Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Thursday, May 24, 2012

SINTOFAHAMU: Kwa nini Haydom haina shukrani?

 Nitasema kweli daima fitina kwangu ni mwiko-Moja ya Ahadi za Mwana TANU

SINTOFAHAMU leo inatimiza wiki ya tatu toka ianze kumulika mada mbalimbali zenye utata na zinazozua maswali mbalimbali katika jamii yetu, maswali ambayo hukosa majibu eidha kwa kuwa wahusika wanaotakiwa kuyajibu hawapo au wamekula "ganzi" au hajulikani nani wa kuyajibu yaani hakuna wa kuwajibika. Tulianza na kumulika kwa nini mashamba ya ngano ya NAFCO yalikufa kifo cha mende kisha tukaangazia uzandiki kama si uhayawani uliotumika katika kugawanya mkoa wa Arusha na kutoa mkoa wa Manyara. Leo kurunzi letu lipo Haydom, SINTOFAHAMU kwa nini Haydom haina shukrani?
Mama Kari alipowasili Haydom na watoto 4
na mumewe Dr Ole H. E Olsen 1961
Mwaka jana (2011) wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika (na miaka 50 ya mama Kari Tanzania?) ilibainika kuwa Mama Kari atarudi kwao Norway ifikapo mwezi Mei 2012. Wengi walishtushwa na mengi yamezungumzwa, yanazungumzwa na yataendelea kuzungumzwa kuhusu uamuzi wake wa kurudi kwao na kama kweli ni kwa mapenzi yake kurudi kwao Baada ya miaka 50 kuishi hapa nchini.
Sintofahamu, Mama Kari ameishi zaidi ya nusu ya maisha yake hapa Haydom, akiitumikia jamii kwa utumishi uliotukuka na sababu ambayo yeye mwenyewe alinipa nilipomwuliza kwa nini ameamua kurudi kwao, japo kwake na ndio ukweli halisia kuwa Haydom ndo nyumbani kwake kwa miaka 50 haikuniridhisha, kulikuwa na mengi yamefichika nyuma ya majibu yake ukiangalia kwa jicho la tatu. Mama Kari alinieleza kuwa umri wake umesonga sana na hataki kuwa mzigo na watoto wake wapo mbali. Nilijiuliza maswali mengi sana, hata huko anakorudi bado watoto wake wapo mbali, wengine wapo Thailand, Saudia, Kenya na sehemu mbalimbali duniani na hatakuwa karibu na watoto wake, inamaana ataenda katika vituo vya kulelea wazee huko kwao. Je kama angebaki anakuwa mzigo kwa nani? Je ameona kuwa hathaminiwi tena na kuchukuliwa kama mzigo? Hapa alikuwa anaishi na kuhudumiwa na Theresia na Yutha ambao wameishi naye kwa zaidi ya miaka 20 na katu hawajawahi kuchoka kumhudumia, iweje ajihisi hivyo? Lazima kuna jambo! Sintofahamu!
Mama Kari ameondoka jana, kimya kimya kama alivyokuja Haydom, pengine kimya zaidi ya hata alivyofika tarehe 10 Desemba 1961 akiwa na furaha ya kuonana na wakwe zake na kuungana na mume wake akiwa na watoto wake wanne lakini ameondoka akiwa na peke yake tena katika umri wake mkubwa wa miaka 85. Zaidi ameambatana na dereva na Selina Sanka ambaye amemsindikiza hadi KIA, huku shughuli za kawaida za kila siku HLH zikiendelea kama vile ni upepo unapita tu, hata wafanyakazi waliofanya naye kazi, kwanza wote wamemkuta na wamekulia mikononi mwake wakiwa hawana habari. Hata kwenye mbao za matangazo (Notice Boards) HLH achilia mbali sehemu mbalimbali Haydom hakukuwa na taarifa yoyote kuhusu kuondoka huko....kweli Sintofahamu maana najua wananchi wengi wamenyimwa fursa ya kumshukuru hata kumpa tu mkono!
Juzi jioni nilipata bahati ya kufanya naye mahojiano, alikuwa mwenye huzuni sana kiasi kwamba sikutamani kushuhudia akiondoka na jana sikuthubutu kushuhudia akiondoka. Niliwaza mengi sana jinsi anavyojisikia kuondoka na kuacha nyuma kazi kubwa aliyoifanya maisha yake yote. Kila alipopita na kila siku Mama Kari haachi kusema kuwa Haydom ni muujiza unaoishi! Haydom is a miracle! Haydom ilikuwa pori, simba, chui na fisi ndio waliotawala na hakukuwa na tumaini la maisha pande hizi. Hapa nikajiuliza, hivi Haydom ingekuwaje kama Mama Kari angekataa kuungana na mume wake kuja kuishi Haydom? Ni mwanamke gani ambaye atayaacha maisha mazuri mjini achilia mbali ulaya, tena akiwa na waoto wanne na kuamua kwenda kuishi Afrika, ndiyo pori la Afrika ambako hakuna shule wala huduma zozote za jamii? Baada ya yote hayo anaondoka bila thamani wala kupata heshima inayostahili!
Haydom haina shukrani na kwa hili tumepotoka, wote tuliopo hapa, nasema woooooooote na mimi nikiwemo, tungekuwa wapi kama siyo Dr. Olsen na Mama Kari? Kupitia wao umeme ulifika Haydom kabla hata ya wilaya na mikoa mbalimbali hapa nchini, kabla ya Mbulu na Karatu, kupitia wao tukapata maji, kupitia wao barabara zikajengwa, shule, makanisa, hadi wakati wa njaa na hadi anaondoka misaada ya chakula imekuwa ikitolewa na zaidi ya yote WENGI WALISOMESHWA NA KUPATA ELIMU NA NAFASI ZINAZOWAPA KIBURI KUPITIA WAO! Sipati picha leo wangekuwa wapi kama siyo juhudi hasa za Mama Kari kutafuta wafadhili kuja kutusomeshea watu wetu, watu ambao baada ya yote wamekosa shukrani ama kweli shukrani ya punda ni mateke! Inauma sana na inasikitisha sana
Mama Kari alikuwa mfamasia wa HLH na pia alikuwa mhasibu, kazi zote alizifanya kwa moyo wakati kukiwa na uhaba wa wataalamu tena wafanyakazi hulipwa kwa siku, hakuwahi kuwa na housegirl na alikuwa na watoto sita wa kuwatunza, Sintofahamu katukosea nini kuondoka kimya vile!
Kwa zaidi ya mwezi sasa amekuwa akipita maeneo na kwa watu mbalimbali akiwaaga kwa ``Reja reja``, leo kaenda kuaga shule ya Mama Kari, kesho Tafsiri ya Biblia ya Kidatoga, mara yupo anawaaga Hazina, utasikia anawaaga wamama, jumapili hii yupo Harar anawaaga kanisani, chuo cha VETA, familia binafsi n.k.
kote huku wanaimba sifa za mama Kari, na kuwa bila mama Kari wasingekuwepo hapo walipo, siku zilivyozidi kwenda niliamini kabla hajaondoka labda angeagwa inavyostahili, kama shujaa huku watu wakilia, hapa nazungumzia Serikali, HLH, Dayosisi ya Mbulu(KKKT) na Jumuiya nzima ya Haydom lakini mpaka anaondoka ilifanyika hafla uchwara ya soda na biskuti tu huku akiambulia zawadi za khanga na ngoma! Serious! After all she did, kweli tunampa khanga? Atukumbuke kwa khanga?
Hapa ninajiuliza hivi siku akifa tutajitia unafiki upi kulia? Je nani atathubutu kwenda Norway kuhudhuria mazishi yake akipewa hiyo nafasi? Hatujamthamini akiwa hai tukiwa na nafasi, akifariki kwa nini tumthamini wakati hata kwa heri yenye heshima hatukumpa? Sintofahamu
Mwaka 2005 alikuja Mfalme wa Norway, alikuja Haydom hakwenda Dar bali alikuja Haydom! na kuwatunuku nishani ya kifalme (Knighthood) mama Kari na Dr. Olsen, hivi tunajua maana ya kuwa knighted? Na tunamjua mfalme sisi? Akaja Waziri Mkuu akawatunuku nishani ya kitaifa, viongozi lukuki wa serikali walikuwa hawakauki Haydom, wapo wapi leo? Hata wabunge wetu (Iramba, Mbulu na Hanang) hawamtambui wakati wapiga kura wao ndio wanaofaidika na juhudi zake? Hivi unaweza kukumbuka ni lini baada ya hapo kiongozi wa kitaifa amekuja tena Haydom? Kama siyo Jakaya kwenye kampeni? Inauma sana unajua!
Siku moja kabla ya kuondoka
Kila mtu anamapungufu yake na yawezekana alifanya makosa makubwa kiasi cha ``wahusika`` kuamua kumchinjia baharini nakumpotezea mazima, lakini kwa hili tumevuka mipaka ya ubinadamu, jamani hata kumwandalia usafiri wa ndege basi hadi Arusha imeshindikana? Na umri wake kusafiri na gari katika barabara zetu mbovu huku akiwa na safari nyingine ndefu ya zaidi ya saa 12 jamani inahitaji kuwa Professor wa Harvard University kulitambua hili? Sintofahamu na katu haitaniingia akilini
Najua wengi watanichukia kuyasema haya, potelea mbali lakini ujumbe umefika! Tunaweza kujitetea kuwa Dr. Olsen hatukupata nafasi ya kumuaga kwa heshima kwa sababu alienda kwa matibabu lakini kuondoka kwa mama Kari kulijulikana miezi sita kabla lakini hakukuwa na mtu yeyote ``hasa kwa wahusika`` wenye dhamana ya uongozi walioona kuwa yafaa kumuaga kwa heshima, tutakuwa na lipi la kujitetea, tunaye diwani tena anafanya kazi HLH, viongozi wa Kata, Halmashauri za wilaya ya Mbulu, Hanang na Babati wote kimya, au kwa sababu uchaguzi upo mbali? Kama kusoma hatuwezi basi hata picha hatuwezi kuzitambua?
Katika mahojiano yangu naye juzi jioni nilimwuliza kuwa anajisiaje kuondoka? Na je anadhani ameagwa inavyostahili? Alinijibu kuwa popote alipoenda ameguswa sana na mapenzi ya watu kwake na jinsi watu wanavyotambua mchango wake, anaondoka akiwa hana deni moyoni na ameutumikia wito aliokuja kuufanya huku Haydom. Lakini je angejisiaje kama jamii nzima ya Haydom, Serikali na HLH wangekuja pamoja kumuaga badala ya kuagwa kimafungu? Tena yeye ndiye aliyekuwa anaenda huko kuwaaga, japo zawadi ni zawadi lakini kote anakoenda hakuna jipya ni yaleyale ya khanga, khanga, khanga na vyeti! Sijui kama kweli amevibeba vyote maana ni vingi sana kutosha kwenye mizigo yake anayoruhusiwa kuwa nayo kwenye ndege.
Historia ni mwalimu mzuri sana ndugu zangu na huwa inatabia ya kujiandika yenyewe, japo sasa ameondoka kimya na kupita kama upepo, historia itamtambua kama shujaa hata kama hatutabaini sasa. Historia pia huwa inajirudia sana na sijui kwa nini hatujifunzi, mengi yalisemwa wakati Dr. Olsen alipofariki, wapo watu waliovuta pumzi ya ahueni lakini sasa hivi kila mtu anamkumbuka, neno laiti huja baadaye na ndicho kinachotokea maana kila kona ya Haydom (sizungumzii HLH tu bali hadi vijijini) imekuwa ``laiti kama Dr. Olsen angekuwa hai`` katika kila kitu iwe polisi, barabara, maji n.k! Kifuatacho kitakuwa laiti kama Mama Kari angekwepo tungeshakuwa na shule, tungeshapata walimu, kanisa letu lingekamilika, n.k Tujifunze kuenzi watu wanaofanya mambo mazuri katika jamii hasa tunapopata nafasi ya kufanya hivyo wakiwa hai.

Maji yashamwagika, ila huu ndiyo ukweli na utaendelea kuwa ukweli japo unauma, kweli itatuweka huru kama tukiamua kuukubali ukweli, ni vyema kuachana na unafiki na kuwa na moyo wa shukrani pale panapostahili. Tusisubiri kumsifia mtu anapokufa, sasa hivi yupo hai bado hatujachelewa.

But the truth is.....She didn't get the farewell she deserved! Hate me or love me.....muungwana atafikiri na kuyaweka kichwani kisha kuchukua hatua. Kwani wahenga walisema "Muungwana akikutwa uchi, huchutama" 


Mama Kari amefanya mahojiano marefu sana na Ohayoda juu ya maisha yake kabla ya kuja Haydom, changamoto za kujenga Haydom, kutunza familia na kazi, kifo cha mumewe na maisha yake baada ya kifo cha mume wake na hatimaye uamuzi wa kuondoka kurudi kwao ambako amefunguka na kueleza mengi usiyoyajua. Yatakujia hapa hapa!

3 comments:

 1. This comment has been removed by the author.

  ReplyDelete
 2. Ohayoda sina la kuongeza. Uliyosema ni kweli kabisa .... kuna watu hapo kazi ni kuangalia matumbo yao tu.
  To be completely honest mama Kari na familia yake wameijenga haydom kuliko hata serikali .. wafanyakazi wote wote wa ngazi ya juu ya HLH Shame on you ..... after everything this is how you say goodbye, very embarrassing .. you could do better than Khanga ...

  ReplyDelete
 3. It hearts, we need to repent, we did a terrible sin.

  ReplyDelete

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda