Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Wednesday, May 9, 2012

Shujaa Wetu: John Steven Akwari


Kila siku ya jumatano, Ohayoda itakuwa inakuletea mtu ambaye kwa namna moja au nyingine amefanya jambo la kukumbukwa na kuiletea jamii yetu na nchi kwa ujumla heshima. Wiki hii tutaangalia jinsi John Steven Akwari alivyofanya jambo la kukumbukwa daima katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Mexico City, Mexico mwaka 1968.

Akwari akimaliza mbio 1968 Mexico

Mara nyingi kama si zote ``mashujaa wa Olimpiki``ni wale waliotwaa medali katika mashindano haya magumu lakini John Steven Akwari aliyekuwa wa mwisho kumaliza mashindano ya marathon mwaka 1968 Mexico City katika mioyo ya mamilioni ya watu anakumbukwa kama shujaa ambapo mwaka 2008 katika mashindano ya Olimpiki ya Beijing nchini China miaka 40 baadaye, Akhwari aliteuliwa kuwa balozi wa heshima wa Olimpiki.                                                          

Katika mashindano hayo ya mwaka 1968, Akwari akiwa na umri wa miaka 30 akiiwakilisha Tanzania alikuwa mwanariadha wa mwisho (57) kumaliza mashindano kati ya 75 walioanza. Mshindi wa mashindano hayo Mamo Wolde wa Ethiopia alitumia saa 2:20:26 huku Akhwari akimaliza zaidi ya saa moja baadaye yaani alitumia saa 3:25:27 kukiwa na watazamaji wachache uwanjani na jua lilikwisha kuzama.
Awali wakati anaanza mbio hizo, Akwari alianguka na kupata majeraha kwenye goti ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya hewa ya Amerika ya kati kuwa tofauti na nyumbani. Wanariadha wenzake walimpita moja baada ya mwingine na hivyo kukatiza ndoto yake ya kuiletea Tanzania medali ya kwanza kabisa ya Olimpiki, lakini hakukata tamaa bali alinuia kumaliza hayo mashindano.
Akiwa amefungwa bandage mguuni huku akitokwa na damu, Akhwari alitokeza uwanjani saa moja baada ya mshindi kutangazwa, na kukiwa na watazamaji wachache na waandishi wa habari na giza likianza kuingia, uwanja ulizizima kuona Akhwari anachechemea akiwa na maumivu kuelekea mstari wa kumaliza mbio, wengi waliguswa baada ya kushuhudia tukio hilo.
Alipoulizwa na waandishi kwa nini aliendelea na mashindano baada ya kuumia, aliwajibu kwa utulivu jibu rahisi
``Nchi yangu haikunituma maili zaidi ya 5000 kuanza mbio, bali kuzimaliza``
Baada ya nashindano hayo, Akhwari alirudi katika maisha yake ya kawaida huku akiulizwa mara kwa mara kuhusu mashindano hayo, alijibu kwa utulivu pasipo kuchukulia kuwa ni jambo la aibu kuwa wa mwisho wala kutokushinda.
``Nilifanya kama wazazi wangu walivyonifundisha`` alisema Akwari akizungumza na Xiaoyu akiwa Beijing 2008 ``walinifundisha kuwa, ukianza jambo lolote, hakikisha unalikamilisha, vinginevyo usianze kabisa``
Mtengeneza filamu Bud Greenspan katika filamu ya ``Mexico Olympics Documentary Film`` alimwelezea Akhwari kama mtu wa mwisho kumaliza marathon kwa zaidi ya saa tatu, lakini kutokana na vikwazo katika vyombo vya habari enzi hizo, watu wachache hawakuweza kujua kuhusu Akhwari na kutambulika kama shujaa wakati huo.
Katika miaka iliyofuata, aliendelea na riadha na hata baada ya kustaafu aliamua kuwa kocha wa riadha kwa vijana wanaochipukia akiwarithisha uchu na mapenzi yake kwa mchezo wa riadha.
Akhwari akiwa Beijing China 2008
                                                    
Miaka 40 baadaye, wakati Akhwari na matukio ya Mexico City yamekwisha sahaulika, wanamuziki wa kichina You Hongming na Wang Pingjiu baada ya kuiona filamu hiyo, walitunga wimbo wa ``Hero`` yaani shujaa kwa ajili ya mashindano ya Olimpiki ya Beijing. Kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini China, Yang Lan aliguswa na wimbo huo alitoa fedha kwa ajili ya kutengeneza video ya wimbo huo na kumtafuta Akhwari, shujaa halisi wa wimbo huo awepo kwenye ``shooting`` ya video ya huo wimbo. Japo kulikuwa na baridi, alisisitiza kuvaa track suit nyepesi za riadha kipindi chote cha kupiga picha kwa ajili ya filamu hiyo na hata baada ya kumaliza shughuli hiyo, alionekana akikimbia na vijana wadogo akiamsha hisia na ari ya mashindano yaliyokuwa mbioni kuanza.
                                       
``Ni heshima kwangu kutunga na kuimba wimbo huu, zaidi ya kutoa heshima kwa Akhwari bali ni kusherehekea ubinadamu`` alisema You Hongming
``Alichokifanya Akhwari kinatufundisha mengi sana siyo tu katika mashindano ya marathon bali hata katika maisha yetu ya kila siku. Maisha ni kama marathon, haijalishi nini kimetokea au kinatokea hatuna sababu ya kukata tamaa`` You Honhming alieleza.
John Steven Akhwari alipoulizwa baada ya kusikiliza wimbo huo na kuona video yake, alishindwa kuzuia machozi yasimtoke akikumbuka yaliyotokea mwaka 1968
``Nimefurahi wametunga wimbo na kufanya habari zangu zifahamika nchini China kote na ulimwengu mzima na watu waweze kujua kuwa mimi ni shujaa`` alisema Akhwari

John Steven Akhwari aliyezaliwa Mbulu mwaka 1938 aliiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olimpiki ya Mexico City nchini Mexico na mwaka 1970 katika michuano ya Jumuiya ya Madola alimaliza katika nafasi ya Tano na kustaafu rasmi mwaka 1978. Baada ya kustaafu alikubali jina lake litumike katika kuanzisha ``John Akhwari Foundation`` kwa ajili ya kusaidia wanariadha wa Tanzania. Mwaka 2000 alialikwa katika mashindano ya Olimpiki ya Sydney Australia na mwaka 2008 akateuliwa kama balozi wa heshima wa Olimpiki nchini China!
                                   Bonya hapo kati kuona video ya Akhwari akimaliza mbio 1968

Akwari anatufundisha mengi sana na bado na hazina kubwa sana kwa taifa letu, vijana tunaweza kujifunza mengi sana toka kwake na pia juhudi zahitajika kuuenzi mchango wake hasa katika riadha nchini. Tusisubiri mpaka mtu awe marehemu ndipo tuutambue mchango wake. Akhwari aliweza na sisi tunaweza.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda