Kulitokea matukio yaliyofululizana ya utekaji lakini yaliyoamsha hisia za watu wengi ni kutekwa kwa gari la mizigo aina ya Scania mali ya Bwana Mathias Molam wa Haydom kwenye eneo la Qorong`ayda ambapo watekaji waliweka magogo na kulisababisha gari hilo kuanguka, lakini cha ajabu watekaji hao hawakuondoka na kitu chochote cha maana.
Wakati bado tukio hilo lingali masikioni mwa watu, gari la kubebea wagonjwa "Ambulance" la Hospitali ya Kilutheri Haydom lilitekwa likiwa linamgonjwa, lakini cha kushangaza kama si kustaajabisha ni kuwa watekaji waliishia kumpiga dereva tu bila kuchukua kitu chochote. Katika matukio yote haya hakuna gari wala kifaa cha gari lililochukuliwa na watekaji wake.
Pamoja na jitihada za polisi kuwasaka watuhumiwa kutokufanikiwa, lakini wananchi wakachachamaa kwa kuitisha mkutano wa jadi wa wananchi wa maeneo hasa eneo utekaji ulipofanyika. Baada ya mikutano mingi na watuhumiwa kutokupatikana, imebaki hatua moja tu, KUKATA RUFAA KWA MUNGU! Ndiyo, ni rufaa ambayo hawamwachii tu Mungu bali huchukua hatua na kufanya dua na kutoa laana kwa wahusika ambapo mpaka siku ya jumamosi tarehe 5 May 2012 kama hawatajitokeza itabidi itekelezwe.
Lakini je laana hii inatolewaje na humwathiri nani? Linapotokea jambo la uhalifu kama hili lautekaji magari hasa ya wagonjwa, ambalo linachukuliwa kama uuaji, mhusika huombwa kujitokeza na kama hatajitokeza basi yeyote anayejua chochote ambacho aidha linahusiana na tukio hilo moja kwa moja au kwa namna moja au nyingine anaombwa ajitokeze, yaani aliyeona, aliyesikia, aliyesema na hata aliyetenda. Kama usipojitokeza laana inakuhusu pia hata kama haujatenda.
Mengi yamejitokeza, vibaka wengi wamejitokeza na kukiri kuwa ni kweli wao ni wezi hasa wa simu na kukaba watu usiku lakini hawahusiki na utekaji na wala hawana taarifa. Suali kubwa ni kuwa kwa nini wanaogopa laana kuliko kitu chochote? Je ni kweli inafanya kazi?
Wazee husema nia ya laana ni kuirekebisha jamii na kuwafanya wahalifu wakiri, tofauti na laana zingine, anapotubu maswahibu humwondoka mhusika. Laana inapotolewa, hutamkwa maneno yanayoeleza mabaya yatakayompata mhalifu na mara zote yamewakuta wahusika na wasipotubu hufa vifo vibaya ndani ya muda fulani, na vifo hivyo hutajwa kwenye laana. Mara nyingi wanalaani kwa kusema mhusika apate ugonjwa wa kuhara damu, au afe kwa nateso n.k na ushuhuda wa wengi huonesha yote huwakumba na kuwaumbua wahusika.
Akiongea na Ohayoda, shuhuda moja ambaye hakutaka kutaja jina lake wale majina ya waliokubwa na maswahibu hayo ambao kiukweli wanafahamika na jamii yote, alitaja mfano wa watu waliohusika na mauaji ya mama moja aliyekuwa mfanyakazi wa hospitali ya haydom, ambao wahusika wote hata wale walioukalia ukweli kimya japo hawakutenda walikufa kwa kuhara damu sawasawa na laana ilivyotolewa. Shuhuda huyo akiungwa mkono na wadau wengine waliendelea kutolea mfano wa wahusika waliochoma moto nyumba moja katika kijiji cha Kidarafa wilayani Iramba, mkoa wa Singida na kuua ng`ombe wote waliokuwa ndani, wao pia walikufa kwa kuungua kwa moto katika mazingira tofauti.
Aidha ipo mifano mingi sana ya majanga yaliyowapata wakaidi au yanayoendelea kuwapata hao wakaidi, lakini wapo wanaokiri pale wanapoona cha moto na wazee hufanya dua na kuwaombea msamaha na kurudi katika maisha ya kawaida. Pia yapo matukio ambayo laana zimefanyika lakini imepita miaka zaidi ya mitano lakini bado haijajulikana kama madhara yamewapata wahusika au la!
Unaweza usiamini, lakini huo ndio ukweli, laana kama njia ya kukata rufaa inatumika sana huku kwetu. Wao huamini kuwa "Unaweza kumhonga hakimu, lakini Mungu hahongeki", na hata viongozi wa dini huheshimu sana maamuzi ya wazee.
(Nitakuletea mchakato mzima utakavyoenda siku ya jumamosi, endelea kunifuatilia, unaweza kuacha maswali au maoni yako hapa chini)
No comments:
Post a Comment