Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Tuesday, May 15, 2012

Amani Ward: Kituo pekee Nchini kinachowahudumia waathirika wa pombe na dawa za kulevya ...(Sehemu ya pili)

  • Wagonjwa wafurahia huduma 
  • Kuna ``wakurugenzi``, wafanyabiashara, Afisa Afya wilaya na wanafunzi
  • Waona 250,000/= wanayolipia ni kidogo kulingana na huduma wanayoipata
  • Washauri kituo kipanuliwe ili wengine wasaidike
Katika makala iliyopita tuliweza kuongea na mkuu wa kitengo au wodi ya Amani, ndugu Paulo Tango na kutueleza mambo mbalimbali kuhusu wodi hiyo inavyowasaidia waathirika wa pombe na madawa ya kulevya. Leo hii tunaendelea na shemu ya pili na ya mwisho ya makala haya kwa kuwaletea mahojiano yaliyofanyika baina ya Ohayoda na wagonjwa hao waliolazwa katika wodi hiyo....ennnnnndeleeeea!
Amani Ward ya HLH
Nilipofika Amani Ward nikiongozana na mkuu wa wodi hiyo ndugu Paulo Tango, sikutarajia kama wagonjwa hao wangenipa ushirikiano na kukubali kufanya mahojiano nao pengine kwa hofu au kujificha ``stigma`` kuwa wao ni waathirika wa pombe hivyo wangeona ni jambo la aibu lakini tofauti na matarajio yangu, wagonjwa wote (12) waliokuwepo wodini hapo walijitokeza na kushea stori zao ili kuwasaidia wengine.
Wagonjwa hao wanatoka sehemu mbalimbali nchini hasa Arusha (ikiwa na idadi kubwa zaidi), Dar es Salaam, Moshi, Karatu na Haydom wanaishi kwa ushirikiano mkubwa utadhani wamefahamiana kitambo kumbe wengine wana siku chache.
Malebo Trans akiwa na Tango
Hemedi Miraji maarufu kama ``Malebo trans`` kutoka Arusha alieleza kuwa alikuwa anatumia madawa ya kulevya hasa Cocaine, lakini tangu afike Amani Ward, hali yake imebadilika kabisa
``Nilikuwa nimekonda na sikuwa na hamu ya chakula kabisa, nilipofika hapa nililazwa kwenye wodi ya kawaida kabla ya kuletwa kwa siku tatu ili kutoa ``arosto`` niliyokuwa nayo mwilini, sasa hivi nina wiki tatu ninajisikia fresh, sina tena arosto na nimeanza kunenepa kama unavyoniona`` alieleza Malebo trans!
Naye Gift ambaye anatarajia kujiunga na chuo cha mahakama Lushoto baadaye mwaka huu alifunguka na kueleza kuwa alipata habari za Amani Ward baada ya ndugu yake kupata matibabu hapa na yeye kwa hiari yake alidhamiria kuacha kunywa pombe kwani inamrudisha nyuma kimaendeleo na inamshushia heshima yake katika jamii kwani yeye bado ni kijana mdogo. Pia alieleza kuwa zaidi ya kupona na ulevi amejifunza kuishi na watu.
``mwanzoni niliogopa nikidhani nitakutana na watu waliochoka na wakorofi (makauzu), na pia mazingira ya huku ni tofauti na Dar es Salaam nilikotokea, lakini nimejifunza kuishi nao vizuri na pia hata kufanya kazi kama usafi na hata mama yangu akisikia ninapiga deki atafurahi sana``
Gift na Erick wakifanya usafi

Wagonjwa wote walieleza kuwa siku za mwanzo huwa ngumu sana hasa wanapolazwa katika wodi za kawaida wakati wao walikuja wakiwa wazima na hawajichukulii kama wagonjwa, ambako hupimwa ili kujua kiwango cha sumu itokanayo na madhara ya pombe au dawa za kulevya na kisha kupewa dawa za kutoa hiyo sumu (detoxification) na kupewa dawa za kuongeza hamu ya chakula.
Saulo, mkazi wa Ng`wandakw ambaye ni mara yake ya pili kulazwa Amani ward, alieleza kuwa baada ya kutoka mara ya kwanza hakuwa na dhamira ya dhati ila baada ya kukaa na kutafakari kwa kina ameamua kabisa kuacha na ndio maana amerudi mwenyewe kwa ridhaa yake.
Pengine aliyenigusa zaidi ni Afisa Afya wa wilaya ya Karatu ndugu Nicodemu Malonange alisema kuwa alikuwa anafahamu kuhusu wodi hii, na kwa dhamira yake ya dhati akaamua kuchukua likizo kazini na kujilipia gharama za matibabu. Naye Yona Hosea ambaye anafanya kazi katika Hospitali ya Kilutheri ya Karatu alidai kuwa alikuja huku kwa ajili ya matibabu na hakujua kama angeletwa Amani Ward....``mwanzoni ilikuwa ngumu sana kukubali niliona nalazimishwa na mwajiri wangu, lakini sasa nawashukuru nimesaidika, sasa ninaendelea vizuri`` alieleza Yona ambaye alipoulizwa kama kweli akirudi ``mtaani`` ataepuka kurudia unywaji alisema kuwa ``vishawishi ni vingi na kazi nayofanya (Mortuary) inanifanya ninywe pombe, siwezi kusema kama nitarudia au la``
Tumeamua kuacha ulevi wa pombe na dawa

Sifa za Amani Ward zinafahamika hata kwa taasisi zingine na zimekuwa zikiwashauri wagonjwa (recommendation) waje Amani Ward, kama alivyofunguka Mishael Emmanuel, mhitimu wa chuo cha diplomasia cha Dar es Salaam mkazi wa Arusha
``Nililazwa Hospitali ya Mount Meru kwa matatizo ya Celebral Malaria lakini pia nilikuwa natumia pombe sana, nilishauriwa na daktari moja aitwaye Boni kuja Haydom, japo siku za mwanzo iliniwia vigumu kuweza kuyamudu mazingira na ile hali ya kulazwa kwa siku tatu lakini kwa kuwa nilidhamiria kuacha pombe nilikubaliana na hali halisi`` alieleza
Richard Pamphili ambaye ni dereva wa kampuni ya utalii ya Fun Safaris, alikubaliana na maelezo ya Mishaeli ya kudhamiria kuacha pombe na kuongeza kuwa suala la kuacha ulevi ni dhamira ya mtu ``unaweza kuacha pombe bila hata ya kuja Amani Ward`` Richard iliendelea kufunguka kuwa madereva wengi wa makampuni ya utalii huingia kwenye ulevi kwa kutumia vileo vikali wanavyopewa na wageni hao kama ofa na hata pombe inayoachwa na wageni, lakini pamoja na unywaji wake hajawahi kusababisha ajali toka alipokuwa makampuni ya Bakombi na TST kabla hajahamia Fun Safaris
Aidha Richard na Mishaeli walizidi kueleza kuwa wamejifinza mengi hasa masomo ya kuhusu pombe na madhara yake, na kuwa ulevi hautokani na ushirikina kama watu wengi wanavyoamini kuwa mtu ``kalogewa pombe`` ni tatizo la kijamii zaidi.
Nilipata fursa ya kuongea na Erick ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Adol Printing ya Dar es Salaam ambaye alisema kuwa alikuja huku akiambatana na mkewe ambao kwa pamoja walikubaliana aje Amani Ward ili aweze kuachana na ulevi.
Nao Joshua Shuma kutoka Moshi na Ernest Manaseh mwenyeji wa Arusha ambao ni wafanyabiashara walieleza kuwa wameamua kuacha ulevi wa pombe baada ya kubaini kuwa pombe haina faida yoyote zaidi ya kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

Wagonjwa hao walipendekeza kuwa kituo hicho ni kidogo kulingana na uhitaji kwani watu wengi zaidi wangependa kuja kupata matibabu hapo lakini kwa kuwa nafasi haitoshi inabidi kuweka foleni. Aidha walisema kuwa wanafurahia huduma sana chakula wanachokipata ni kizuri sana na wanakula milo mitano kwa siku tofauti na awali ambako hata mlo moja ulikuwa kwa taabu. Pia walisema kuwa hela wanayolipa yaani shilingi 250,000/= kwa muda wote wa matibabu (wiki sita) ni kidogo sana kulingana na huduma wanayoipata.

Ohayoda inapenda kutoa shukrani za pekee kwa wagonjwa wote kwa kutoa ushirikiano na kukubali kushea ``experience`` zao ili watu wengine wasaidike pia. Shukrani za pekee zimwendee Paulo Tango kwa kuturuhusu kufanya mahojiano naye binafsi na pia kuturuhusu kuongea na wagonjwa katika wodi yake pamoja na uongozi wa HLH kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Ohayoda.

Chonde chondeee.....Ulevi nooooomaaaaaaaa!

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda