Kweli

NANYI MTAIJUA KWELI.....NAYO KWELI ITAWAWEKA HURU....NANYI MTAKUWA HURU KWELI KWELI

Mbiu ya Jamii

Tangaza Biashara yako hapa...wasiliana nasi sasa kwa 0753038005

WELCOME TO HAYDOM CULTURAL FESTIVALS 2013

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA

NORWEGIAN CHURCH AID TANZANIA
PROUD PARTNERS OF HAYDOM FOUR CORNERS CULTURAL PROGRAMME (4CCP)

Saturday, May 12, 2012

Amani Ward: Kituo pekee Nchini kinachowahudumia waathirika wa pombe na dawa za kulevya ...(Sehemu ya kwanza)

  • Kinapokea wagonjwa toka ndani na nje ya nchi 
  • 250,000 kwa wiki sita kwa aijili ya matibabu, malazi na chakula
  • Wizara ya Afya ``waikaushia``
  • Wengi wamesaidika
Amani ward-Tumaini la waathirika wa pombe na dawa za kulevya

``Chonde chonde, ulevi noooomaaaa!``....tangazo hili linakujia kwa udhamini wa Wizara ya Afya na Jeshi la Polisi``
Hili ni tangazo la redio ambalo limekuwa likisikia mara kwa mara kupitia vituo mbalimbali vya redio nchini, tangazo hili limekuwa na mafanikio makubwa sana kufikia malengo yake kwani limewafikia watu wengi na kuupata ujumbe juu ya madhara ya pombe. Lakini suala la ulevi wa pombe wa kupindukia na utumiaji wa madawa ya kulevya unahitaji mkakati mpana zaidi kuliko wa kutumia matangazo ya redio. Kusema hivyo haimaanishi kuwa napingana na hilo tangazo, la hasha! ila najaribu kuangalia tatizo la ulevi kwa kutumia jicho la uhalisia zaidi.
Paulo Tango akitoa vipeperushi kwa wagonjwa kujisomea

Tuachane na hayo ya wizara na tangazo hilo, leo nilipata bahati ya kutembelea wodi ya Amani (Amani Ward) ya Haydom Lutheran Hospital ambacho kinahudumia wagonjwa walioathirika kutokana na ulevi uliopindukia wa pombe na matumizi ya dawa za kulevya. Kituo hiki au wodi hii ya Amani kama inavyotambulika na wengi, kilianzishwa baada ya utafiti kubaini kuwa kuna waathirika wengi sana wa ulevi wa pombe (alcohol abuse) katika mkoa wa manyara hususan Haydom. Kulingana na ripoti ya utafiti alioufanya Paulo Tango mwaka 2008 unaonesha kuwa eneo la Haydom pekee, 55% ya watu wenye umri kati ya miaka 20-40 walikuw waathirika wa ulevi wa kupindukia wa pombe.
Kituo hiki kilifunguliwa rasmi mwaka 2007 kwa msaada mkubwa wa Dr. Olav Espegren kabla hajawa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Tiba wa HLH na akiwa bado yupo Norway kikiwa na uwezo wa kupokea wagonjwa 12 tu.
Ohayoda ilipata fursa ya kuongea na Paulo Tango ambaye ni mkuu wa wodi ya Amani ili kujua mambo mbalimbali yanayohusu wodi hiyo ya pekee kabisa nchini;
Ohayoda: Mmepokea wagonjwa kutoka mikoa gani zaidi?
Tango: ``Kituo hiki toka kianzishwe kimesaidia wagonjwa (waathirika) wengi sana wa ulevi wa kupindukia hasa wa pombe na madawa ya kulevya. Tumekuwa tukipokea wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali nchini hasa kutoka Arusha, Dar es Salaam, Moshi, Mbeya, Dodoma, Shinyanga, Singida na Manyara. Pia tumepokea wagonjwa kutoka Kenya.
Ohayoda: Ni nini tofauti ya kituo hiki na vituo vingine nchini?
Tango: Wodi ya Amani ni kituo pekee nchini kinachowasaidia waathirika wa ulevi wa kupindukia wa pombe na dawa za kulevya. Vituo vinginge hujishughulisha na watu wenye matatizo ya akili ila sisi tunawasaidia waathirika ma matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya warudi kwenye hali yao ya kawaida
Ohayoda: Je matibabu huchukua muda gani?
Tango: Programu ya matibabu huchukua wiki sita, kwanza kabla hatujampokea mgonjwa na kumwingiza kwenye program hii, mgonjwa hufanyiwa vipimo ili kujua kiwango cha uathirika na kisha hulazwa kwa muda wa siku tatu kwenye wodi za kawaida ili kupewa dawa za kupunguza sumu itokanayo na pombe na dawa za kulevya (detoxification), na kisha huanza programu hii ya wiki sita.
Ohayoda: Wanapokuwa wodini, wagonjwa hufanya nini?
Tango: Kuanzia jumatatu hadi Ijumaa, kunakuwa na programu ya mafunzo ambapo wagonjwa hufundishwa madhara ya pombe na dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kupata muda wa kusoma vitabu mbalimbali vinavyohusu pombe na dawa za kulevya. Vile vile kunakuwa na mafunzo ya neno la Mungu, somo la hatua 12 za jinsi ya kuacha ulevi wa pombe na dawa za kulevya, ushauri nasaha kwa mgonjwa mojamoja na huduma za kichungaji (pastoral counselling) kwa anayehitaji. Siku za jumamosi ni siku ya usafi na kuruhusu ndugu na jamaa kuwatembelea wagonjwa kwa waliokaa wodini kwa zaidi ya wiki 3 na siku ya jumapili wagonjwa waliokaa wodini kwa zaidi ya wiki tatu huruhusiwa kwenda kanisani ila katika makundi.
Ohayoda: Je baada ya hizo wiki sita, kuna programu yoyote wanayoendelea nayo?
Tango: Baada ya kumaliza wiki sita, wahitimu hupewa cheti na kuendelea na matibabu akiwa nyumbani kwa muda wa wiki 11 zaidi.
Ohayoda: Je wanawake wangapi wamefika hapa kituoni na kupata matibabu?
Tango: Tumepokea wanawake 15 kati ya wagonjwa 209 toka mwaka 2008 na mwaka huu hatuna mgonjwa yeyote wa kike. Kumekuwa na ugumu wa wanawake kujitokeza kuja kupata matibabu na sababu haswa hazijulikani.
Ohayoda: Ni Masharti gani wagonjwa hupaswa kufuata wanapokuwa wodini?
Tango: Kwanza hawaruhusiwi kuwa na simu, fedha kiasi chochote wala redio binafsi. Pia hawaruhusiwi kutoka nje ya geti la wodi ispokuwa siku za jumamosi na jumapili kwa waliofikisha wiki 3 hapa wodini.

Ohayoda: Mgonjwa hulipa gharama kiasi gani kupata matibabu?
Tango: Mgonjwa hulipa shilingi laki mbili na elfu hamsini tu kwa wiki zote sita, ikiwa ni pamoja na malazi, chakula (milo mitano kwa siku) na matibabu. Kiasi hiki ni kidogo sana kulingana na gharama halisi, hivyo hospitali hugharimikia pia matibabu haya

Ohayoda: Kuna kampeni ya serikali kupitia Wizara ya Afya na Jeshi la Polisi, je mnapata msaada wowote toka kwa hizo taasisi au wanatambua mchango wenu?
Tango: Wizara ya Afya inafahamu kuhusu hii programu na tulijaribu kuwakaribisha waje kututembelea bila mafanikio, kituo hiki hugharimikiwa na Hospitali ya Kilutheri ya Haydom kwa asilimia 100%, na hao jamaa wa wizara badala ya kutu``support`` wao wanataka tuwalipe per diem kuja kututembelea.

Ohayoda: Ni changamoto gani mnakabiliana nazo katika utendaji kazi?
Tango: Zipo changamoto nyingi sana, kama uhaba wa wataalamu wa ushauri nasaha hasa katika matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya, uhaba wa vitendea kazi, ugumu wa ufuatiliaji wa wagonjwa wanapomaliza programu na ongezeko la wagonjwa kwani tunapata maombi mengi sana na tunauwezo wa kupokea wagonjwa 12 tu kwa wakati moja.
Ohayoda: Nini mipango ya baadaye ya kituo hiki?
Tango: Kwa sasa tupo kwenye mchakato wa kuwa na kiwanja cha michezo na pia kuongeza vitendea kazi.
Ohayoda: nashukuru sana kwa kunipa ushirikiano na nakutakia kazi njema
Tango: Asante na karibu sana
Aidha ohayoda ilifanikiwa pia kufanya mahojiano na wagonjwa mbalimbali wanaoendelea kupata matibabu katika wodi hii maalum kwa ajili ya kutibu madhara yanayosababishwa ba na matumizi mabaya ya pombe. Ungana nami katika sehemu inayofuata ya makala haya, hapa hapa.........
No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Ohayoda