mashirika ya umma katika miaka ya 1990
Wapo wanaodai kuwa mashamba haya, kama yalivyomashirika mengine ya umma yalikufa kutokana na mabadiliko ya sera ya uchumi ya nchi kutoka ujamaa na kuingia ubepari. Serikali ilipunguza uwekezaji na ruzuku na hatimaye mashamba haya yakashindwa kujiendesha hatimaye kufa

2. Kuondoka kwa wa-Canada
Wakanada ndio waliokuwa waanzilishi na wafadhili wakuu wa mashamba haya wakitoa vifaa vya kisasa kabisa kama matrekta, greda, combine harvesters pamoja na kuwasomesha wataalamu wa kilimo kwenye vyuo vya nchini Canada. Mara baada ya muda wa mkataba wa ufadhili kwisha na walipoondoka, mashamba haya yalishindwa kusimama yenyewe na hatimaye kufa.

3. Mvua za El-Nino 1998
Baada ya Wakanada kuondoka na serikali kupunguza ruzuku, mashamba haya yalitegemea mauzo ya ngano wanayoivuna kwa kujiendesha kuanzia mishahara ya wafanyakazi, ununuzi wa vipuri, mafuta, ankara mbalimbali, mbolea na mbegu. Mvua za mwaka 1998 zilisababisha hasara kubwa sana na serikali haikuweza kutoa fidia au ruzuku kwa misimu iliyofuata na mashamba haya yakafa kifo cha kimya.

4. Uongozi Mbaya wa mameneja
Wadau wengi wanaamini kuwa katu haya mashamba yasingekufa kama si mameneja wa haya mashamba kugeuka mchwa na kutafuna fedha na rasilimali za mashamba. Katika miaka ya 1990 mameneja na wafanyakazi wa NAFCO walianza kujenga majumba katika mji wa Katesh na Arusha, wakiwasomesha watoto wao nje ya nchi. Kwa ujumla maisha ya wafanyakazi wa NAFCO katika kipindi cha uhai wa mashamba yalikuwa hayashabihiani na hali halisi ya maisha ya Watanzania walio wengi.
Inasemekana baada ya mkataba wa NAFCO na Wakanada kumalizika, mameneja hawa hawakutaka kuingia mkataba mpya wakidai kuwa wanauwezo wa kujiendesha wenyewe ilhali nia yao ni waweze kutafuna mali za shirika kwa uhuru pasipo kuingiliwa.


5. Siasa na uroho wa madaraka.
Habari zisizo rasmi zinasema kuwa, baadhi ya waliokuwa mameneja wa mashamba hayo (majina tumeyahifadhi) walianza kuingia kwenye siasa na kuonesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali kwenye chama tawala na hata kuingia bungeni. Yasemekana kuwa, uwezo wao mkubwa kifedha ulikuwa tishio kwa waliokuwepo madarakani kipindi hicho na ili kuwadhibiti, walishawishi mashamba kutokupewa ruzuku na fidia hasa baada ya kuathiriwa vibaya na mvua za El Nino.


6. Laana ya Wadatoga
Wakati wa uanzishaji wa mashamba haya, wananchi hasa jamii ya wafugaji wa kidatoga walihamishwa kwa nguvu na serikali pasipo kulipwa fidia wala kupewa maeneo mapya ya kuhamia. Baada ya mashamba kufa, wengi wanaamini kuwa ni laana ya kuwanyang`anya maeneo japo ukweli ni kuwa wadatoga huwa hawamiliki ardhi, wao huhamahama kutafuta malisho mapya kwa ajili ya mifugo yao. Suali linabaki kuwa, je kwa mashirika mengine ya umma yaliyokufa nayo yana laana gani? SINTOFAHAMU


Bado kuna Sintofahamu kuhusu mashamba ya NAFCO, mashamba yaliyokuwa yakitoa ajira kwa wananhi wengi na kuchochea maendeleo hasa ya mji wa Katesh ambao ulikua kwa kasi kipindi cha uhai wa mashamba hayo. Baada ya migogoro mingi, wananchi kuvamia mashamba hayo kwa kilimo na ufugaji hatimaye mashamba mawili ya Gawal na Gidagamowd yaligawiwa kwa wafugaji huku mengine matano yakibinafsishwa kwa wawekezaji binafsi ikiwepo shamba la Mulbadaw lililochini ya Haydom Lutheran Hospital(HLH)


SINTOFAHAMU!

1 comment:

  1. Katika sababu zote hizo zilizotajwa kufa kwa mradi wa NAFCO, namba moja ni laana ya Wadatooga, kama ilivyokuwa kuanguka kwa utawala wa makaburu ilikuwa ni laana ya Wazalendo. Laana za aina hiyo zimejengwa katika "resistance" (ukinzani) dhidi ya jambo lenyewe. Halafu si kweli kwamba Wadatooga hawamiliki ardhi. Wao ardhi humiliki kwa namna yao ya kimila jambo ambalo watawala na wavamizi wa ardhi ya Wadatooga ama hawalijui au hawataki kujifunza.

    ReplyDelete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda